Friday, August 26, 2011

Mkanganyiko Wa Leo; Kipi Kimemkuta Jairo?


Ndugu zangu, 

Nchi yetu sasa imekumbwa na masika ya habari, imekuja na mafuriko pia. Ndio,  kuna tuliofunikwa na  mafuriko ya habari, hatujui ni ipi ya kuanza nayo.

Lakini,  hili sakata la Jairo na Bunge ni burudani pia. Tafsiri yangu inakuja siku sijazo. Nimeona nianze na mkanganyiko huu; najiuliza, hivi Jairo kapelelekwa likizo, kasimamishwa au kapumzishwa?

Si tuliambiwa kuwa Jairo alikuwa kwenye likizo fupi ya malipo? Juzi hapa karudishwa kazini kwa mbwembwe, au tuseme kakatishwa likizo yake na Katibu Mkuu Kiongozi. Na sasa karudishwa kwenye likizo ndefu na Mheshimiwa Rais!

Ni likizo ndefu kwa vile itasubiri mpaka Kamati Teule ya bunge imalize uchunguzi wake, si leo, si kesho. Maana, ripoti ya uchunguzi itasomwa na kujadiliwa bungeni Novemba mwaka huu. Ndio, mwezi kabla ya Krismasi na kufunga mwaka. Hivyo tunaweza kusema; likizo ya Jairo inaweza kuunganishwa na likizo yake ya Krismasi.  Huu ni mkanganyanyiko, au?

Na vipi hao watumishi wanaosukuma gari la Jairo?  Yaonekana walichukua ' Mapumziko mafupi' . Wakaacha ofisi zao na kwenda kusukuma gari la Jairo. Au labda walikuwa wanakwenda kazini na njiani wakaliona gari la Katibu wao Mkuu, kisha wakaitana na kuanza kulisukuma!

Na aliyechangisha fedha za maua ya kumkaribisha Katibu Mkuu naye aliacha ofisi yake na kupita kila idara kuchangisha, au? 

Na Utumishi wa Umma una miiko na maadili yake. Inasemwa; Goverments will come and go, but civil servants will stay. Ndio, Serikali huja na kuondoka, lakini utumishi wa umma hubaki pale pale.

Ni kukiuka miiko na maadili ya Utumishi wa umma  kwa jamaa hao pichani kuacha kuutumikia umma na kumtumikia mtendaji wa Serikali, tena kwa kusukuma gari lake! Tunajua, kuwa Civil servants nao ni binadamu; wana ushabiki wa Simba na Yanga, Man United na Chelsea, CCM na Chadema na mengineyo. Lakini, weledi kwa maana ya profesionalism  ni kuweka ushabiki kando na kufanya kazi ya utumishi wa umma, kwa serikali yeyote iwayo, ali mradi imechaguliwa na wananchi.

Na Ngeleja nae kwenye picha ndogo? Naye ni habari, ni burudani pia. Lakini, hata kwenye football kuna half time.  Twendeni kwenye ' mapumziko' mafupi! Vinginevyo, tutapelekwa ' likizo ndefu'- Isiyo na malipo itakayopelekea ' pumziko la milele'!

Maggid, 
Iringa.

No comments: