Monday, April 04, 2011


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kufuatia kifo cha Mwandishi wa Habari maarufu, Adam Lusekelo kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili siku ya Ijumaa tarehe 1 Aprili, 2011 kutokana na ugonjwa wa kisukari.


Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu vema Marehemu Adam Lusekelo kwa jitihada zake kubwa za kuendeleza Taaluma ya Uandishi wa Habari kwa kuandikia magazeti mbalimbali hapa nchini yakiwemo magazeti maarufu ya Serikali ya Daily News na Habari Leo.“Ninamkumbuka zaidi Marehemu Lusekelo kwa safu yake maafuru ya “The Light Touch” iliyokuwa na mafundisho muhimu kwa jamii yetu”, amesema Rais Kikwete na kuongeza, “Kifo cha Marehemu Adam Lusekelo ni pigo kubwa kwa Taaluma ya Uandishi wa Habari na Wanahabari wenyewe hapa nchini, na kimeacha pengo kubwa katika Taaluma hiyo ambalo si rahisi kuzibika”.

Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete ametoa pole kwa familia ya marehemu Lusekelo kutokana na kuondokewa na mpendwa wao ambaye amesema alikuwa mhimili madhubuti na tegemeo kubwa kwa ustawi wa familia.

Aidha, amesema yeye binafsi yuko pamoja na familia ya marehemu Lusekelo katika maombolezo ya msiba huo mkubwa, na amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya Marehemu Adam Lusekelo.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
03 Aprili, 2011



No comments: