Sunday, January 15, 2012

Mwalimu ageuka ombaomba Dar es Salaam

Mwalimu Saada King’ombe akiwa na watoto wake chini ya mti karibu na Viwanja vya Gymkhana, Upanga jijini Dar es Salaam. (Picha na Fadhili Akida).


Imeandikwa na Angela Semaya wa Habari Leo

MWALIMU wa shule ya msingi aliyepata kufundisha kwa miaka 19 katika shule kadhaa za mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, Saada King’ombe amegeuka ombaomba, chini ya mti na watoto wake sita huku akitegemea fadhila za wasamaria. Kati ya watoto hao, mmoja ni mchanga, akiwa amezaliwa Jumapili ya Januari mosi mwaka huu. Ana umri wa wiki mbili. Saada ambaye ana asili ya Mkoa wa Kigoma, akizungumza na gazeti hili juzi, alisema kiini cha hayo ni matatizo kazini kwake hata kumfanya awe katika mazingira aliyonayo sasa.

“Nilijikuta napoteza ajira yangu ya ualimu baada ya kufiwa na mama yangu, ikabidi niende Kigoma, lakini nilichelewa kurudi kazini nikajikuta nafukuzwa kazi, hata sijui ni wizara au nani, basi tu ndiyo hivyo kazi yangu ikaishia hapo,” alisema mama huyo mwenye jumla ya watoto wanane.

Anakumbuka wakati anapata matatizo kazini, tayari alikuwa na watoto wawili ambao kwa sasa wamechukuliwa na ndugu wa mume aliyekuwa akiishi naye ambaye kwa sasa ni marehemu. Watoto wengine sita aliwapata akiwa katika harakati za kujikwamua kimaisha, lakini kwa bahati mbaya wanaume aliokuwa na uhusiano nao kwa nyakati tofauti, waliishia kumzalisha na kumtelekeza.

Hata hivyo, Saada mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza, huku akisisitiza ana akili timamu, alisema anawakumbuka wanaume wote aliozaa nao. Aliwataja kuwa wanatoka mataifa sita tofauti, wakiwamo Watanzania, Mkenya, Mzambia, Mkongo, Mwafrika Kusini na Mgiriki.

1 comment:

Tausi Usi Ame Makame, Oslo said...

Maskini mwalimu Saada pole sana. Hivi kuna mtu anaweza kutafiti jinsi gani naweza kumpata mwalimu Saada?