Kipindi cha mwezi mmoja
nimejionea mengi kuhusu
polisi inavyofanya kazi.
Kwanza mdogo wangu anayeendesha bajaji ya mizigo alikamatwa na kuwekwa rumande kwa zaidi ya masaa 12. Kisa ni kukutwa na bajaj yake akipakia mizigo ya mteja wake aliyemsimamisha barabarani tu dakika chache zilizopita. Kweupe mchana, mbele ya geti la kiwanda, gti limefunguliwa, walinzi wawili wanasaidia kupakia mzigo, watu wengine wawili wapo wanasaidia pia na mteja wake (mwanamke) ambaye ni mfanyakazi wa hapohapo kiwandani naye yupo yupo anangojea mzigo wake upakiwe kwenye hiyo bajaj.
Ghafla bosi mmoja akaja, akasema yule mama (mteja wa mdogo wangu) ameongeza mzigo wa wizi. Kuna mali amenunua lakini ameongeza pengine furushi moja au mawili ya mabaki ya matairi yaliyo na thamani ndogo, pengine elfu 20 hivi. Kiwanda hicho kinafanya retreading ya matairi. Wakambembeleza sana, lakini akaamua kuwaita polisi.
Matokeo yake, landrover ya polisi ikaja, wote wakaswekwa rumande Mwanza pale central police. Kwa wanaume ni chumba kimoja kinanuka ile mbaya hata ukiwa mita 200 huwezi kuvumilia, kwa kutokana na joto, wanakaa vifua wazi. Chakula cha kugombania au ni kwa vibaka sugu tu ambao mle ni kama nyumbani kwao nk.
Kwa bahati tu mdogo wangu alinipigia simu kuwa anapelekwa polisi kuna issue ndogo ya kutolea maelezo. Nilipoona kimnya baada ya saa moja hivi nikaenda kufuatilia nini kulikoni. Kwenda huko nikaambiwa ndugu yako ana kosa kubwa sana la ujambazi/wizi/kupanga kuiba nk. hawezi kutoka hivihivi mpaka faili lake lipatiwe polisi wa upelelezi na mambo mengine mengi tu.
Kwa vile ana athma nilihangaika sana kumwekea dhamana ili atoke, lakini haikuwezekana mpaka usiku saa 5 hivi, na alitoka kwa bahati tu, angelala rumande hivihivi. Suluba hazikuishia hapo kwani alikuwa amefunguliwa jalada la kesi kama mshtakiwa wa wizi, kwa hiyo kazi ya kutoa maelezo na mengineyo yalifanya tukeshe huko tena kwa muda wa siku tatu hivi.
Narudi kwako DM: Ushauri niliopewa na wanaoijua nchi hii vizuri: bora angehonga kulekule, akaepuka kuletwa rumande kwani hata mtu aliyekubuhu u-mbux3 ataelewa kuwa kijana huyu hakuwa na shtaka la kujibu.
Hapa ndipo tulipofika. Hatuwezi kujua 240,000/- au 10,000/- ndiyo sahihi kwani inategemea unavyojali muda wako, afya yako iwapo itabidi ulale rumande na kadhalika.
Mchezo mwingine nimeujua hivi karibuni ni wa mstakiwa wako ambaye umemfungulia kesi polisi kukugeuzia kibao na wewe ndiyo kuwa mstakiwa, tena wa kesi mbaya zaidi.
Kinachofanywa ni mshtakiwa wako kwenda polisi kufungua kesi ya kupunguza makali ya kesi yake, kama ana connection huko mchezo unakuwa rahisi zaidi. Akifika huko anaandikisha mashtaka kuwa umemtishia kumuua kwa maneno na shahidi mmoja anatajwa, pengine mwanaye. Tangu hapo wewe unaanza kutafutwa na polisi kama mstakiwa, wakikupata unawekwa ndani. Matokeo yake badala ya wewe kuhangaikia kesi yako, unahangaika na namna ya kujitoa kwenye kesi mpya. Haya yamemtokea binti yangu, tena tuliambiwa walikosa gari tu, wangeenda kumkamata kazini kwake!
Jamani siyo Wahindi tu wanakumbwa na matatizo ya polisi. Halafu naona pengine bora utoe chochote hukohuko mtaani ili mradi usifike rumande, tena isiwe usiku au wikendi, utateseka mno hata kama huna kosa au una kosa dogo kama la Dr. Mohamed. Wengine mtasema woga, sawa tu. Muhimu ni kulitatua tatizo hili kwenye mzizi wake.
Rich... (kutoka Tanzanet)
No comments:
Post a Comment