Friday, February 03, 2012


SALAMU ZA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SIKU YA SHERIA TAREHE 03 FEBRUARI, 2012


Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria;
Mheshimiwa Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu;
Mheshimiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika;
Mahakimu na Watumishi Wengine wa Mahakama;


Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana:


Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kuadhimisha Siku ya Sheria kwa mwaka 2012. Nakushuru pia kwa kunipa nafasi ya kutoa salamu kwa hadhara hii ya mabingwa wa sheria na watoaji haki. Lazima nikiri kuwa baada ya kusikiliza nasaha maridhawa zilizotolewa katika hotuba yako nzuri na nyinginezo za walionitangulia mimi sintokuwa na mengi ya kusema. Hakika tumepata darasa la kutosha. Hivyo, nitasema machache.

Niruhusuni nianze kwa kutakiana heri ya Mwaka Mpya. Naungana na viongozi wa dini waliotuombea dua hapa leo hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuumaliza mwaka uliopita salama na tunamuomba atujaalie neema na baraka tele mwaka huu wa 2012. Tumuombe atujaalie ndoto zetu zitimie na tunayopanga yafanikiwe.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nakupongeza sana wewe binafsi kwa kazi yako nzuri uifanyayo ya kusimamia na kuuongoza mhimili wa Mahakama. Wahenga walisema ‘nyota njema huonekana asubuhi’. Katika kipindi kifupi ulichokuwa Jaji Mkuu umeonyesha kuwa wewe ni kiongozi mahiri na mtetezi

shupavu wa maslahi ya mhimili wa Mahakama na haki za raia. Aidha, umekuwa daraja imara kati ya mihimili yetu mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Kupitia kwako, mafanikio mengi yamepatikana na heshima na taswira ya Mahakama katika jamii inazidi kuboreka. Nakushukuru sana.

Nawapongeza, pia, Majaji wa Rufaa, Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu pamoja na watumishi wengine wote wa Mahakama. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa na nzuri pamoja na kuwepo changamoto mbalimbali. Mimi na wenzangu Serikalini pamoja na wananchi walio wengi tunatambua na kuthamini mchango wenu muhimu katika utoaji wa haki. Jitihada zenu ndizo zimewezesha Mahakama kupata mafanikio ambayo tunayazungumzia leo. Mimi naamini kuwa mwelekeo wetu wa siku za usoni unaleta matumaini makubwa.

Ujumbe wa Mwaka

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nawapongeza sana kwa mada nzuri ya maadhimisho ya Siku ya Sheria mwaka huu inayosema “Adhabu Mbadala Katika Kesi za Jinai na Faida zake katika jamii”. Kwa hakika huu ni ujumbe ambao umekuja wakati muafaka kabisa.

Jambo hili ni muhimu sana. Ni ukweli ulio wazi kwamba mfumo wetu wa sasa wa adhabu unasisitiza adhabu ya kifungo jela badala ya adhabu mbadala ambazo zipo katika sheria. Kama adhabu mbadala zingekuwa zinatolewa, idadi ya wafungwa gerezani ingepungua na hata tatizo la msongamano katika magereza lisingekuwepo au lingepungua sana.

Hatuna budi kutumia adhabu mbadala kama sheria ya The Community Act inavyoruhusu kwa makosa yanayostahili. Sheria hiyo inajenga dhana kwamba jukumu la kuwarekebisha wahalifu haliko mikononi mwa Serikali pekee na kwamba jamii wanakotoka wahalifu nayo ina wajibu wa kushiriki katika kuwarekebisha wahalifu. Sheria ya kufanya kazi ya kijamii ililenga kuwaepusha na adhabu ya kifungo wale

wafungwa ambao wameonyesha tangu awali kwamba waliteleza, wametubu na kuomba msamaha.Utekelezaji wa sheria hizi una changamoto zake ambazo Mheshimiwa Jaji Mkuu umezieleza kwa ufasaha. Moja ya changamoto hizo ni ile ya jamii kukubali ukweli kwamba wahalifu wanarekebishika. Adhabu zinazotolewa zina lengo la kumrudi na kumrekebisha mhalifu.

Inapodhihirika kuwa mwenendo wa mhalifu una muelekeo mzuri na hasa unapopima uzito wa kosa alilofanya ni dhahiri kwamba ni kwa manufaa ya mfungwa kurekebishwa na jamii badala ya kumtenga kwa kumfunga gerezani. Hii ni namna nyingine ya kumpa mhalifu fursa ya kujirekebisha katika jamii yake.

Hata hivyo, kuna changamoto ya jamii kutambua na kukubali kuwa inao wajibu mkubwa katika kusaidia kuwarekebisha wahalifu. Naelewa ugumu uliopo kwa jamii kulielewa jambo hili kwani wengi wanaamini kwamba adhabu pekee ya mhalifu ni kumfunga gerezani. Hivyo, ipo kazi kubwa ya kutoa elimu ili watu nao waelewe kuwa wanao wajibu wa kusaidia kuwarekebisha wafungwa wawe na tabia njema.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Changamoto nyingine ni jinsi jamii itakavyojipanga kufanya kazi ya kuwarekebisha wahalifu katika jamii zao. Ingefaa wadau muhimu, kama vijiji, Halmashauri na Mamlaka nyingine wabuni kazi na kutenga maeneo ya kufanya kazi zenye manufaa kwa umma. Kazi hizo zisiwe za kukwaza, bali ziwe za kuwarekebisha wahalifu. Ni muhimu kwa ajili hiyo basi, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na viongozi wengine wa Serikali za Mitaa wakahusishwa kwa ukamilifu katika utekelezaji wa adhabu mbadala. Tukifanya hivyo mpango huu utakuwa umepewa msukumo wa pekee na kupata mafanikio.

Kuhusu suala la msongamano wa wafungwa, baada ya kutembelea magereza ya Keko, Ukonga na Segerea na kuyaona niliyoyaona, nimeshawishika tuchukue hatua. Nimetoa maagizo kwa wahusika kuandaa maoni yao. Baadhi wamekamilisha na wengine wanamalizia.

Hivi karibuni tutakutana kujadili hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja kuongeza magereza, kuharakisha kusikiliza na kumaliza kesi, kupata nakala ya hukumu, kukamilisha upelelezi haraka na kuiwezesha Mahakama kwa watu na rasilimali.

Mwisho
 
Mheshimwa Jaji Mkuu,
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuzungumzia baadhi ya mambo uliyoyataja katika hotuba yako. Kwa upande wa mgao wa fedha kuwa kati ya asilimia 60 na 70 ya lengo, hilo halikuwa tatizo lenu pekee. Karibu Serikali nzima ilikuwa hivyo. Sababu kubwa ni jukumu la kulipa malimbikizo ya madeni ya mwaka wa fedha 2010/2011 ambayo tulilazimika kuyalipa katika mwaka huu wa fedha. Bahati nzuri mzigo huo wa madeni umepungua sana hivyo katika nusu hii ya pili ya mwaka wa fedha 2011/2012 hali itakuwa bora zaidi.

Aidha, napenda kukuarifu kuwa bajeti ya Mahakama, kwa maagizo yangu, imewekewa wigo wa kutolewa kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, toeni hofu kwani kile chote kilichopangwa kitapatikana. Kuhusu baadhi ya stahili za Majaji ambazo hazijalipwa suala hilo linashughulikiwa na tumefikia mahala pazuri.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Kuhusu ajira ya Majaji wapya, nasikitika kwamba imechukua muda mrefu. Taratibu za kirasimu karibu zinafikia ukingoni na bila shaka zoezi litakamilika muda si mrefu. Kwa upande wa upungufu wa Mahakimu, Serikali inalitambua tatizo hilo na nimekwishamuelekeza Waziri wa Sheria hatua za kuchukua ili mgawo wa nafasi za ajira za Mahakimu uongezeke.

Bahati nzuri hivi sasa ipo idadi ya kuridhisha ya Mahakimu waliohitimu kutoka katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama kule Lushoto. Mwaka jana nilipohudhuria Mahafali ya 11 ya Chuo na nilishuhudia jinsi Chuo kinavyofanya kazi kubwa na nzuri ya kusomesha Mahakimu wengi. Hivyo basi, tatizo la uhaba wa Mahakimu litamalizika muda si mrefu. Ni matumaini yangu kwamba ongezeko la Majaji na Mahakimu litasaidia sio tu kusajili kesi nyingi zinazowasilishwa Makahamani, bali pia litawezesha kesi zinazopokelewa Mahakamani kusikilizwa na kumalizika kwa wakati.

Baada ya kusema maneno yangu hayo mengi kwa mara nyingine tena nawatakia kazi njema mwaka huu, nawatakia kila la heri katika kuboresha mfumo wetu wa adhabu tusiwaache wananchi wetu mbali ili waukubali mfumo huu na wauunge mkono.

Asanteni kwa kunisikiliza

No comments: