Thursday, November 05, 2009



Vigogo wa dawa za kulevya

wanafahamika


VIGOGO wa biashara wa dawa za kulevya nchini wanafahamika ila ni vigumu kuwashitaki.

Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za kulevya imetangaza kuwa, inawafahamu wanaotuhumiwa kuwatuma vijana wa Tanzania kwenda kuchukua dawa hizo nje ya nchi.

Kamishna wa tume hiyo, Christopher Shekiondo, amewaeleza waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, vigogo wa biashara ya dawa za kulevya wanafahamika ila ni vigumu kuwashitaki kwa kuwa si wanaokutwa na dawa hizo.

Shekiondo amesema, tume hiyo inawafahamu wanaotuhumiwa kumiliki dawa hizo, na kwamba , mahakama imewaonya wengi wa wanaotuhumiwa kufanya biashara hiyo haramu.

Ameonya kuwa, wamiliki wa biashara ya dawa za kulevya ni hatari kwa kuwa wapo tayari kufanya chochote ili kufanikisha azma yao.

Shekiondo amesema, mahakama imewaeleza watuhumiwa hao kuwa, kuna taarifa kwamba wanafanya biashara ya dawa za kulevya, waache, wakibainika watafungwa.

Kwa mujibu wa Shekiondo, si wote wanaokamatwa na dawa hizo walitumwa, na kwamba, baadhi yao ni wamiliki wa dawa hizo za viwandani zikiwemo Cocaine, Heroine na Mandrax.

“Wenyewe ukiwauliza wanasema kuliko nikae nife masikini, sina kitu, ngoja nijaribu” amesema Shekiondo wakati anasoma taarifa ya hali ya dawa za kulevya mwaka 2008 na kubainisha kwamba, kazi ya kudhibiti uingizaji wa mihadarati ni ngumu.

Amesema, mwaka jana, kilogramu 10.45 za Heroine na zaidi ya kilogramu tatu za Cocaine zilikamatwa nchini, na amefafanua kwamba, Cocaine hazijazagaa sana nchini kwa kuwa zinatumika zaidi Ulaya.

Kamishna Shekiondo amesema, ingawa kuna tuhuma kwamba, miongoni mwa vigogo wa biashara ya dawa za kulevya ni wanasiasa, tume haijalibaini hilo na huenda tuhuma hizo zinasababishwa na mtazamo wa jamii kuhusu neno ‘kigogo’.

Amesema, kwa mtazamo wa tume hiyo, kigogo ni mtu yeyote anayemtuma mtu mwingine kwenda kuchukua dawa za kulevya nje ya Tanzania hivyo si lazima awe mwanasiasa au mtu mwenye madaraka ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Shekiondo, watanzania wengi waliokamatwa nchini na dawa hizo walitoka Brazil na kwamba, vijana wengi watanzania wamekuwa wakitumika kusafirisha Cocaine kutoka nchini humo.

Amesema, kati ya mwaka 2006 hadi 2008, watanzania 102 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya wakiwemo 63 waliokamatwa mwaka 2006, 19 mwaka 2007, na 21 waliokamatwa mwaka jana.

Kamishna Shekiondo amebainisha kuwa, mwaka jana, watanzania sita walikamatwa Pakistani, sita walikamatwa Mauritius, wawili walishikwa Brazil, mmoja alikamatwa Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE), wanne ‘walidakwa’ Uingereza, na mmoja alishikwa Oman.

Amesema, watanzania wengi wanaanza kutumia dawa za kulevya wakiwa na umri wa miaka tisa hadi 10, na kwamba, wengi wa waliokubuhu wana umri wa miaka 15 hadi 38.

Kamishna huyo amesema, kuna kazi kubwa ya kuwaelimisha vijana wasitumie dawa hizo zikiwemo bangi na mirungi kwa kuwa wanaotumia ni mzigo kwa familia na taifa kwa ujumla kwa kuwa hawapo kwenye mzunguko wa kawaida wa uzalishaji wa mali.

Kwa mujibu wa Shekiondo, kuna ongezeko kubwa la matumizi ya Heroine katika miji mikubwa ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Tanga, Zanzibar, Arusha, na Mbeya.

Amesema, dawa za kulevya ni tishio kwa wanaotumia na wasiotumia kwa kuwa licha ya kumuathiri mtumiaji, zinasababisha ongezeko la maambukizi ya Ukimwi.

No comments: