Tuesday, April 27, 2010

Aliyemwua Malcolm X
aachiwa baada ya miaka 44

Malcolm X (Al Hajj Malik El Shabazz)

Thomas Hagan (69), aliyekuwa akijulikana kama Talmadge X Hayer, akiwa na umri wa miaka 22 mwaka 1965, ni mtu pekee aliyekubali kuwa ndiye aliyemwua Malcolm X (Al Hajj Malik El Shabazz) ameachiwa na bodi ya msamaha baada ya kutumikia kifungo cha miaka 20 hadi maisha. Alihukumiwa mwaka 1966 na wenzake wawili, Muhammad Abdul Aziz na Kahlil Islam, wote watatu wakiwa wanachama wa kikundi cha Kiislamu cha Waafrika Waamerika kijulikanacho kama Nation of Islam. Aziz na Islam wamekana katakata kuhusika na mauaji wa Malcom X, nao walifungwa maisha. Aziz alisamehewa mwaka  1985 na Islam mwaka 1987.



Malcom X alipigwa risasi na kuuawa alipokuwa akitoa hotuba kwenye ukumbi wa Audubon Ballroom mjini New York tarehe 21 Februari 1965, mbele ya mkewe Dr. Betty Shabbaz na watoto wake wanne.





Malcolm X alikuwa mwanachama wa Nation of Islam na akajitoa na kuanza kumlaumu kiongozi wao wakati huo, Elijah Muhammad kuwa ni mwongo, ndumilakuwili, mnafiki na punguani. Kujitoa kwa Malcolm X kutoka kwenye Nation of Islam kulimjengea maadui wengi, kiasi mwenyewe alianza kuhisi kuwa maisha yake yako hatarini.


Mwanzoni Malcom X alikuwa na itikadi kali sana kuhusu watu wengine, kiasi cha kuonekana kama mbaguzi wa rangi, lakini alibadili msimamo pale alipokwenda kuhiji Mekka. Alipokuwa Mekka alikutana na watu wa aina mbalimbali na kufunguka macho. Akabadili jina na kujiita Malik El Shabazz.



Muda mrefu Thomas Hagan amekuwa akiomba kusamehewa, lakini amekuwa akikataliwa. Mara ya mwisho alipoomba alipewa sharti la kutafuta kazi na kuwa nayo kwa muda mrefu, kupimwa kuangalia kama hatumii madawa. Amekuwa akifanya kazi nje kwa miaka saba sasa na amesoma akiwa jela hadi kuchukua shahada ya uzamili ya sosholojia. Anasema bado ni mwislamu lakini si mwanachama wa Nation of Islam. Hagan amefurahi kuwa huru na kusema kuwa atatumia muda mwingi aliobaki nao kuwa pamoja na watoto wake, wenye miaka 21, 17, 14 na 10.



No comments: