Serikali kutengeneza hati mpya za kusafiria
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Khamisi
Kagasheki, amesema serikali imeanza mchakato wa kutengeneza hati mpya za kusafiria
ambazo haziwezi kughushiwa.
Kauli hiyo aliitoa bungeni jana alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Magu, Festus Limbu (CCM), aliyetaka kujua mkakati uliopo serikalini
katika kuzuia vijana wanaosafiri nje ya nchi kwa kutumia hati za kughushi.
Balozi Kagasheki alisema licha ya kuwepo kwa baadhi ya
vijana wanaotumia hati za kusafiria za kughushi lakini wapo wanaosafiri bila hata
hati hizo.
Alidai kuwa vijana wengi wanazamia na kwenda nje ya nchi
kwa malengo ya kusaka maisha bora na pindi wanapobainika hurejeshwa nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali ipo katika
mchakato wa kuhakikisha inatengeneza hati ambazo haziwezi kughushiwa ikiwamo
kuanza kutengeneza vitambulisho vya kitaifa.
Alifafanua kuwa baada kumalizika kutengeneza vitambulisho
vya kitaifa, itasaidia kubaini kuwapo kwa watu ambao si Watanzania na
kuwarejesha makwao.
Kutoka
gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment