Vurugu za Mbarali
KUNA vurugu zimeripotiwa kule kwetu Mbarali. Kijana mmoja amepoteza uhai kwa kupigwa risasi ya kichwa na ubongo kufumuka. Mwingine amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi ya kiuno. Kosa lao: Kuhoji mamlaka.
Mbarali ni kwetu. Nimefika Mbarali mara kwa mara. Nimewasikia wanaMbarali wanaonung'unika. Nimeandika makala kadhaa kuelezea kilio cha wanaMbarali. Kwangu mimi, kilichotokea Mbarali ilikuwa ni suala la wakati tu. Na mamlaka husika zisipolifanyia kazi haraka hili la Mbarali, nahofia madhara zaidi kutokea.
Sasa kule Mbarali kuna marufuku ya magari makubwa kufika Rujewa na Ubaruku kusomba mazao kwa vile yanaharibu barabara. Marufuku hiyo ina karibu mwezi mmoja sasa. Hali hiyo inamfanya mkulima wa mpunga Mbarali kuuza kilo yake ya mchele kwa shilingi 650 mpaka 700 badala ya elfu moja.
Wachuuzi wa mchele wanadai wanafidia gharama ya kukodi magari madogo kusomba magunia ya mchele mpaka barabara kuu pale Igawa. Mkulima huyu kwa kuuza kilo ya mchele kwa shilingi mia saba ina maana ya kupunjika zaidi. Faida yake ukitoa gharama zote inabaki kuwa shilingi mia au hata shilingi 80 kwa kilo. Mkulima huyu anahitaji kumsomesha mwanawe pia.
WanaMbarali wanashangaa na kuhoji, ipigwe na wakati huo huo wanaona malori makubwa ya mafuta yanapita barabara hiyo hiyo kupelekea mafuta kwa wenye biashara hiyo. Ndio sababu ya baadhi wenye hasira, juma la jana wakafikia hatua ya kusimamisha lori na kuhoji. Wenzao wakapigwa risasi.Ndipo wananchi kwa hasira wakachoma moto lori na kituo cha mafuta. Ndiyo, kilichofuatia ni majonzi makubwa.
Tunalaani tena mauaji yale yaliyofanywa na polisi wetu. Bomu la machozi lilitosha kuwatawanya waliokusanyika badala ya kutumia risasi za moto. Kulikoni jeshi la polisi?
Na sasa kuna taarifa zinatolewa. Kuna ya ukweli, kuna ya kupotosha. WanaMbarali wanaujua ukweli. Wana kilio. Ni kilio cha haki. Wanahitaji mtu wa kwenda kuwasikiliza. Autafute ukweli. Kisha itafutwe suluhu ya mgogoro unaofukuta kabla maafa makubwa zaidi hayajatokea. Inahusu ardhi. Mashamba yao, binafsi na ya umma yaliyouzwa kwa wawekezaji katika hali ya utata. Wawekezaji wanaowanyanyasa wanaMbarali ikiwamo kuwafungia wananchi maji ya mifereji kwa mashamba yao ya mpunga.
Ndiyo, inahusu hali za wakulima na wafugaji wa bonde la Usangu. Serikali iingilie kati sasa kuwasaidia watu wake wa Mbarali badala ya kuwalazimisha kuchukua hatua wenyewe. Na nimepata kuandika, kuwa kamwe huwezi kuyazuia maji yatokanayo na chemchemi kwa kumwagia mchanga.
Na kuna namna mbili za mwanadamu kuula mkate, ama aukate slesi kwa maana ya vipande vipande, au aufakamie. Hilo la mwisho hufanywa na mtu mlafi, mtu mchoyo. Mtu mbinafsi.
Watanzania tuna bahati mbaya ya kuwa na baadhi ya viongozi wenye hulka za kibepari miongoni mwa jamii ya watu wengi wanaoishi maisha ya kijamaa. Viongozi wenye kuendekeza tamaa ya mali na hata kufikia kuwatelekeza wananchi wanaowaongoza.
Naam. Kwa Serikali kubinaifsisha yaliyokuwa mashamba ya taifa ya mpunga; Kapunga na Mbarali, kisha waziri mhusika, mwaka 2006 kujibu manung’uniko ya wananchi kwa kuwaambia “Serikali imeuza chake”, ni sawa kabisa na kujaribu kuzuia maji ya chemchemi kwa kumwagia mchanga. Manung’uniko ya wananchi hayakupungua, yanaendelea kutolewa. Ni chemchemi ya ukweli, haikaushwi kwa kumwagia mchanga.
Kule Mbarali wananchi wana kilio cha haki. Wamebaini dhuluma waliyofanyiwa na Serikali yao kwa kushirikiana na wanaoitwa wawekezaji. Pamoja na kuwa zaidi ya ekari elfu saba ( 7000) za mashamba ya mpunga ya iliyokuwa NAFCO kubinaisishwa wawekezaji ama wachukuaji hao wa mali ya umma wamefikia hatua ya kuchukua maeneo nje ya mipaka ya yaliyokuwa mashamba ya NAFCO. Wameingia kwenye maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakijilimia mashamba yao ya mpunga. Wakulima wa Kata za Songwe, Rujewa na Ubaruku leo ni mfano wa wanaoishi kwa mashaka kwenye bonde la Usangu. Walichofanyiwa ni dhuluma kubwa. Ni uonevu mkubwa. Umefanywa mchana wa jua kali.
Wananchi wa Mbarali wanajiuliza, wameikosea nini Serikali yao? Miaka ya sitini wazazi na babu zao waliambiwa waondoke kwenye maeneo ya makazi na mashamba yao ili wapishe mradi mkubwa wa Taifa wa kilimo cha mpunga. Walikubali. Si tu kukubali na kukaa kando, walishiriki kwa hali na mali kufanikisha mradi huo.
Serikali ilipoamua kubinafsisha mashamba hayo, walitarajia wangepewa nafasi ya kuingia ubia na wawezekaji kupitia vyama vyao ya ushirika. Hilo halikutokea. Mawaziri wale wawili wakishirikiana na vingozi a Wilaya walikuwa mstari wa mbele kufanikisha zoezi lililowanyima haki wananchi.
Kimsingi, uamuzi wa kubinaifsisha mashamba ya Kapunga na Mbarali ulikuwa ni uamuzi wa makosa na ulioharakishwa kwa sababu za kutanguliza maslahi binafsi ya viongozi walioongoza zoezi hilo. Na historia itawahukumu wote walioshiriki na wanaondelea kushiriki kuitenda dhuluma hii kwa wananchi.
Uamuzi wa makosa wa kuyabinafsisha mashamba ya mpunga ya Kapunga na Mbarali umesababisha kuporomoka kwa uchumi wa Mbarali. Mathalan, mji mdogo wa Rujewa uliokuwa ukikua kwa kasi sasa umeanza kusinyaa. Shughuli za kiuchumi zimepungua. Hakuna mzungunguko wa fedha kama zamani. Umasikini wa kipato umeongezeka.
Na si tu uchumi wa watu wa Mbarali unaporomoka kutokana na ubinaifshaji huu kipofu, bali hata umaarufu wa chama tawala, CCM nao unaporomoka miongoni mwa wanaMbarali.
Katika nchi zetu hizi, ufisadi hujificha katika zinazoitwa sera za serikali kama hii sera ya ubinafsishaji. Ndani ya ubinafsishaji huu kuna ufisadi uliojificha. Akili ya kawaida inatuambia, kuwa hakuna mantiki ya kuwanyima haki ya kumiliki mashamba wazawa walioonyesha uwezo mkubwa wa kuendesha kilimo endelevu na kutoa mazao mengi yenye kuyajaza maghala ya vyakula.
Tangu mwaka 2001 wananchi wa Mbarali wameomba kutaka kuyamiliki mashamba ya iliyokuwa NAFCO. Sababu za kuyamiliki mashamba wanazo, nia ya kufanya hivyo wanayo na uwezo wa kuyamiliki mashamba hayo wanao. Kinachokesekana ni dhamira ya kweli kutoka kwa wanasiasa na watendaji wengine ya kuwamilikisha mashamba hayo wananchi.
Kwa kiasi fulani, hii inachangiwa na ufisadi. Na tujiulize, wakati wananchi wa Mbarali hawajaonyesha kushindwa kuyamiliki na kuyaendesha mashamba hayo, iweje leo waje kumilikishwa wengine kirahisi tu?
Tufanye nini?
Kama Serikali inavyofanya katika maamuzi mengine yaliyofanyika nyuma na yaliyo na mapungufu, haina budi kupitia upya uamuzi huu wa kuyabinaifsisha mashamba ya Mbarali.
Tujiulize, hivi ni wawekezaji gani hawa wanaokuja kuwekeza wakati tayari mashamba yapo na miundo mbinu imeshatayarishwa kwa nguvu za serikali yetu, nchi rafiki ya China na wananchi wetu? Ni wawekezaji gani hawa wanaokuja kuvuna kilichopandwa?
Nchi hii ina mabonde ya maji makubwa tisa. Kwanini wasiende kuwekeza kwenye mabonde ambayo hayajaendelezwa kama lile bonde la Ziwa Rukwa? Wananchi wa Mbarali bado wana imani ya kilio chao kusikilizwa. Kwamba dhuluma hii wanayofanyiwa ikomeshwe, sasa.
Maggid Mjengwa
Alhamisi 20 Januari 2011
1 comment:
Mambo vipi! Karibu Tanzania!
Post a Comment