Uharibifu wa mazingira Mara ya Kaskazini
Asalaam-aleikum Vijana wenzangu!
Unapoona picha za watu wanavyoathirika kutokana na uzembe, tamaa, uchoyo na ukatili wa binadamu wengine (angalia nakala iliyopita), hisia zinaweza kuchukua mkondo wake na ukabaki na fikra ambazo sio sahihi au zilizopotoka kwa namna moja au nyingine. Kwahiyo, baada ya kutulia nikaamua kuliangalia sakata la vitendo vya Barrick Gold Mine, na matokeo yake - uharibifu wa mazingira na athari zake kwa afya za watu - kwa utulivu.
Kama kijana wa Kitanzania, sitegemei au sitaki kuanzisha shari, lakini naaminikuwa wananchi wanastahili kujua kinachoendelea na kujibiwa maswali yao. Na hilo ni jukumu la uongozi wa Barrick GM, Mara na Serikali yetu. Kama kuna sehemu ambayo nimekosea kwenye uchambuzi au mtitiriko wa yanayojiri huko Mara, nitakubali kukosolewa na kuwekwa sawa (mimi sio mkemia wala mwanasheria)!
Tatizo la uchafuzi na uharibifu wa mazingira kwenye sehemu zinazozunguka mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na Barrick GM lilianza mnamo Mei 2009. Na Wizara ya Nishati na Madini ilifanya uchunguzi.
Ripoti ya Wizara iliyotolewa tarehe 4 Juni, 2009 ilijadili uharibifu wa mazingira tu. Chanzo cha haya yote kilikuwa ni maji ya acid kutoka kwenye dampo la Barrick GM yaliyokuwa yanaingia kwenye mto Tighithe. Maji hayo yalikuwa yanaingia kwenye mto kupitia bwawa lililokuwa halina vizuizi. Cha kusikitisha na kushangaza sana ni kilichoandikwa kwenye ripoti:
Jamani, uchunguzi wa Wizara yetu, inayopaswa kuheshimika na kuaminiwa, ni kuangalia pH level tu? Yaani kwenda pale na litmus paper/solution auphenolphthalein? Kwenye karne hii? Hawajui kwamba labda kulikuwa na elementsnyingine zinazoweza kuhatarisha maisha ya binadamu? Ni kama kumpima mgonjwa wa Ukimwi kwa kuangalia upele wake tu; na kumwambia akaoge maji ya chumvi.
Majadiliano kati ya 'wawakilishi' wetu na uongozi wa Barrick GM yalikuwa kama ifuatavyo:
Bila chembe ya aibu na kukataa jukumu lao, uongozi unatupia lawama uhalifu unaofanywa na wananchi. Na kuna Watanzania wanaodiriki kusema, "(Waathirika) wameyataka haya matatizo wenyewe." Tuwekane sawa kwanza: Jukumu la Barrick GM ni kuwaelimisha wananchi kuhusu mambo yote yanayoendelea na utupaji wa taka kutoka kwenye mgodi. Kama kuna takataka za sumu ilipaswa wataarifiwe na waelimishwe madhara yake. Pia, ulinzi wa kutosha unatakiwa uwepo sehemu kama hizi muda wote. Ukifuatilia mambo yanayoendelea kwenye sehemu kama hizi (mining sites na nuclear plants) kwenye nchi zao (Ulaya na Amerika), utaona jinsi mitaro ya takataka ilivyojengwa kwa zege zito ambalo kibaka hawezi hata kuchora juu yake. Doria za wanausalama ni masaa 24! Lakini kwasababu shughuli zinafanyika Tanzania...
Ripoti inamalizia kwa kusema:
Haya yalipaswa kutekelezwa kabla shughuli za uchimbaji haujaanza. Nina uhakika haya matatizo tunayoyaona na kuyasikia leo yasingetokea kama Wizara yetu na uongozi wa Barrick GM wangekuwa makini.
Cha kusikitisha zaidi kwenye matukio yote haya ni kitendo cha viongozi wetu kuwasahau kabisa watu wanaoishi kwenye vijiji vilivyoko jirani na mgodi - hasa watumiaji wa mto Tighithe. Ripoti ya Wizara haitaji wala kujadili athari zozote kwa afya za wananchi.
Athari za uchafuzi wa maji ya mto Tighithe kwa afya za watu zilianza kuonekana.Foundation HELP ya Mara ilianza zoezi la kupima afya za baadhi ya waathirika wenye dalili ambazo ni rahisi kuziona. Dalili za waathirika zinatofautiana; kuharisha, kutapika, kujikuna, maumivu ya tumbo, mapunye (madonda makubwa makubwa) na wengine wana dalili za magonjwa ya kansa ya ngozi. Makelele haya yalifika kwenye masikio ya viongozi wa Barrick GM, ambao walitupia lawama uwizi unaofanywa na wananchi (kumbuka, hili lingeweza kuepukwa).
Kwa mujibu wa Foundation HELP, eneo zima la Mara Kaskazini lipo katika mkondo ambao ni hatari. Ikumbukwe kuwa pamoja na kuwa kulikuwa na shughuli za wachimbaji wadogo hapo kabla, hakukuwahi kuwa na matukio kama hayo ambayo Barrick wanalaumu. Eneo hilo lina miamba inayotengeneza acid, na acid hii inayeyusha vitu vingine (heavy metals).
Binafsi nadhani hapa ndipo "siasa" inapoingia - kuweka facts pembeni na kujitahidi kuonesha umma kuwa hakuna kosa lililotendeka. Wakati huo huo afya za watu walioathirika zinazidi kudhoofika.
Dalili za waathirika zinaasharia madhara ya kula heavy metals. Watu wa Barrick wanadai eneo hilo lina heavy metals kupita kiasi cha kawaida. Je, kama wanalijua hilo, kwanini hawakuwa waangalifu zaidi kuhakikisha yanayotokea sasa hivi hayatokei??
Suala la fidia kwa waathirika? Barrick ni corporation kubwa na wana bima ya kufidia walioathirika kwenye hii "ajali". Mbona kimya mpaka leo? Au hawajawaona waathirika?
Serikali yetu nayo imekuwa bubu. Si ni wajibu wenu kututetea wananchi; au angalau kutujibu maswali yetu?
Kusema ukweli sakata zima linasikitisha sana na kutia hasira! Kwa wale waliokuwa na imani hata chembe na Serikali na viongozi wetu nadhani sakata hili litawafumbua macho. Na inashangaza pale vyombo vya habari vinapogoma kufanya kazi yao.
Kutoka: http://vijanafm.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment