Friday, December 30, 2011


Ipi ni lugha ya taifa Tanzania?


Natumaini Watanzania wote katika kila pembe ya nchi yetu ni wazima wa afya. Kama kuna baadhi wamepatwa na maradhi nawaombea kwa Mungu waweze kupona.

Naamini kila mmoja wetu siku chache zilizopita, tuliungana pamoja kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu. Ni kweli kabisa yapo mengi mazuri, ambayo tunapaswa kuwapongeza viongozi tangu kipindi hicho hadi hivi sasa.

Leo nina mada ambayo imejificha kidogo, lakini ni muhimu ikawekwa wazi ili watanzania tukaweza kufahamu. Ni wazi kila nchi hapa dunia ina lugha yake ya taifa, lugha ambayo inatumika katika shughuli zote za kiserikali.

Mfano mzuri ukienda Kenya, lugha yao ya taifa ni Kiswahili na Kiingereza na ndio maana katika shughuli zote za mambo ya serikali, wanatumia lugha hiyo ya kiingereza na Kiswahili. Ukienda hospitali, mahakamani, shule na hata katika vyuo vya elimu ya juu, lugha inayotumika ni kiingereza tu.

Hebu tujiulize hapa kwetu Tanzania ni ipi ni lugha ya taifa? Kila mara napata wakati mgumu, ninapoona watu wakichanganya lugha - yaani Kiswahili na Kiingereza! Watoto wa mijini wanaita mchanganyiko huo wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza eti ‘kiswanglishi.’

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa lugha ya taifa hapa nchini ni Kiswahili, lakini cha ajabu watu hawakitumii inavyostahili, kutokana na madai eti wakiongea Kiswahili, wataonekana si wasomi!

Naamini kama utakuwa mzalendo halisi, utakubaliana nami kuwa Kiswahili hakipewi umuhimu, ingawa ndio lugha ya taifa; na badala yake hata viongozi wamekuwa na tabia ya kuchanganya kiswahili na kiingereza!

Mfano mzuri mara nyingi ninapokuwa nikitazama bunge letu kupitia runinga, wabunge wetu wana tabia ya kuchanganya lugha, yaani kiingereza na Kiswahili! Kwa kufanya hivyo, watanzania wa vijijini kama babu yangu, itakuwa vigumu kuelewa kwa urahisi kinachozungumzwa kutokana na mchanganyiko huo wa lugha.

Lakini pamoja na baadhi ya wabunge hao kutumia lugha ambayo si ya taifa, kiongozi wa bunge hajawahi kukemea wabunge hao! Au ndio kusema wakizungumza Kiswahili bila kuweka ‘kimombo’, wataonekana hawajafika vyuo vikuu?

Kwa upande wa baadhi vyombo vya habari kama redio na runinga, tatizo hili lipo na inaonekana ni jambo la kawaida. Unaweza kusikiliza redio ikitangaza kipindi kikiwa na jina la kiingereza, lakini kipindi ni cha Kiswahili!

Pia, kwa baadhi ya watangazaji ni jambo la kawaida kutumia maneno ya kiingereza katika vipindi vya Kiswahili, wakiamini kufanya hivyo ndio wataonekana mahiri katika kazi yao! Hii si sahihi kwani wapo wasikilizaji wengi vijijini, hawafahamu lugha hiyo ya kiingereza na hatimaye  watakosa fursa ya kuelewa kinachozungumzwa katika kipindi hicho.

Pia, kuna baadhi ya vituo vya runinga na redio, siku hizi ni kituko kabisa, kwani mbali ya kuchanganya kiingereza na Kiswahili katika vipindi vyao, lakini hata Kiswahili wanachotumia si Kiswahili fasaha!

Mfano unaweza kusikia mtangazaji akisema ‘niaje machizi wangu kila kona’. Kiswahili cha namna hiyo, naamini ni cha kihuni na ni vijana hasa wa mijini watakaoweza kukielewa, lakini kwa watu wazima na watu wa vijijini, siyo rahisi kuelewa.

Kwa upande wa tasnia ya filamu zetu hapa nchini, nako tatizo la kuchanganya kiingereza na Kiswahili, limekuwa ni jambo la kawaida. Mfano mzuri filamu nyingi wanazipa majina ya kiingereza, ingawa ndani wametumia lugha ya Kiswahili!

Binafsi sijatambua kwa nini wanafanya hivyo! Labda pengine majina ya kiingereza, ndio yanafanya filamu zao zinunuliwe! Mbali ya hilo ndani ya filamu hizo, ni jambo la kawaida kuona waigizaji wakichanganya Kiswahili na kiingereza!

Kwa tabia hii ya kuchanganya lugha, kuna baadhi ya watazamaji watashindwa kuelewa kwa urahisi kinachozungumzwa, pia wanachangia kwa asilimia kubwa kuzorotesha lugha yetu ya Kiswahili.

Hospitali nako wapo baadhi ya madaktari, wana tabia hiyo ya kuchanganya kiingereza na Kiswahili.

Niliwahi kufika hospitali moja, wakati napewa maelezo na daktari aliyekuwa akiongea Kiswahili chake cha lafudhi ya kihaya, ghafla alizungumza kiswahili huku akichanganya na kiingereza kwa msisitizo, “make sure haunywi pombe kipindi chote unachotumia dawa.”

Mitaani nako baadhi ya Watanzania wengi wasomi, imekuwa ni jambo la kawaida
kuchanganya Kiswahili na kiingereza. Wanaamini kufanya hivyo ni kujitambulisha katika jamii, kuwa wao ni wasomi wa elimu ya juu!

Ni jambo la aibu kwa msomi, kuwa mstari wa mbele kudharau lugha yake ya taifa! Hii ni dhana potovu iliyopo katika vichwa vya Watanzania wengi, wakiamini kuwa bila kuchanganya Kiswahili na kiingereza, hawataonekana wasomi.

Kujua kiingereza haimaanishi kuwa wewe ni msomi, kwani kiingereza ni lugha tu! Lugha ambayo mtu yeyote yule anaweza kujifunza na kumudu kuongea! Mfano mzuri nchi za dunia ya kwanza kama China, unapokwenda kusoma ni lazima ufahamu lugha ya Kichina na utafundishwa kwa lugha hiyo.

Hapo utatambua kuwa wenzetu wanaipa umuhimu mkubwa lugha yao ya taifa. Pia, wanaona fahari kubwa kuzungumza lugha yao tofauti na hapa ukizungumza Kiswahili bila kuweka neno la kiingereza, watu wanakuona si msomi!

Ni jukumu letu watanzania, kubadilika na kuachana na dhana hii potovu ya kuweka maneno ya kiingereza tunapozungumza Kiswahili. Naamini kila mtanzania akiachana na dhana hii, tutaweza kudumisha vema lugha yetu ya Kiswahili.

sereva20002@yahoo.co.uk (Mwananchi 29.12.2011)

2 comments:

Mtaa wa Swahili Kariakoo said...

Hapa mwandishi umenena. Ni kweli umenena. Kuna watu yaani wakizungumza lazima watie maneno ya Kiingereza kana kwamba hakuna maneno mbadala ya Kiswahili. Huwa nashangaa kweli na kushikwa na huzuni. Wengine ni kujionyesha kuwa wamesoma na wanakijua. Wengine ni kuonyesha kuwa wanakijua!!!

Kutoka Luton town said...

Utafikiri ukizungumza Kiingereza ndio basi tena. Kama mwandishi alivyoandika kuwa - Kiingereza ni lugha kama lugha nyingine yoyote. Mtu yeyote anaweza kujifunza na kumudu kukizungumza hata kama hakusoma. Mbona kuna watu mathalani Uingereza wanakizungumza ni watu wa kawaida. Hatusemi watu wasijifunze na kukijua au wasikizungumze, la hasha kizungumzwe pale kinapopaswa. Na Kiswahili kizungumzwe bila kuchanganywa na Kiingereza! Mimi nimekaa Uingereza miaka 20 na bado nazungumza bila kuchanganya na Kiswahili na sijakisahau Kiswahili. Misamiato mipya najaribu kuifuatilia kwenye mitandao na ninapokuwa Bongo.