Monday, April 26, 2010



Tunawatakia sikukuu njema
Watanzania wote kwa
kuadhimisha miaka 46 ya
Muungano.

Chama Cha Watanzania Oslo, Norway.

****************************
YAJUE MAENEO 22 YA MUUNGANO

MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar, uliasisiwa Aprili 26, 1964 na kuanzishwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka huu, muungano huo unatimiza miaka 45 tangu kuasisiwa kwake.

Katika kuhakikisha Muungano huo unakuwa na ustawi, kuna maeneo 22 ambayo yameorodheshwa katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Maeneo hayo ni Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya Nchi za Nje; Ulinzi na Usalama; Polisi; Mamlaka juu ya mambo yanayohusiana na hali ya hatari; Uraia; Uhamiaji; na Mikopo na Biashara ya Nchi za Nje.

Mengine ni Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania unaosimamiwa na Idara ya Forodha; Bandari, mambo yanayohusika na usafiri wa anga, posta na simu; na Mambo yote yanayohusika na sarafu, fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti), mabenki (pamoja na mabenki ya kuweka akiba) na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.

Pia yapo maeneo kama vile Leseni za Viwanda na Takwimu; Elimu ya Juu; Mahakama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano; Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na Gesi asilia; Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo; Usafiri na usafirishaji wa anga; Utafiti; Utabiri wa Hali ya Hewa; Takwimu; na Uandikishaji wa Vyama vya Siasa na mambo mengine yanayohusiana na hayo.


KATIBA YA TANZANIA

Katiba ni moja ya mambo ya Muungano yaliyoorodheshwa kwenye nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Tanzania inaendelea kuwa na Katiba ambayo inaheshimiwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Taratibu mbalimbali ambazo Katiba imeweka katika kuulinda Muungano zimekuwa zikifuatwa na viongozi na wananchi kwa ujumla.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia utekelezaji wa mambo yote ya Muungano ikiwa ndio yenye Dola (Sovereignity). Zanzibar ina Katiba yake ya mwaka 1984 na ina mamlaka ya mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar. Aidha, masuala yote ya Muungano yamewekwa bayana katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


MAMBO YA NCHI ZA NJE

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ndiyo yenye wajibu wa kuratibu na kusimamia masuala yote ya Kimataifa yaliyo ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pande zote mbili za Muungano zimekuwa zikishirikishwa katika uwakilishi wa masuala muhimu ya kimataifa yakiwamo makongamano ya biashara, uwekezaji na mikutano yote muhimu ya kimataifa.


MIKOPO NA BIASHARA YA NCHI NA NJE

Serikali ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio yenye Dola inawasiliana na wahisani kupata mikopo nafuu ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa utaratibu uliopo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaweza kuzungumza na Wahisani moja kwa moja kwa lengo la kupata misaada.

Zanzibar inapata gawio la asilimia 4.5 itokanayo na misaada na misamaha ya madeni. Hata hivyo, Serikali imetambua umuhimu wa kuwa na utaratibu wa kudumu wa kugawana mapato yatokanayo na vyanzo vya mapato ya Muungano na kuchangia gharama za Muungano.

Hivyo basi, Tume ya Pamoja ya Fedha ilipewa jukumu hilo na tayari imewasilisha Serikalini mapendekezo yake kuhusu vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano. Mapendekezo ya Tume ni mengi na yanahitaji uchambuzi wa kina na majadiliano kati ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kabla ya kufanyiwa uamuzi.

Kuhusu uimarishaji wa uchumi kwa pande zote mbili, Serikali inatekeleza Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (JAST). Mkakati huu ni muhimu ili kuleta uwiano wa maendeleo kwa pande zote mbili za Muungano. Huu ni Mpango wa Taifa kwa ajili ya kudumisha ushirikiano kimaendeleo kati ya Serikali ya Muungano na Wafadhili katika kuleta maendeleo ya Taifa kwa ujumla na kupunguza umaskini nchini.


SARAFU NA FEDHA

Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Na. 1 ya mwaka 1995 iliyotungwa inazingatia maslahi ya pande zote za Muungano. Aidha, kuna Sheria inayosimamia benki zote zote nchini.

Benki Kuu ya Tanzania ina matawi yake pande zote mbili za Muungano. Aidha, pande zote za Muungano zina uwakilishi katika Benki Kuu ya Tanzania na zinapata faida na huduma za kibenki kutoka Benki Kuu. Zanzibar inaendelea kupata gawio la asilimia 4.5 kutokana na faida inayotokana na shughuli za Benki Kuu.


UTUMISHI SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO

Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003 zimeweka utaratibu wa wazi wa ajira katika Utumishi wa Umma na kuondoa dosari zilizokuwapo. Ajira katika Sekta za Muungano uzingatia vigezo vilivyowekwa kama Elimu, Uzoefu na Sifa husika.

Hata hivyo, kuna tatizo la ushindani katika soko la ajira kwani kuna tofauti ya mitaala ya elimu ya Msingi na Sekondari kati ya pande mbili na hivyo kusababisha tofauti ya viwango vya elimu ambavyo husababisha matatizo katika fursa za ajira. Imeundwa kamati yenye jukumu la kurekebisha mitaala na tayari imeshafanya vikao vitatu Desemba 2006, Machi 2007 na Desemba 2007. 4.

Kodi ya Mapato na Forodha Suala la Kodi ya Mapato ni suala muhimu katika Nchi yetu na Nchi nyinginezo.

Kuna tatizo la malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili. Juhudi mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mtandao wa ASYCUDA++ ambao umeanza kufanya kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Zanzibar ili kuondoa tatizo la kodi.

Aidha, Mamlaka imeendelea kuijengea uwezo wa kiutendaji Bodi ya Mapato Zanzibar chini ya mradi wa ‘’Tax Modernization Project’’ (TMP).


BANDARI, MAMBO YANAYOHUSIKA NA USAFIRI WA ANGA, POSTA NA SIMU. 

Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji wa anga ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwanja wa ndege – Zanzibar, ndege kubwa kuruhusiwa kutua Zanzibar na kuruhusu mashirika ya watu binafsi kuendesha biashara ya usafiri na usafirishaji wa anga.

Usafiri wa majini nao umeboreshwa kwa kuwaruhusu watu binafsi kutumia vyombo vya kisasa kusafirisha wananchi wa pande zote mbili kati ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Zanzibar na Pemba. Hali kadhalika hali ya mawasiliano ya simu imeendelea kukua kwa kasi kubwa katika pande zote mbili za Muungano. Mfano matumizi ya simu za viganjani na Makampuni ya simu hizo yanafanya kazi pande zote za Muungano bila vikwazo.

Aidha, juhudi mbalimbali zimechukuliwa na Serikali kuimarisha Bandari pande zote mbili za Muungano. Wizara husika za pande mbili kwa kushirikiana na Wizara ya Afrika Mashariki imeainisha miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar ambayo itaingizwa katika miradi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Miradi iliyokubalika ni pamoja na Ujenzi wa Bandari mpya ya Marhubi (New Marhubi Hub Port).

Zanzibar inawakilishwa ipasavyo katika Tume ya Mawasiliano ambayo inasimamia Sera na udhibiti wa shughuli za Mawasiliano ya Posta na Simu. Aidha, suala la usimamizi, udhibiti na Sera ya usafirishaji wa anga linaendelea kuwa suala la Muungano.


BARAZA LA MITIHANI LA TANZANIA

Chombo hiki kipo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Serikali ya Muungano wa Tanzania. Kazi kubwa ya Baraza la Mitihani ni kutunga na kusahihisha mitihani kwa pande mbili za Muungano isipokuwa kwa mitihani ya kidato cha tatu ambayo hutungwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Baraza la Taifa la Mitihani linaendeshwa na Bodi ya Wakurugenzi ambapo Zanzibar ina wajumbe katika Bodi hiyo. Aidha, Baraza huajiri watumishi kutoka pande zote za Muungano, ili kuwa na uwiano wa watumishi.

Sekta za elimu za pande mbili za Muungano hivi sasa zinaendelea na mchakato wa kuhakikisha mitaala inayotumika katika shule za Msingi na Sekondari za Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara inaainishwa ili Baraza la Taifa la Mitihani linapotunga mitihani iwe na ushindani ulio sawa.


ELIMU YA JUU

Kwa mujibu wa Sheria Na. 25 ya Mwaka 1978, Elimu ya juu ni mafunzo yatolewayo baada ya kumaliza mafunzo ya cheti cha kuhitimu kidato cha sita au elimu nyingine inayofanana na hiyo ambapo mhitimu hutunukiwa shahada ya kwanza au Stashahada ya juu.

Kutokana na tofauti ya mitaala ya elimu ya msingi na sekondari wanafunzi kutoka Tanzania Zanzibar hushindwa kuingia katika soko la ushindani na hatimaye kuwa na fursa chache katika kujiunga na vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo Tanzania Bara. Hata hivyo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa, mitaala inayotumika katika shule za Msingi na Sekondari za Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara inaoanishwa ili ushindani kwa pande zote mbili za Muungano uwe sawa.


LESENI ZA VIWANDA

Shughuli za Leseni na Takwimu za Viwanda zipo chini ya Wizara ya Biashara na Viwanda ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na chombo cha utekelezaji ni Mrajisi wa Viwanda na Bodi ya Utoaji wa Leseni za Viwanda.

Mrajisi wa Viwanda na Bodi ya Utoaji wa Leseni za Viwanda wanashirikiana na Naibu Msajili wa Viwanda Zanzibar. Aidha, BRELA imeendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kila inapohitajika. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inawakilishwa kikamilifu kupitia wajumbe wawili katika Bodi ya Leseni za Viwanda.


BRELA

imetoa nakala ya Sheria mpya ya makampuni inayotumika kwa sasa Tanzania Bara kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuoanisha na Sheria ya Makampuni Zanzibar. Pande zote mbili zilishiriki kikamilifu katika mchakato wa kubadili Sheria ya kuandikisha majina ya biashara iliyofanyika Agosti 2005 na pia katika mchakato wa kuunganisha Sheria za “Intellectual Property Rights” kuwa Sheria moja.

MAHAKAMA YA RUFANI TANZANIA

Mahakama ya Rufani ni ya Jamhuri ya Muungano na inasikiliza kesi zinazohusu masuala yote isipokuwa kesi zinazotokana na masuala ya dini ya Kiislamu zilizoamuliwa kwa upande wa Zanzibar.

Ibara ya 98(2) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inazuia Mahakama ya Rufani kutekeleza madaraka yake kuhusu kesi za Dini ya Kiislamu, kesi zinazohusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar na mambo mengine yaliyoainishwa katika Katiba hiyo au Sheria zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi. Mahakama ya Rufani ina vituo saba kwa Tanzania nzima ambavyo ni Dar es Salaam ( Makao Makuu), Mwanza, Dodoma, Arusha, Zanzibar, Mbeya na Tanga.


MALIASILI YA MAFUTA NA GESI ASILIA

Katika kufanya utafiti wa kuchimba mafuta katika maeneo ya Pwani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia mkataba na kampuni za kimataifa. Kabla ya kazi hiyo kuanza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa na hoja ya msingi ambayo ilibidi itatuliwe kwanza.

Hoja kuu ilikuwa ni namna ya kugawana mapato yatakayotokana na mafuta endapo yatapatikana. Serikali zetu baada ya kujadiliana ziliamua kuwa atafutwe Mshauri Mwelekezi ili atoe ushauri wa kitaalamu kuhusu suala la mgawanyo wa mapato kwa nchi zilizoungana.

Makadirio ya gharama za Mshauri Mwelekezi na maandalizi ya zabuni pamoja na mpango wa utekelezaji wa mchakato wa zabuni kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, zimekamilika na endapo ratiba ya utekelezaji itafuatwa, kazi ya Mshauri Mwelekezi itakamilika mwishoni mwa mwezi wa Agosti, 2008.


UANDIKISHAJI WA VYAMA VYA SIASA

Suala la kusajili Vyama vya Siasa linaendelea kuwa suala la Muungano ambapo hadi mwaka 2008 vyama 17 vimesajiliwa na vimeshiriki kikamilifu katika masuala mbalimbali ya kisiasa nchini. Aidha, Ofisi ya Msajili wa Vyama imefungua tawi la ofisi zake Zanzibar ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia vyama vya siasa pande zote mbili za Muungano.

UTAFITI

Suala la Utafiti linasimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria Na. 7 ya Mwaka 1986 ambayo hutumika Zanzibar pia. Bodi ya usimamizi wa Tume ina wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano.

UTABIRI WA HALI YA HEWA

Chombo hiki kinasimamiwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa chini ya Wizara ya Miundombinu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushirikiano kati ya ofisi za Mamlaka zilizopo Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara ni mzuri, jambo hili linatakiwa kuimarishwa ili Muungano uimarike katika sekta hii.

TAKWIMU

Kila upande wa Jamhuri ya Muungano una Sheria na Idara yake ya kusimamia shughuli za Takwimu, hata hivyo wakati wa kuhesabu watu (census), Idara hizo mbili zinafanya shughuli hiyo kwa pamoja.

UHAMIAJI

Sheria ya Uhamiaji Na. 6 ya mwaka 1995 ilitungwa na hivyo kufuta sheria zote zilizokuwapo awali kwa Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara. Wananchi wa Tanzania wanaweza kuingia na kutoka Tanzania Zanzibar na Bara bila matatizo. URAIA Sheria inayotumika ni Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995. Sheria hii ilitungwa ili kufuta sheria mbalimbali zilizohusu uraia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuleta mkanganyiko kwenye suala Uraia.

UTANGAZAJI WA HALI YA HATARI

Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Hali ya Hatari ya 1986 kinampa Mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza hali ya hatari na anaweza kukasimu madaraka hayo kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika Sheria tajwa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamepewa madaraka kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kutangaza hali ya hatari katika maeneo yao.


POLISI

Jeshi la Polisi ndilo lenye jukumu la kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa kwa wananchi pamoja na kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa. Tangu Muungano ulipoanza Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa sio tu kudumisha amani bali hata kushirikiana na wananchi wa kawaida katika shughuli nyingine za maendeleo. Aidha, msukumo wa makusudi wa kuwezesha Maofisa wa Polisi kufanya kazi pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano zimechukuliwa.

ULINZI NA USALAMA

Suala la Ulinzi na Usalama limeendelea kutekelezwa kimuungano ambapo vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimeendelea kufanya kazi ya kulinda Nchi yetu na kushiriki katika shughuli za kijamii. Vijana kutoka pande zote za Muungano wanapewa fursa ya kujiunga na vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwamo mafunzo.

USAFIRI NA USAFIRISHAJI WA ANGA

Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha sekta ya usafiri wa anga hii, ikiwa ni pamoja na kuuboresha uwanja wa ndege wa Zanzibar, kufungua Ofisi ndogo ya msaidizi wa Mamlaka ya usafiri wa anga Zanzibar na kuruhusu mashirika ya watu binafsi kuendesha biashara ya usafiri na usafirishaji. Aidha suala la usimamizi, udhibiti na Sera ya usafiri na usafirishaji wa anga vimeendelea kusimamiwa na kuratibiwa vizuri katika sura ya Muungano.



No comments: