Monday, January 25, 2010


Mzungu ajitangazia Jamhuri
yake Bukoba



RAIA wa Uingereza, Robert Maintland amejitangazia jamhuri yake kwa kupora ardhi ya wananchi wilayani Karagwe mkoani Kagera, huku uongozi wa wilaya hiyo na polisi wakishindwa kumchukulia hatua za kisheria.

Habari ambazo zimelifikia Tanzania Daima, zinasema wananchi wa eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao na kwenda kujificha kwenye vichaka kwa zaidi ya mwezi mmoja wakihofia kipigo kutoka kwa raia huyo, polisi na mgambo wanaodaiwa kumlinda.

Ubabe wa raia huyo wa kigeni na kulindwa kwake na dola, kumebainika baada ya timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kufanya ziara ya siku moja ili kujua ukweli wa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi kwa raia huyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, wananchi walisema kwa muda mrefu sasa wamelazimika kulala na kushinda porini ili kuepuka kipigo kutoka kwa askari wanaodaiwa kutoka ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera na mgambo wanaokodishwa kutoka maeneo yasiyojulikana.

Wananchi wengi wanadai wameshindwa kujishughulisha na kazi za kilimo kutokana na vitisho, vipigo na kuwekwa rumande, huku wakibambikizwa kesi mara wanapokutwa katika eneo hilo ambalo Maintland amelifanya kama nchi yake ndani ya Tanzania.

Mmoja wa wananchi hao, Bahati Mussa (32) alisema chanzo cha mgogoro huo kimetokana na Maintland kwenda kijijini hapo mwaka 2003 na kuanza kuweka mipaka ya mashamba bila kushirikisha jamii husika.

“Mwaka 2008 Maintland alirejea tena nchini na baada ya siku tano kupita baadhi ya wananchi walikwenda kumsalimia kama jirani yao, ambapo katika hali isiyo ya kawaida aliwataka waondoke katika eneo hilo,” alisema Bahati.

Hata hivyo, Musa alisema walilazimika kumhoji na yeye mwenyewe kuahidi kuwalipa sh 100,000 hadi 350,000.

Naye Elenestina Eleneus (74) alisema kutokana na kutokuwa na nguvu anapata shida kwa vile anatumia muda mwingi kushinda porini ili kusalimisha maisha yake.

Jenipha Romwad (29) alidai Novemba 2, 2008 alipata kipigo kikali kutoka kwa askari mmoja aliyemtambua kwa jina moja la James ambaye inasemekana aliagizwa na Maintland huku akivurumisha risasi kadhaa hewani za kuwatishia.

Kwa upande wake Maintland, alisema katika eneo hilo hakuna raia wa Tanzania anayeishi kwani wote waliopo ni wakimbizi kutoka nchini Burundi.

Alidai watu hao wanatumwa na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Willson Masilingi kuendelea kuishi katika ardhi yake ili aendelee kupata wapiga kura wengi kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Masilingi akizungumzia suala hilo, alikiri kupokea taarifa za malalamiko ya manyanyaso wanayofanyiwa wananchi hao.

Alisema siku za nyuma aliwahi kufanya mkutano wa hadhara akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Angelina Mabula ambapo waliagiza raia huyo akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria, lakini anashangaa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi.

Masilingi alisema inaonekana mzungu huyo anataka kumiliki kitongoji kizima licha ya wakazi wa eneo hilo kuishi miaka mingi katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Salewi alipotakiwa kutoa ufafanuzi, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwani anayeweza kulitolea ufafanuzi ni mkuu wa mkoa.

“Nina shughuli nyeti, kama waandishi wa habari mnataka mtu sahihi wa kuwapa ukweli nendeni mkaongee na mkuu wa mkoa, mimi sina la kuongea na waandishi kwa leo, ni siku ya mapumziko,” alisema Salewi.

Tanzania Daima imebaini kuwa eneo linalogombaniwa kabla ya uhuru lilikuwa na ukubwa wa ekari 900 na baadaye 200 ziligawiwa kwa wananchi na mara ya mwisho eneo hilo lilipimwa Septemba 15, 1927 na kugawawia kwa wananchi mwaka 1961.

Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: