| |
Sunday, 10 April 2011 07:25 | |
Freddy Macha LABDA si wasomaji wengi wa Kiswahili wanaomfahamu mwandishi wa habari wa siku nyingi aliyefariki dunia wiki iliyopita, Adam Lusekelo Mwakang’ata. Nilimfahamu Lusekelo mwaka 1970 wakatu tunasoma wote sekondari. Tulimkatia jina la mbabe mpiganaji, yaani Njinja Maloni. Adam “Njinja” alikuwa bondia na baadaye kujifunza Shotokan karate ( toka Korea) wakati akisomea uandishi wa habari, Nairobi. Aliwahi pia kupanda mlima Kilimanjaro mara kadhaa. Bahati mbaya alipoacha mazoezi na kujisahau (kwa pombe kupindukia ) akakumbwa na kisukari. Nikiwa rafiki yake wa utotoni nilishtuka nilipomwona alivyokonda mara ya mwisho mwaka juzi, mjini Dar es Salaam. Ulikuwa mfano wa tabia yake ya masihara yaliyojaa ujumbe. Usingeacha kucheka ulipokutana na Adam Lusekelo. Alikuwa chizi kupindukia na ucheshi wake ulijionyesha katika mamia ya makala za kejeli alizoziandika katika safu ya “With A Light Touch.” Miaka ya mwisho alifungua pia blogu (“Adam Lusekelo On Line”) aliyoendeleza mada zake. Adam Lusekelo hakuwa mwoga. Ingawa marehemu babake alikuwa zamani katika serikali (tulipofahamiana 1970, Mzee Aaron Mwakang’ata, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha), Adam hakuhofia kuwasakama viongozi mafisadi. Kinyume cha baadhi ya watoto wa vigogo wanaofunga macho na kufaidi matunda ya wazazi wao, alitumia nafasi hiyo kukemea ufuska. Novemba 14, 2010 aliandika : “Jini Hatimaye Limeamka” ..akichambua namna vijana wa Kitanzania walivyochoshwa na wanasiasa waongo. “Hao wanaolifanya Bunge hoteli ya kupangisha yenye hewa safi ya baridi itabidi waamshwe na kupigwa mateke makalioni. ” Adam aliandika mada za kila aina, ikiwemo kumshauri mwigizaji Steve Kanumba aliyesutwa kwamba hajui Kiingereza alipoingia Big Brother Afrika Kusini, 2009. Kinachofurahisha, makala hii ni namna anavyochangamsha hoja akitumia Kiingereza chepesi. Kinyume cha waandishi wanaojifaragua kwa lugha ya mawe, iliyojaa maneno magumu, aliandika sentensi fupi za utani, utani... Anamkumbusha Kanumba juu ya watu wengi kukuonea wivu hasa mtu anapofaulu katika maisha. “Ukibahatika kufahamika, wapambe watataka kuimanya hata rangi ya chupi yako,” anasema. Hata mwanamke unayekwenda naye atachunguzwa. “Wataanza kusema sura yake mbaya kama jini, kwamba miguu yake mirefu kama ya twiga. Ndo’ ubinadamu huo.” Adam Lusekelo aliendeleza lugha ya uandishi Tanzania akitumia Kiingereza safi chenye utamaduni wa Afrika Mashariki. Unapokisoma Kiingereza chake ni kama kumsikiliza Mswahili akiongea lugha fasaha ya kigeni bila kujisahau atokapo. Anakumbusha enzi Mzee John Malecela alipokuwa balozi wetu Umoja wa Mataifa akiongea Kiingereza fasaha cha lafidhi ya Kigogo na Kiswahili. Siri ya ujuzi wake nini? Kila nilipoongea naye, Adam, hakuacha kunitajia kitabu fulani alichokuwa akisoma; alikuwa mwanafunzi mzuri wa fasihi na lugha, jambo linalozidi kudhoofika miongoni mwa waandishi chipukizi leo Bongo. Ucheshi wake kiuandishi uliimarika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipoandika kejeli katika “ Punch”. Alifichua tabia mbalimbali za wanafunzi akiwaudhi baadhi na kufurahisha wengine. Alijiunga pia na kikundi cha tamthiliya, Paukwa akashiriki igizo kali la kisiasa (Ayubu) lililoangalia mazingira magumu ya Tanzania , mwaka 1983. Utani utani wake ulistawi alipoingia, Daily News. Wakati huo nilikuwa naandika safu ya Jumapili (“Cultural Images”) na kuwasikia waandishi wa habari wakinong’oneza namna Adam alivyowasanifu. Alinidokezea kuwa lengo lake lilikuwa kukemea ulimbukeni. Mtanzania mwanamuziki mkazi Norway, Nasibu Mwanukuzi (aliyefanya naye kazi Daily News) anasema alimshangaa Lusekelo alivyokuwa tofauti, kitaaluma. “Alijua kupiga taipu kutumia vidole vyote (“touch method”) badala ya viwili kama waandishi wengi wa habari wanavyokuwa.” Mwaka 1984 nchi yetu ilifikia kilele cha tatizo la uhaba wa bidhaa madukani baada ya vita vya Idi Amin, 1979. Wananchi walilazimika kuhonga au kupiga foleni kupata vyakula adimu. Wageni na vigogo tu ndio hawakudhurika wakiendesha magari ya fahari na namba zilizoanza na “TX”. Adam aliandika namna nchi ilivyoshabikia tabaka la ma-TX, huku ikidhulumu hohehahe kwa unafiki wa eti kujenga Usawa na Ujamaa. Kipindi hicho hicho alibahatika kwenda Libya katika tamasha la sanaa na kikundi cha Paukwa. Aliandika namna ambavyo haikuruhusiwa kunywa pombe huku akifichua pia taswira ndogo ndogo za kinafiki alizoziona ikiwemo kuwanyima wananchi haki ya kusema. Ni miaka 27 iliyopita na sasa tunashuhudia harakati za kudai haki nchini Libya. Ama kweli aliona mbali. Kuna wakati Adam alifanya kazi idhaa ya habari ya BBC hapa London. Makala zake zilielezea hali ya hewa ya baridi na tabia za wakazi Majuu kutowasiliana kirahisi. Ilimpa taabu sana, hasa kwa kuwa alizaliwa na ugonjwa wa pumu. Mara ya mwisho nilipozungumza naye katika simu mwaka jana aliniambia kuwa hapendi Majuu. “Mi na baridi hatupatani. Nawaachieni nyinyi huko...” Kama rafiki wa utotoni nilisikitishwa maana nilitegemea Njinja Maloni angeendelea kupigana ngumi, kukimbia mbio za jogging, kupanda Kilimanjaro na kujiangalia kiafya. Hili ni fundisho kwa vijana na Watanzania wenzangu kuijali miili yetu, kufanya mazoezi ya viungo huku tukipambana na maisha magumu. Kufa ni kudra ya Mungu ila vile vile wajibu wetu wanadamu. Maisha magumu leo Bongo kuliko miaka 40 iliyopita hivyo inatubidi tuwe makini na kujiangalia wenyewe. Sitakosea kusema Adam Lusekelo alitumia ngumi zake kuandika makala kali zilizojaribu kuupinga uongo wa ngazi za juu bila kuogopa kukejeli maafa yanayokabili maendeleo yetu. Pia sichelei kupendekeza: iwapo marehemu angeendelea na michezo labda angekuwa kama Madiba Mandela ambaye bado hai kutokana na kufanya mazoezi maisha yake yote hata akiwa jela. Kufa si jambo zuri ingawa wote kitatufika. Ila kifo cha watu waliojitahidi kufanya mambo ya maana chaweza pia kutukumbusha masuala fulani. Mungu aiweke roho yake Adam “Njinja Maloni” Lusekelo peponi. Amina. -London, Jumanne, 5 Aprili, 2011. -Email: kilimanjaro1967@hotmail.com -Web: www.freddymacha.com Chanzo: Gazeti la Mwananchi |
Sunday, April 10, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment