
JAMAA awliyefahamika kwa jina la Sinda Saidi mkazi wa Mtaa wa Saronge wilayani hapa, amenusurika kuuawa baada ya kubainika ana tabia ya kuwauzia watu nyama ya mbwa akidai kuwa ni ya mbuzi.
Tukio hilo la kustaajabisha lilitokea hivi karibuni baada ya raia wenye hasira kumzingira bwana huyo wakati akiwa amebeba mbwa ndani ya gunia akielekea kumchinja tayari kwa kuwauzia watu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, jamaa huyo alikuwa akifanya biashara ya kuuza nyama aliyodai kuwa ni ya mbuzi kilo shilingi 1,000 lakini baadaye ikagundulika kuwa nyama hiyo haikuwa ya mbuzi wala kondoo bali ni ya mbwa, ndipo wananchi waliamua kumuwekea mtego.
Siku ya tukio majira ya saa 11 jioni muuza nyama huyo alionekana katika mtaa wa Soronge akiwa amebeba gunia ambalo watu walilitilia shaka hivyo kumzingira na kutaka kujua alichokuwa amekibeba na kukuta ni mbwa.
“Unajua imekuwa ni tabia yake kukamata mbwa mtaani na kwenda kuwachinja porini kisha kuja kuwauzia watu...siku hiyo nadhani ilikuwa ndiyo arobaini yake, kwani tulipomweka chini ya ulinzi tukabaini alikuwa kabeba mbwa aliyekuwa akienda kumchinja,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Juma.
Akazidi kueleza kuwa, walipombana, kijana huyo alikanusha kuuza mbwa na kwamba kibudu huyo alikuwa ametumwa na tajiri yake aliyemtaja kwa jina la Mama Rhobi aende kumzika.
Katika hali ya kustaajabisha, kijana huyo alipolazimishwa kula kipande cha mbwa huyo alitafuna mnofu wake huku akisema kuwa ni mtamu sana jambo lililowaacha watu na butwaa.
Alipobanwa zaidi, alikiri kuuza nyama ya mbwa kwa kuchanganya na ya mbuzi na kudai kwamba kwa muda mrefu amekuwa akifanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha.
Majibu hayo yaliamsha hasira za watu waliokuwepo kwenye tukio ambapo walianza kumpiga lakini akaokolewa na polisi wa Kituo cha Bomani.
Mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya, (RCO) David Hiza alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Kutoka Global Publishers Ltd.
No comments:
Post a Comment