Visiwa vya Maldives:
Kikao cha baraza la mawaziri
chafanyika chini ya bahari ya Hindi
Rais wa visiwa vya Maldives vilivyopo kwenye bahari ya Hindi, Mohamed Nasheed, makamu wake na mawaziri 11 walipiga mbizi chini ya maji siku ya jumamosi na kuweka historia duniani kwa kufanya kikao cha baraza la mawaziri ndani ya maji.
Rais Nasheed aliamua kufanya kikao hicho na mawaziri wake chini ya maji ili kuushinikiza umoja wa mataifa kuchukua hatua za kudhibiti uchafuzi wa hali ya hewa.
Kikao hicho kilifanyika chini ya maji kwa muda wa dakika 30 kwenye kisiwa cha Girifushi kilichopo kilomita 35 toka mji mkuu wa Maldives, Male.
Nasheed na mawaziri wake walitia sahihi waraka wa kuushinikiza umoja wa mataifa uchukue hatua ya kudhibiti uchafuzi wa hali ya hewa.
Kalamu maalumu zisizopitisha maji ( waterproof pencil) ndizo zilizotumika kutia sahihi waraka huo ulioandikwa kwenye vipande vyeupe vya plastiki.
Rais Nasheed ana cheti cha taaluma ya kupiga mbizi majini wakati mawaziri wake ilibidi wapewe darasa la kupiga mbizi wiki kadhaa kabla ya tukio hilo.
Visiwa vya Maldives viko mita 2.1 toka usawa wa bahari lakini kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa, wananchi wa Maldives wanahofia visiwa vyao vitafunikwa na maji ya bahari.
No comments:
Post a Comment