Tuesday, August 09, 2011


NA HARUNI SANCHAWA

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Frank Kakobe amepanda katika Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwakilishwa na Wakili Mariam Majamba ambapo amewachambua wachungaji waliomshitaki na kumlalamikia kuwa amefuja fedha, shilingi Bilioni 14 kanisani hapo.

Kampuni hiyo ya uwakili imeingia Mahakama Kuu ikiwa na nyaraka mbalimbali ilizoziwasilisha wiki iliyopita ambapo imekanusha mashitaka yote waliyopeleka walalamikaji, Wachungaji Dezidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma katika kesi namba 78 ya mwaka 2011.

Katika utetezi wake wa kimaandishi aliousaini Julai 29, mwaka huu kabla ya kuufikisha mahakamani (nakala tunayo), Askofu Kakobe amesema Mchungaji Patrick alisimamishwa kuwa mwanachama wa FGBF na Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo tangu Septemba 10, 2010 kutokana na tuhuma za ufujaji wa mamilioni ya shilingi katika Kanisa la Mafinga.

Kakobe amesema Mchungaji Mutasingwa alisimamishwa uanachama wa kanisa lake na Bodi ya Wadhamini tangu Julai 6, 2010 kwa kuanzisha Kanisa la Ukombozi ndani ya FGBF na Mchungaji Kaduma amedai alisimamishwa Machi 3, 2010 na alianzisha Kanisa la Voice of Victory.

Ameiambi mahakama kuwa mlalamikaji namba moja alikuwa na mpango wa kumpindua kutoka katika nafasi yake na njama za mkutano wao kurekodiwa na kuandikwa katika magazeti na kwamba ushuhuda wa CD na gazeti atapeleka mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, hali inayoonesha itakuwa gumzo.

Aidha, amekanusha madai yote ikiwa ni pamoja na kughushi Katiba ya FGBF na amesema atawataka walalamikaji kuleta ushahidi mahakamani hapo wakati wa usikilizwaji wa kesi utakapoanza.

Amesema kanisa lina katibu mkuu, mweka hazina na bodi mpya ya wadhamini kinyume na madai ya walalamikaji walioiambia mahakama kwamba watu wa vyeo hivyo hawapo.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Augustino Shangwa aliyewatahadharisha walalamikaji kuwa wafute kesi hiyo kwani kwa jinsi alivyoona wanaweza kushindwa na kujikuta wakilipa mamilioni ya shilingi, imeahirishwa hadi Septemba 5, mwaka huu.

Kutoka Global Publishers

No comments: