Saturday, January 14, 2012

Aina ya nyoka mpya “Atheris Matildae” agundulika Tanzania





Shirika la Wildlife Conservation Society (WCS) limetangaza kugundulika kwa aina ya tofauti ya nyoka mwenye rangi ya njano na nyeusi, anayepatikana katika maeneo ya Kusini Mashariki mwa Tanzania.  Nyoka huyo amepewa jina la "Matilda's Horned Viper" au kwa kitaalamu Atheris Matildae.  Ni jina la binti mwenye umri wa miaka 7 wa meneja wa mradi wa WCS nchini Tanzania, Tim Davenport aliyeshiriki katika utafiti wa mchakato wa kufanikisha vielelezo vya nyoka huyo katika mashirika rasmi ya kuhifadhi maelezo na kumbukumbu hizo kadiri inavyotambulika duniani. Inasemekana kuwa Matilda alivutiwa na kupenda kumtizama kila mara nyoka huyo. Washiriki wengine katika utambuzi huo ni Michelle Menegon wa Museo Delle Science of Trento, Italia na Kim Howell wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Sifa kuu za nyoka huyo ambaye ana urefu wa futi 2.1 (sm 60) ni magamba yaliyoinuka na kuunda mfano wa pembe juu ya macho ndiyo sababu ya kuitwa “Horned” na vile vile nyoka huyo ana sumu, ndiyo maana pia jina lake ni “Viper”.

Watafiti hao wameficha kulitamka bayana eneo hasa anapopatikana nyoka huyo kwa minajili ya kuzuia uharibifu, wizi  na wawindaji wahalifu wanaoweza kumwinda nyoka huyo ili kupata fedha. Wanasema tayari mazingira ya eneo hilo yameshaharibiwa vya kutosha kwa shughuli za kawaida za binadamu kama vile uchomaji mkaa.

Wameazimia kumweka nyoka huyo katika kundi la wanyama walio katika hatari kubwa kabisa ya kutoweka duniani. Katika jitihada hizo, wamekwisha andaa eneo dogo kwa ajili ya kuwahifadhi nyoka hao ili kuwaruhusu kuzaliana kwa wingi.

Kwa taarifa zaidi kumhusu nyoka huyo, peruzi tovuti zifuatazo:


No comments: