Saturday, December 24, 2011

Mafuriko ya maji Dar es Salaam wiki hii



Kumbe Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa tahadhari Septemba mwaka huu?


Gazeti la Mwananchi Septemba 8, 2011


MAMLAKA ya Hali ya Hewa (TMA), imetabiri sehemu kadhaa za nchi yetu kukumbwa na maafa makubwa yakiwamo mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu mkubwa wa miundombinu na mazingira wakati wa mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza mwezi huu hadi Desemba.
   
Mbali na sehemu hizo kukumbwa na balaa hilo, TMA imeonya pia kuwa, baadhi ya maeneo ambayo hayatakumbwa na maafa ya mvua hizo za vuli yanatarajiwa kukumbwa na uhaba  wa chakula kutokana na kupata mvua chini ya wastani.
Kwa maneno mengine, wananchi wa sehemu hizo za nchi yetu watakabiliwa na njaa.
   
Hizi bila shaka siyo habari njema hata kidogo, hasa kwa kutilia maanani kwamba nchi yetu imekabiliwa na janga la ukosefu wa umeme kwa muda mrefu sasa ambapo uchumi wake umeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na sekta nyingi, zikiwamo biashara na viwanda kufanya kazi chini ya uwezo wake. Janga la ukosefu huu wa umeme limerudisha nyuma juhudi za wananchi kuondokana na umaskini.
   
Pamoja na kwamba taarifa hiyo ya TMA ni ya kuhuzunisha, tunadhani hatuna budi kuipongeza mamlaka hiyo kwa kuhadharisha serikali na wananchi mapema ili iwekwe mikakati stahiki ya kukabiliana na maafa hayo. TMA kwa mara ya kwanza siyo tu imetoa taarifa hiyo kwa kiwango cha juu cha weledi pasipo ubabaishaji, bali pia imeelezea kwa ufasaha mkubwa maeneo ambayo maafa hayo yanatazamiwa kutokea na imependekeza jinsi ya kujipanga kukabiliana nayo.
   
Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi kuwa, mamlaka zinazohusika kukabiliana na maafa na kutoa huduma za afya hazina budi kuchukua tahadhari na kufanya maandalizi ya kutosha ili kuepusha vifo na kutokea kwa milipuko ya magonjwa kama kipindupindu. 
   
TMA inatoa tahadhari katika maeneo matatu. Kwanza ni maeneo ambayo yatapata mvua zilizo juu ya wastani, kwa kuleta mafuriko yatakayoleta milipuko ya magonjwa na kuathiri mazao, mifugo na miundombinu . Eneo la pili ni maeneo yatakayokuwa  na mvua za wastani ambapo hali ya mazao na malisho ya mifugo inategemewa kuimarika. Eneo la tatu ni sehemu zitakazopata mvua chini ya wastani na ndizo zitakazokabiliwa na uhaba wa chakula.
   
Huo hakika ndiyo hasa ujumbe wa TMA kwa serikali na wananchi. Kwamba baragumu la kuashiria maafa tayari limepulizwa na serikali inashauriwa kujipanga vyema kwa kuandaa mikakati na kubuni mbinu mpya za kulinda uchumi wa nchi na ustawi wa watu wake. Huu ndio wakati wa serikali kuhamasisha Kikosi cha Maafa kwa kuhakikisha kina vifaa vya kutosha vya kisasa, kwa maana ya usafiri wa anga, barabara na majini, mahema, blanketi, madawa na zana za uokoaji. 
   
Ni bahati mbaya kwamba nchi yetu imekuwa ikipata majanga makubwa kama haya tunayoyategemea lakini yamekuwa yakijirudia kwa sababu tumekuwa hatujifunzi. Sheria haziheshimiwi na maamuzi ya serikali hayatekelezwi wala kusimamiwa. Kwa mfano, uamuzi wa serikali wa kuwahamisha watu wanaoishi mabondeni umekuwa ngonjera ya kudumu, hautekelezwi. Tutamlaumu nani iwapo mvua hizi za vuli zinazotegemewa kuanza kunyesha nchi nzima siku chache zijazo zitachukua maisha ya wananchi?
   
TMA inaonya pia kwamba sehemu kadhaa za nchi yetu, hasa Mkoa wa Mtwara, maeneo ya mashariki mwa Mkoa wa Ruvuma na kusini mwa Mkoa wa Lindi zitakabiliwa na njaa. Serikali ianze sasa kusogeza chakula katika sehemu hizo na iepuke kuchukua hatua za zimamoto za kuanza kupeleka chakula baada ya watu kuanza kufa kwa njaa.
   
Majanga yaliyotabiriwa na TMA ni mengi. Ingefaa basi serikali, kupitia Baraza la Mawaziri kukutana haraka na kufanya maamuzi magumu, yakiwamo kubuni njia za kupata fedha za kukabiliana na maafa hayo na kuandaa mpango mkakati wa kuhamisha haraka watu wanaoishi mabondeni.

1 comment:

Anonymous said...

Tena basi Mamlaka waliliomba baraza la mawaziri kukutana kujadili ripoti yao, lakini wapi nchi yetu inaendeshwa kiujanja ujanja haki ya Mungu!!!