Friday, November 18, 2011

Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania au Tanganyika?

Evaristy Masuha

LEO katika kona hii ya Upembuzi wa Kihistoria nimeamua kuandika vile ambavyo wasomaji wamekuwa wakiniuliza.

Kwa hakika maswali hayo ndiyo yameibua hoja hii ya kutaka kujua kama kweli Watanzania wameelimishwa juu ya tukio hili ambalo kwa hivi sasa zinafanya kuwe na shamrashamra kila sehemu.

Wingi wa maswali hayo ndio umenifikisha katika kufanya utafiti wangu wa kienyeji kabisa kupitia vyombo ya habari ikiwa ni pamoja na wataaluma wa vyombo hivi.

Wapo wanaotambulisha tukio hili kama miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, wakati wengine wakiliita miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, wakati wengine wakisema miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Kituko cha mwisho kabisa katika mkanganyo huu ni Pauline Kazana, mmoja wa wafuatiliaji wa kona hii akiwa huko kisiwani Nyamguma, Kibara Bunda aliyewahi kujadiri nami mada hii kwa simu huku akisimama katika kupingana na wale wanaouita uhuru wa Tanzania, wakati yeye anaamini uhuru huu ni wa Tanganyika.

Msimamo wa awali wa Kazana ulisimama katika ukweli kwamba, Tanzania ni zao la muungano wa nchi mbili kati ya iliyokuwa ikiitwa Tanganyika na ile ile ya Zanzibar, tukio lililofanyika Aprili 26 1964.

Kwake yeye kwa vile Tanganyika ndiyo ilipata Uhuru mwaka 1961, basi haikuwa sahihi kusema Uhuru wa Tanzania ambayo ina miaka 47 leo hii tangu mwaka 1964 zilipoungana Tanganyika na Zanzibar.

Ni wazi kwamba kwa muda wote huo Kazana anaamini mawazo na fikra zake, alikuwa hajafuatilia vizuri vyombo vya habari vinavyoripoti tukio hilo.

Hivi karibuni ndio akachanganyikiwa kabisa baada ya kuchunguza vizuri moja ya vipindi vya runinga ambapo bendera moja inaonekana ndani yake kuna neno 50 kuashiria tukio lenyewe.

Kwa mujibu wa maelezo yake ambayo amelazimika kupiga simu akinijulisha juu ya kufuta kauli yake, huku akibaki kinywa wazi pasipo kujua tukio lipi ambalo amekuwa akilishadidia kwa muda mrefu ni pale alipogundua kwamba bendera ile inayoonekana si bendera ya Tanganyika ilipoyapata uhuru mwaka 1961, bali ni bendera ya nchi ya Tanzania iliyoanzishwa baada ya muungano wa nchi mbili.

Anasema kwa uelewa wake, kama tukio lingekuwa ni kumbukumbu ya miaka 50 ya Tanganyika, alitegemea kuiona bendera ya Tanganyika ambayo rangi yake ni kijani kwa juu ikifuatiwa na njano wakati rangi nyeusi inakuwa kubwa zaidi katikati.

Chini yake inafuatia rangi ya njano wakati kijani tena inamalizia kwa chini.

“Bwana mpembuzi, mbona hii bendera ni ya Tanzania na si Tanganyika ambayo nimekuwa nikiamini kwamba ndiyo inabeba tukio lenyewe?” anahoji.

Hilo lilikuwa swali la Kazana huku akiwa amekwama kuelewa kipi ni kipi?

Kwa tathimini hiyo fupi ni kweli kwamba Watanzania hawajui uhalisia wa tukio hili. Wapo wanaoamini kwamba tukio hili ni kumbukumbu ya watu wa bara wakati wengine wakiamini ni tukio la Watanzania wote.

Kwa upande wa historia Watanzania wanaelewa kabisa historia kwamba Tanganyika ilikuwepo siku nyingi hadi Desemba 9, 1961 ilipopata uhuru kutoka kwa Mwingereza.

Baada ya tukio hilo, jirani yake ambao ndiyo iliyokuwa Zanzibar nao wakaendesha mapambano yaliyowafikisha katika uhuru kwa njia ya mapinduzi.

Tukio hili likiwa limefanyika Januari 1964, miezi mitatu baadaye ndipo wakaunganisha nchi hizi na kuipata Tanzania.

Kwa kuitambua historia hiyo ndipo wanapotumia elimu yao hiyo kupiga mahesabu yanayowafikisha katika umri wa miaka 47 tu kwa ile inayoitwa Tanzania, wakati kwa Zanzibar ni miaka hiyohiyo wakati Tanganyika ambayo kwa sasa haipo ndio inakuwa na miaka 50.

Kuna haja ya kuwaelemisha Watanzania kabla ya kilele cha tukio lenyewe.

Kutoka Tanzania Daima 


No comments: