Saturday, February 04, 2012


Taarifa ya madaktari kufuatia tamko la serikali Bungeni jana


TAARIFA YA KAMATI YA MUDA YA KUSHUGHULIKIA MADAI YA MADAKTARI KUFUATIA TAMKO LA BUNGE (ILIYOTOLEWA LEO KWENYE VYOMBO VYA HABARI);
--
Baada ya taarifa ya bunge kuwasilishwa leo ijumaa, kamati ya madaktari inaazimia haya yafuatayo;

• Kamati inalishukuru bunge la jamhuri ya muungano kupitia mwongozo wa spika kwa kuiagiza kamati ya kudumu ya huduma za jamii kuanza kazi mara moja ya kukutana na jumuiya madaktari.

• Kamati pamoja na jumuiya ya madaktari ipo tayari kukutana na kamati ya huduma za jamii.
• Kwa kuwa suala hili ni la umuhimu na dharura kubwa, Mkutano wa jumuiya ya madaktari unatarajiwa kufanyika jumamosi tarehe 04/02/2012 kuanzia saa 4 asubuhi.

• Kamati inasikitika kuwa kauli ya waziri wa afya iliyotolewa bungeni ilijaa upotoshaji mkubwa kwa jamii na wabunge na kwa kuwa busara za naibu spika zilitoa ufafanuzi kuwa kauli hiyo ni ya upande mmoja na wangependa kusikia kutoka kwa madaktari lakini kanuni haziruhusu,kamati imeona kuwa ni muhimu kufafanua baadhi ya masuala yaliyopotoshwa na ambayo hayajatolewa ufafanuzi wowote;

1. Si kweli kuwa huduma zinaendelea kama kawaida katika hospitali tajwa,kwa mfano KCMC taarifa za jana zinaonyesha kuwa hali ilikuwa mbaya sana kiasi cha kusitisha huduma zote kasoro huduma ya magonjwa ya ngozi ,hali hiyo ililazimu Askofu mkuu wa KKKT kufika hospitalini hapo kuwasihi madaktari,jambo ambalo lilishindwa kutatua tatizo. Propaganda za waziri ni msiba mkubwa kwa taifa.

2. Si kweli kuwa madaktari bingwa walikataa kwenda mikoani,taarifa ya kweli ni kuwa taratibu hazikufuatwa kabisa,badala yake kejeli na ubabe ulitumika huku madaktari bingwa wengi kati yao wakihamishwa kupitia magazetini. Mfano upo wa madaktari ambao walienda kuripoti mikoani wakasumbuliwa na kuzungushwa kupewa masurufu ya safari,hospitali ya mkoa ikimuelekeza kuwa jukumu hilo ni la wizara na wakati huo huo wakienda wizarani wanaambiwa jukumu hilo ni la mikoa.

3. Mojawapo ya madai ya madaktari ni suala la uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa na mazingira ya kazi, waziri amelikwepa na kupoteza muda wa wananchi kuzungumzia propaganda zisizo na tija.

4. Suala la bima ya afya kwa watumishi wa afya hajatolea tamko lolote.
5. Suala la uwajibishwaji wa watendaji wa wizara ya afya akiwemo yeye, amelikwepa kabisa.

6. Serikali inazungumzia na kutoa ahadi siku zote bungeni kuwa inapeleka watumishi wa afya wilayani na vijijini lakini Mh Waziri akifahamu kuwa dai mojawapo la madaktari ni kuomba serikali iingize posho ya mazingira magumu kwa watumishi wa afya wanaopelekwa maeneo ya mazingira magumu mojawapo ikiwa mikoa ya pembezoni mfano ni Rukwa anapotokea waziri mkuu, hili hajalitolea tamko wala kulizungumzia kabisa.

7. Bw Waziri ametumia muda mrefu kupiga propaganda za mshahara badala ya kusema wao wanatoa ofa gani ili tuelekee kwenye meza ya mazungumzo.

• Mwisho kabisa , jumuiya ya madaktari inaona kuwa serikali haina nia ya dhati kupata ufumbuzi wa mgogoro huu. 
--

No comments: