Tuesday, January 10, 2012

Barua ya msomaji kwenye gazeti la Mwananchi 10.Januari 2012



Profesa Kahigi kitetee Kiswahili Bungeni


NILIFURAHI sana niliposikia mwalimu wangu wa lugha ya Kiswahili na msomi mahiri wa lugha hiyo, Profesa Kulikoyela Kahigi amechaguliwa kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Kwangu nilifurahi kwa kuwa niliamini sasa Bunge letu limempata mmoja wa watu watakaokuwa mstari wa mbele kupigania matumizi ya lugha ya Kiswahili bungeni.

Kwa kweli hali ya sasa katika chombo hicho cha kutunga sheria inatisha, kwani asilimia kubwa ya mazungumzo kwa watunga sheria wetu yamekuwa yakichanganya na lugha ya Kiingereza. Sijui kama wawakilishi hawa wananchi wanajua kuwa, idadi kubwa ya wafuatiliaji wa mijadala ya Bunge ni wananchi amabo hawan ufahamu wa lugha ya Kiingereza. Inashangaza wao kuendelea kuzungumza huku wakitumia lugha ya kigeni.

Naomba Profesa Kahigi ajue kuwa licha ya kuwawakilisha watu wa jimbo lake na hata kulinda maslahi ya chama chake, bado ana dhima kubwa ya kuitetea lugha ya Kiswahili ambayo kwanza ndiyo iliyompa chati ya kuwa msomi gwiji hapa nchini. Kama ilivyo kwa wabunge wengine wanaosifika kwa kuwa watetezi wa ufisadi au hata posho za wabunge, namuomba Profesa Kahigi ajipambanue na aanze kuwa mtetezi wa kweli wa Kiswahili.

Awe mstari wa mbele kukemea matumizi ya Kiingereza Bungeni ili wananchi wa kawaida waweze kujua yala yanayojadiliwa na wawakilishi wao. Njia za kumwezesha kufanya hilo ziko nyingi ikiwamo kuwasilisha hoja binafsi.Kwa kweli inatia aibu kuona Kiingereza kikitamalaki katika mazungumzo ambayo wahusika wake wote wanajua Kiswahili na hata wanaowasikiliza wanaijua lugha hiyo.

Hebu wabunge wetu acheni kasumba na utumwa wa kutumia Kiingereza, na kama kweli mnadhani Kiingereza ndiyo lugha bora, basi amueni kutumia lugha hiyo siku zote na katika vikao vyote.
 

Naamini hamuwezi kufanya hivyo kwani wengi wenu hamna ufahamu wa kutosha na lugha hiyo. Sasa iweje mng’ang’anie lugha ambayo kumbe hamuijui fika? Profesa Kahigi, tumia hoja hizi kuwaeleza wakubwa wenzako huko Dodoma.

Sanura Bakar
Morogoro


No comments: