Tanzania –
nchi ya amani na utulivu..?!
Kile kilichotokea Tunisia, kinaweza kutokea Tanzania. Wimbo wa “Nchi yetu ni ya amani na utulivu” unaanza kufifia kwa matukio yaliyojitokeza na yanayojitokeza nchini.
Tuchukue mfano wa Tunisia. Fikiria jamaa kamaliza chuo kikuu, hana kazi. Kaamua kujitafutia ajira yake mwenyewe kwa kuuza mboga mboga. Polisi wamemvuruga akili kwa kumkataza jamaa kuuza mboga mboga, mpaka jamaa akaamua kujitia kibiriti na kumaliza maisha yake. Kitendo cha jamaa kikaanzisha mapinduzi ya Yasmin yaliyomwondoa madarakani Rais Zine El Abidine Ben Ali, akakimbilia Saudi Arabia.
Waziri mkuu wake, ametaka kuunda serikali ya mpito kufikia uchaguzi mkuu, wananchi wanaonyesha kuwa hawataki mabadiliko nusu nusu. Wanataka mabadiliko ya jumla. Yaani wanataka viongozi wote waliokuwa chini ya Rais Ben Ali wang´atuke! Bado wanaandamana!!!
Hii inaonyesha kuwa tayari Watunisia walikuwa wamechoshwa na dhuluma, ufisadi, ujeuri na ubabe wa viongozi wao. Kujichoma moto kwa huyo kijana ilikuwa ni kama kupulizia moto uliokuwa chini ya kuni!!!
Tunisia ni moja kati ya nchi chache za Kiarabu zilizo na mwelekeo wa maendeleo ya jinsia zote na ni moja ya nchi za Kiarabu zilizokuwa na wimbo wa “nchi ya amani na utulivu” kama Tanzania.
Maisha ya kila siku yanayowakera Watanzania wengi, yanafanana na yale ya Watunisia. Kilichotokea Tunisia kinaweza kutokea Tanzania. Tusidanganyane!
Tunawaomba viongozi wetu waangalie nini kilichosababisha Watunisia kuanzisha mapinduzi ya Yasmin, warekebishe ili nasi Watanzania tusije tukawa kama Watunisia.
Naamani kabisa jamaa wa intelijensia ya Tanzania (Usalama wa Taifa = UWT/ Tanzania Intelligence & Security Service = TISS), wanapitia pitia kwenye blogu na mitandao ya jamii. Tafadhalini mkiisoma hii, ifikisheni kwa wanaohusika ifike kwa wakuu wa nchi. Tunaona uchungu na nchi yetu na tunaitakia mema Tanzania nchi yetu ya amani na utulivu.
Mungu ibariki Afrika
1.
Mungu ibariki Africa
Wabariki Viongozi wake
Hekima Umoja na Amani
Hizi ni ngao zetu
Afrika na watu wake.
Wabariki Viongozi wake
Hekima Umoja na Amani
Hizi ni ngao zetu
Afrika na watu wake.
Kibwagizo:
Ibariki Afrika
Ibariki Afrika
Tubariki watoto wa Afrika.
Ibariki Afrika
Tubariki watoto wa Afrika.
2.
Mungu ibariki Tanzania
Dumisha uhuru na Umoja
Wake kwa Waume na Watoto
Mungu Ibariki,
Tanzania na watu wake.
Dumisha uhuru na Umoja
Wake kwa Waume na Watoto
Mungu Ibariki,
Tanzania na watu wake.
Kibwagizo:
Ibariki Tanzania
Ibariki Tanzania
Tubariki watoto wa Tanzania.
Ibariki Tanzania
Tubariki watoto wa Tanzania.
Wenu mdau wa blogu hii,
Jamaldeen T. Kandahar Bin Mazar E Shariff Ibn Zenjibari
Barua pepe: jamaldeenshariffzenjibari@gmail.com
1 comment:
Yeeeeeeeeessssss! Jamaldeen!
Thanx
Post a Comment