Tuesday, April 19, 2011

Goodluck Jonathan ashinda uchaguzi wa Naijeria

Tume ya uchaguzi ya Nigeria Inec imemtangaza rasmi Goodluck Jonathan kuwa rais baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.

Bw Jonathan ametangazwa mshindi baada ya kupata kura milioni 22.5. Awali ghasia zilizuka kaskazini mwa Nigeria wakati matokeo ya awali ya urais yakionesha Goodluck Jonathan akielekea kushinda.

Nyumba za wafuasi wa Bw Jonathan, mgombea anayetetea kiti cha urais, zilishambuliwa katika miji ya Kano na Kaduna.

Wafuasi hao wanahisi uchaguzi umevurugwa katika baadhi ya maeneo upande wa Kusini.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa kuna watu waliokufa katika ghasia hizo.

Rais Jonathan ametoa wito wa kuwepo kwa hali ya utulivu, akisema "Hakuna mwanasiasa mwenye thamani ya kumwaga damu ya Wanigeria".

Huku kura karibu zote zikiwa zimehesabiwa, mgombea wa chama cha PDP Goodluck Jonathan - anayetokea eneo lenye Wakristo wengi na lenye mafuta la Niger Delta - ana kura karibu mara mbili ya mpinzani wake mkuu.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Muungano wa Afrika wamesema uchaguzi wa Nigeria ni mzuri kuwahi kuonekana kwa miaka mingi. BBC



No comments: