Sunday, May 10, 2009


Watanzania bara kulipa

kodi ya ardhi Zanzibar


Watanzania wanaomiliki ardhi Zanzibar watalazimika kusajiliwa na kulipa kodi ya dola za Marekani 5,000 kila mwaka kwa hekta kwa vile kisheria hawana haki ya kumiliki ardhi visiwani humo.

Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Mohammed Hashim Ismail, alisema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana baada ya kuteuliwa kuwa wakala wa kusimamia na kukusanya kodi ya ardhi visiwani humo.

Uteuzi huo umefanywa na Waziri wa Maji, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, Machi mosi, mwaka huu. Alisema kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1992, ni Mzanzibari pekee ndiye mwenye mamlaka kisheria ya kumiliki ardhi na wageni wote wanapaswa kukodishwa na kulipia kodi kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Wazanzibari ndio wana haki ya kumiliki ardhi na watu ambao si Wazanzibari yaani wageni wanapaswa kukodishwa na kama wapo watapaswa walipe kodi”, alisema Kamishna huyo.

Alisema kwamba baada ya Bodi ya Mapato kupewa jukumu la kukusanya kodi ya ardhi, watafanya uhakiki kwa kukagua viwanja vya makazi ya wananchi ili kuhakikisha wageni wote wanalipia dola 5,000 kila mwaka wakiwemo wawekezaji katika sekta za kiuchumi.

Alisema Sera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini ifikapo mwaka 2020 inategemea sana ufanisi wa kukusanya mapato ya ndani ikiwemo kodi ya ardhi visiwani.

Hata hivyo, alisema mwekezaji Mzanzibari atapaswa kulipa kiwango cha dola 5000 kwa hekta moja katika eneo la mradi atakalokuwa ameanzisha ili kuchangia maendeleo ya nchi kwa lengo la kufanikisha uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake.

“Hatua hii itatuwezesha pia kuwafahamu wamiliki wote wakubwa na wadogo wa vipande vyote vya ardhi hapa Zanzibar, pamoja na wale ambao wanaotajwa kuhodhi maeneo makubwa kinyume na utaratibu,” alisema Kamishna Hashim.

Aidha, alisema mpango huo utawezesha kuwatambua wale wote wasiokuwa Wazanzibari kwa mujibu wa sheria wanaomiliki ardhi kinyume cha sheria na kuishauri serikali kuwachukulia hatua inayofaa.

“Bodi itatumia fursa hii kuvipitia upya viwango vya kodi vinavyotozwa hivi sasa ili kufahamu kama vinakwenda na wakati na kuishauri serikali ipasavyo,” alisema Hashim.

Alisema wizara imeamua kuipatia uwakala wa ukusanyaji wa mapato bodi hiyo kwa vile hivi sasa ulipaji wa ardhi sio wa kuridhisha na kusababisha deni kufikia dola za Marekani milioni tatu, wadaiwa wakubwa wakiwa ni wawekezaji katika sekta ya utalii.

Hata hivyo, alisema kabla ya utekelezaji wa zoezi hilo kuanza, bodi hiyo inatarajia kushirikiana na mradi wa SMOLE unaosimamiwa na Idara ya Ardhi ili kuziweka taarifa zote katika mfumo wa kompyuta kwa lengo la kuwatambua wale wote waliokodishwa ardhi Zanzibar pamoja na ramani zao.

Kamishna huyo alisema lengo kubwa ni kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuweka kumbukumbu sahihi za walipa kodi, kuondoa ukwepaji wa kodi pamoja na kupunguza gharama za serikali za ukusanyaji wa kodi na kujenga usimamizi bora.

Idadi kubwa wananchi wenye asili ya Tanzania bara wamefanikiwa kujenga Zanzibar kwa kuuziwa viwanja na baadhi ya wenyeji ambapo hivi sasa watalazimika kus--ajiliwa na kulipa dola 5,000 kila mwaka sawa na zaidi milioni tano za Tanzania kama kodi ya maendeleo ya kupitia sekta ya ardhi.

No comments: