Monday, January 23, 2012


Kikwete tumekukosea nini?


Josephat Isango


HUENDA kuna mambo tumemkosea Rais Jakaya Kikwete ndiyo maana analipa kisasi. Haiwezekani Watanzania mkakataa ukweli huu, hata kama mkikataa, mbona inaonyesha kuwa serikali ya Kikwete ndivyo imedhamiria?

Kosa liko wapi, kwetu au kwake? Je, tulimchagua Kikwete kwa hasara yetu? Je, tujutie sasa kumchagua kiongozi huyo na serikali yake kuwa madarakani? Yawezekana kweli tumekosea sehemu fulani na ndiyo maana tunaadhibiwa na serikali yetu.

Je, hata serikali haina huruma ya kawaida angalau itusamehe tu? Na kama imekosa huruma inaendelea kutuangamiza hivi, mbona ni sisi ndio tulioiweka, kwani aliyeiweka hana nguvu ya kuitoa?

Aliyekusanya hana nguvu ya kutawanya? Aliyepanda hana uwezo wa kuvuna?
Unyonge wetu huu mpaka tufanyiwe haya unatokana na nini? Tuna Tanzania
nyingine kuliko hii ambayo kwa sasa tunaichezea jinsi kila mmoja anavyojisikia?

Tujikumbushe tena, labda tumesahau Nyerere alivyofundisha. Alisema kuwa: “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha.

“Ni unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, tunyanyaswe na tupuuzwe. Sasa tunataka mapinduzi ili tusionewe, tusinyanyaswe na tusipuuzwe tena.”

Mwalimu alizungumza haya akimaanisha kuwasaidia Watanzania kujitambua, alikuwa akipinga mfumo wa maisha ya aina hii, ambayo kwa sasa sisi tunayaishi, bila kuyapenda lakini tunayavumilia na yanataka kuzoeleka kuwa ndio mtindo wa kawaida kwa serikali yetu na chama kilichoiunda.

Maisha yetu yote yamekuwa yakidhibitiwa na watu ambao mtazamo wao ni kujinufaisha, kutuibia, kutukandamiza, kutulipa mishahara midogo tena hata hiyo midogo mara nyingine hatupewi au inacheleweshwa sana.

Bahati mbaya sana kwa miaka 50 tangu tupate uhuru Chama cha Mapinduzi
(CCM) ndio wamekuwa wakiamua kuwe na aina gani ya serikali, shughuli za kiuchumi – kama zipo, elimu watoto wetu wapate. Katika muktadha huu wao ndio wenye maamuzi ya mwisho. Wao ndio wamefinyanga sura ya Watanzania wa kizazi hiki.

Tumekuwa na Watanzania waliopigika kimaisha lakini wakitishiwa tunu ya Umoja na Amani ili wasipigane. Hata kama wananyanyaswa wataambiwa tusipoteze amani ya Tanzania ambayo naamini ipo kwa Watanzania wote si kwa baadhi ya watu.

Rais Kikwete, je, kuna sehemu tutakuwa tumeikosea serikali yako kiasi cha kustahiki manyanyaso haya, uonevu huu au hivi vinafanyika kwa sababu ya unyonge wetu?

Hivi unyonge wetu ndio unasababisha serikali iamue kutoza kodi kubwa kwenye mafuta, vyakula sasa bei yake haikamatiki na kadiri siku zinavyosonga ndivyo inavyoongezeka.

Serikali imeamua kutuua kidogo kidogo. Inapandisha bei ya vitu ili watakaoshindwa kuvipata wakaibe na wakiiba watu wanajichukulia sheria mkononi na kuwaua wenzao. Serikali imepandisha bei ya umeme licha ya kuwa nishati hiyo si ya uhakika na haijawafikia Watanzania wengi, serikali haitoi sababu ya kueleweka ya kupandisha umeme, haisemi kama imeongeza wafanyakazi katika sekta hiyo, haisemi kama imeboresha upatikanaji wa umeme kwa wananchi wake.

Hatuambiwi kama mashine mpya zimenunuliwa au mishahara ya wafanyakazi wa Tanesco imepandishwa lakini inasema kuwa imepandisha gharama za umeme, Je, ni kwanini, kwa ajili ya nani?

Kimsingi maamuzi haya hayajaangaliwa kikamilifu kama yanamsaidia mwananchi au yanamnyonga? Wananchi nao wamekubali kunyongwa au wanakandamizwa kimabavu kwa kuwa hawajui wajibu wao wa kuiwajibisha serikali?

Serikali ya Kikwete itaacha lini utaratibu wa kupitisha sheria, sera na matamko mbalimbali ambayo yapo kwa ajili ya kunufaisha tabaka fulani tu?

Umeme wa Tanzania unapatikana kwa kutumia nguvu za maji, makaa ya mawe na mafuta.

Suala la maji katika maeneo kunapozalishwa umeme kuna mafuriko, maana yake hakuna shida ya uzalishaji, je makali ya umeme yamepungua? Kama hayajapungua ni kwanini?

Mikataba aliyoahidi Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, wakati wa kipindi cha Bunge ilikuwa ni kuwadanganya Watanzania. Tunatofautishaje mikataba ya ukoloni iliyokuwa ya kinyonyaji na hii ya siku hizi ndani ya serikali?

Tunawezaje kumkejeli Chifu Mangungo wa Msovero, kwa kutia sahihi mkataba wa kilaghai miaka ya 1880 na kuwapa wakoloni mkataba wa miaka 99 kumiliki ardhi ya nchi yake, chini ya mpelelezi, Dk. 
Karl Peters.

Vivyo hivyo alivyofanyiwa Chifu Lobengula na Mzungu, Cecil Rhodes, huko Rhodesia. Lakini, kuna tofauti gani kati ya mikataba ya sasa kati
 yetu na wawekezaji tunaoambiwa na serikali na ule wa Chifu Mangungo na Karl Peters?

Ukweli unabaki kwamba kina Chifu Mangungo, Lobengula na Kinjikitile walipogundua wamefanyiwa hila walipambana. Viongozi wetu wasomi wa Havard wanatetea wawekezaji matapeli; inavyoonekana, mikataba ya wawekezaji hao inaandikwa na viongozi hao kwa manufaa binafsi na ya matapeli wabia wao.

Kutokana na hali hiyo, serikali ya Kikwete imeshindwa hata kudhibiti bei ya unga, sukari, mafuta na sasa imeamua kuonyesha kuwa inaweza kutufanyia lolote na sisi tusionyeshe kupinga au kuikasirikia.

Kama tunaona kinachofanywa na serikali ni kizuri, kwanini tulalamikie ugumu wa maisha na ubadhirifu wa mali za serikali unaofanywa na viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza?

Hatujui tumekosa wapi lakini serikali inatuadhibu, serikali nayo imeonyesha haina nia ya kutusamehe. Maisha ni magumu kiasi cha kutosha, nini hatima ya Watanzania?

Nimefanya mazungumzo na mfanyakazi mmoja wa kampuni ya ulinzi mkoani Singida ambaye mshahara wake ni sh 80,000 ambazo hamzitoshi hata kufikisha nusu mwezi.

“Gunia la mkaa ni sh 13,000, debe la mahindi sh 8,000, sukari kilo sh 2500, kusaga debe moja ka mahindi ni sh 1,000, mafuta ya taa lita moja inauzwa sh 2200, mchele kilo moja sh 2400, maji ya kutumia ndoo moja inauzwa sh 500, kodi ya nyumba sh 5,000, umeme sh 5,000,” anasema.

Mfanyakazi huyo anasema katika hali ya kawaida anashindwa kumudu maisha licha ya kufanya kazi aliyonayo, anauliza serikali imemkosea nini kiasi cha kuweka mazingira magumu ya kuishi kwa raia wake?

Akaniuliza kuwa kama yeye mwenye kazi na analipwa mshahara mambo anayaona magumu kiasi hicho, je, yule asiye na kazi wala kipato cha maana anaishije?

Anahitimisha mjadala wetu kwa kunihoji: “Serikali imeamua kuwakomoa wananchi wake kwa kupandisha bei ya kila kitu hata umeme ambao hatungetarajia upande katika musimu huu wa mvua?”

Serikali inanunua umeme kutoka kwa kampuni za kigeni kwa kutumia fedha za kigeni (dola), inawauzia Watanzania kwa kutumia fedha ya hapa nchini ambayo kila siku inashuka thamani kila kukicha.

Sijajua tumekosea wapi, ila mateso tunayoyapata kwa sasa ni fundisho. Siku nyingine tusikimbilie kuchagua ovyo kwa kuhongwa na kudanganywa, lakini sasa nadhani umefika wakati kwa wananchi kujua ni heri punda mzima hata kama ni wa thamani ndogo, kuliko farasi mgonjwa japo ni wa thamani kubwa. Serikali angalieni mnakotupeleka!

No comments: