Thursday, April 29, 2010

Mraba wa Maggid kwenye Raia Mwema

Kudumisha Kiswahili ni kudumisha utamaduni wetu


HATUA ya hivi karibuni ya Serikali kutoka waraka wenye kutaka Kiswahili kitumike katika shughuli mbalimbali za kitaifa ni ya kupongezwa.

Juhudi zozote zile za kuitangaza, kuikuza na kuilinda lugha ya Kiswahili ni juhudi za kuulinda utamaduni wetu. Hakika inahusu utamaduni. Na utamaduni ni utaratibu wa maisha ikiwa ni pamoja na sanaa za maonyesho, muziki asilia, ngoma za asili, tamthilia, lugha, sanaa za ufundi, filamu na chakula. Utamaduni ni utambulisho wa mtu husika.

Tuna kila sababu ya kujikita katika kurejesha heshima, hadhi, moyo na juhudi za kukuza utamaduni wetu unaotishiwa kumezwa na tamaduni za kighaibu hususan zile za kimagharibi. Tutumie utandawazi unaoambatana na sayansi na teknolojia kama nyenzo na fursa ya mafanikio ya jitihada za kuendeleza, kukuza, kusambaza na kuuza utamaduni wetu.

Tuuthamini, kuuendeleza na kuukuza utamaduni wetu.

Leo ukisikiliza muziki unaopigwa kwenye redio zetu, filamu zinazonyeshwa na hata kuigizwa na Watanzania wenzetu. Ukiangalia aina ya mavazi tunayovaa, vyakula tunavyokula na hata lugha tunayozungumza. Vyote hivyo havitoi taswira ya utamaduni halisi wa Mtanzania. Maeneo ya mijini ndiyo yanayoelekea kumezwa zaidi na tamaduni za kighaibu.

Tuna haja ya kutafakari kwa kina juu ya utamaduni tunaoujenga sasa. Itakumbukwa, miaka ile ya mwanzoni mwa uhuru wetu, masuala ya utamaduni yaliwekwa chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Wizara hii ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1962. Kunako Desemba 10, mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliweka bayana majukumu ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, Mwalimu alitamka yafuatayo; " Mabadiliko makubwa niliyoyafanya ni kuanzisha Wizara mpya ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Nimefanya hivyo kwa kuamini kuwa Utamaduni ni kitu muhimu na ni roho ya taifa lolote liwalo.

Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu walikosa ari na moyo wenye kuwafanya kuwa taifa. Moja ya dhambi kubwa ya wakoloni ni ile hali ya kutufanya tuamini kuwa hatuna utamaduni wetu wa asili; au kwamba yote tuliyokuwa nayo hayakuwa na thamani yoyote-kitu ambacho tulipaswa tukionee aibu badala ya kuwa chanzo cha kujivunia.

Baadhi yetu, hususan wale tulioelimishwa na Wazungu tunanajaribu kuwathibitishia wakoloni waliotutawala kwamba "tumestaarabika" ikiwa na maana tumeachana na yale yote yenye kutuunganisha na utamaduni wetu wa asili. Kwamba tumejifunza kuiga utamaduni wa Kizungu. Malengo ya vijana wetu hayakuwa kuwa Waafrika walioelimika bali kuwa Wazungu Weusi." Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962.

Bila shaka, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mfano wa viongozi waliothamini na kuuenzi utamaduni wetu ikiwamo lugha ya Kiswahili. Leo tunashuhudia jinsi jamii yetu ilivyovamiwa na tamaduni za kighaibu. Ni dhahiri kuwa utamaduni unaimarika kwa kuiga yaliyo mazuri kutoka tamaduni nyingine. Lakini katika jamii yetu, tamaduni za kighaibu hususan kutoka Ulaya na Marekani zaelekea kukumbatiwa zaidi na wanajamii na hivyo basi kuhatarisha kuufifisha na pengine kuuangamiza utamaduni wetu.


Vijana wetu wanaona fahari zaidi kuimba na kucheza nyimbo na miziki ya kighaibu. Wanaona aibu kuimba nyimbo za Kiswahili. Nyimbo za makabila yetu kwa mfano Kinyamwezi, Kizaramo na nyinginezo za asili. Vijana wetu wanaona fahari kuongea Kiswahili kwa lafidhi ya Kiingereza. 

Vijana wetu wengi wa siku hizi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kucheza Gombe Sugu, Mganda, Mangala, Konge, Nyang'umumi, Kiduo, au Lele Mama. Hizi ni baadhi tu ya ngoma zetu za asili. Vijana wetu wengi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kupiga vyombo vya muziki vya asili kama vile Marimba, Kilamzi, Ligombo au Imangala.

Na tuangalie ni jinsi gani tutaweza kuuhifadhi, kuuendeleza na kuuimarisha utamaduni wetu. Labda hapa kuna haja ya pekee ya kutoa mfano wa suala la matumizi ya lugha kwa vile ndio kitovu cha utamaduni. Kwa upande wetu ni lugha ya Kiswahili.

Hivi leo kuna wanaozungumza au kuandika kwa Kiingereza mahali ambapo asilimia 90 ya wasikilizaji au wasomaji ni wazungumzaji wa Kiswahili. Hiyo ni hali ya kutojiamini. Ni kubaki katika hali ya utumwa wa fikra. Je, wenye kufanya hivyo wana malengo ya kuwaonyesha "wakoloni" au "wafadhili" wa semina kwamba wao "wamestaarabika"? Au wanafanya hivyo ili kuwaridhisha wafadhili tu? (Rejea kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962 hapo juu). Kwa nini waandaaji wa semina wasitumie wakalimani kuwatafsiria wasio wazungumzaji wa Kiswahili ambao ni asilimia 10 tu ya kadamnasi. Hilo pia lingetengeneza ajira kwa baadhi ya Watanzania.

Suala la kujiamini ni suala la utambulisho. Binadamu hawezi kujiamini kama hana hakika ya utambulisho wake. Tujiulize; sisi ni nani? Hili ni swali gumu na la kifalsafa. Lakini ni swali lenye kuhitaji majibu ili tuweze kujenga msingi imara wa utamaduni wetu.

Katika kujibu swali la sisi ni nani? Hatuna budi kuiangalia historia yetu. Historia ni wakati, muda. Kihistoria jana ni sawa na zamani. Wahenga wetu walitafsiri muda kama mkusanyiko wa matukio ya zamani na sasa. Waliamini yaliyotokea zamani na yanayotokea sasa ndiyo yenye kusaidia kubashiri yatakayotea kesho. Yataamua mustakabali, hali ya baadaye.

Kuna tofauti ya zamani kidogo na zamani sana. Kuna tofauti pia ya sasa hivi na sasa, baadaye kidogo na baadaye sana. Hatuwezi kuyazungumzia ya “ zamani sana” bila kugusia mila, jadi na desturi za wahenga wetu. Mila, jadi na desturi, ni sehemu ya urithi na hazina walizotuachia wahenga. Ni jadi, mila na desturi hizo ndizo zilizojenga msingi wa Taifa hili la Tanzania.

Wahenga wetu waliishi kwa kujikimu na walitumia mbinu na maarifa mengi katika harakati za kuziendeleza jamii zao. Miongoni mwao kulikuwa na mabingwa wa uhunzi, uashi, tiba na mengineyo. Jamii haikusimama kama mlingoti, ilikuwa ikipiga hatua za kimsingi na za kimaendeleo.

Miongoni mwetu kuna wenye majina ya kujivunia na yenye kuonyesha nuru ya historia yetu, mathalan,majina kama, mhunzi, fundi, chuma na mengineyo. Majina hayo yametokana na shughuli za jadi zikionyesha kuwa wahenga walianzisha hatua za maendeleo ya kiteknolojia.

Tusisahau kuwa, kuna miongoni mwetu wenye majina yenye kuonyesha doa jeusi la historia yetu, ukiyasikia majina hayo yanakumbushia majonzi na huzuni kuu iliyowafika wahenga. Majina kama Mtumwa, Kitwana na Kijakazi, Majiyapwani na mengineyo. Ni majina muhimu yenye kubeba historia yetu katika kipindi kile cha biashara ya utumwa. Hiyo ni historia yetu. Utambulisho wetu unatokana na historia hiyo. Hatuwezi kujitenga wala kuikana historia yetu. 

Tujivunie historia yetu na utamaduni wetu ikiwamo lugha ya Kiswahili.
http://www.raiamwema.co.tz/images/hs3.gif

Simu:  
0754 678 252

Barua-pepe:  

Blogu:  


No comments: