Sunday, February 26, 2012

Taarifa kwa vyombo vya habariRais Jakaya Mrisho Kikwete amekipongeza Chama Tawala cha Botswana, Botswana Democratic Party(BDP) kwa mafanikio yaliyopatikana nchini Botswana na watu wake.

Rais Kikwete ametoa pongezi hizo katika Sherehe za Kuadhimisha Miaka Hamsini (50) ya Chama cha BDP  katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Botswana.

"Katika miaka hamsini ya uhai wake, BDP kimefanya mambo mengi mazuri nchini Botswana, katika ukanda huu na Afrika kwa ujumla na kimekuwa na historia nzuri ya kufanya mambo mengi mazuri ya kuvutia na kutolewa mfano barani kote" Rais amesema.

Rais Kikwete ametolea mfano wa Pato la ndani la Taifa la Botswana ambapo, wakati wa uhuru wa Botswana mwaka 1966, lilikuwa dola za kimarekani 70 tu, hadi kufikia dola za kimarekani 16,300 mwaka 2011.

"Haya ni mafanikio makubwa sana Barani Afrika" Rais amesema na kukipongeza kwa dhati Chama cha BDP ambacho kinatawala tangu uhuru wake.
Mapema akizungumza na wananchi Rais wa Botswana PM Gen. Seretse Khama Ian Khama ameeleza kuwa Tanzania imetoa mchango mkubwa na kuwa urafiki wa nchi mbili hizi ni wa kudumu.

"Tanzania imesimamia Uhuru, Haki na Ukweli barani Afrika" amesema na kueleza kuwa nchi yake itaendelea kusimamia na kuheshimu misingi hiyo.
Rais Khama pia amewakumbusha wanachama na wananchi wa Botswana kuwa umoja wao ndiyo ngao kubwa ya Chama cha BDP na kwamba chama hicho bado kiko imara kutokana na umoja wao huo na kinapania kuendeleza, kuuthamini na kuulinda Umoja wao.

Sherehe hizo zimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Bwana Wilson Mukama.

Rais Kikwete anatarajiwa kurejea Dar-es-Salaam kesho tarehe 25 Februari, 2012.  

Mwisho.

Imetolewa na 
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais,
Gaborone, Botswana
24 Februari, 2012

No comments: