Thursday, March 15, 2012

Nani kamuibia Waziri Malima?

Naibu waziri; Adam Kighoma Ali Malima.


Mobhare Matinyi

Beskrivelse: http://www.freemedia.co.tz/daima/anime/amka2.gif
SUALA la kuibiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Adam Malima, si la mchezo hata kidogo kama kweli tunataka  kuheshimu utawala wa sheria na maadili kwa mtumishi wa umma kama yeye,  tena mwanasiasa.

Sasa, kwa mujibu wa vyombo vya habari, vikimnukuu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, hebu tuangalie alichoibiwa waziri huyo:

1.   Laptop tatu, aina ya Dell zenye thamani ya sh milioni 5.6.
2.   Vinasa sauti viwili vya digitali na headphone zake zote ambavyo thamani  yake ni sh milioni moja.
3.   Simu tatu, ya kwanza Nokia C6 ya sh 500,000, Nokia E200 ya sh 250,000  na  Blackberry yenye thamani ya sh milioni 5.5.
4.   Vitu vingine ni pete mbili za almasi zenye thamani ya sh milioni 2.5.
5.   Dola za Marekani 4,000 ambazo ni sawa na sh milioni 6.5.
6.   Fedha taslimu sh milioni 1.5.
7.   Kadi mbili za benki.
8.   Mabegi matatu ya nguo.
9.   Baraghashia mbili zenye thamani ya sh 50,000.
10.  Nyaraka mbalimbali za serikali.

Pia awali ilitajwa na vitu hivi:
11.  Pasipoti mbili za kusafiria (zimeokotwa jalalani karibu na hoteli).

Lakini bahati yake hakuibiwa silaha hizi, Bastola moja na bunduki iliyotajwa bila aibu kuwa ni SMG (Sub-Machine Gun).

UCHAMBUZI RAHISI
1.   Kuna element ya excessiveness kwenye orodha ya vitu hivi. Kwa maoni  yangu huu ni ulimbukeni kama wa hadithi ya zuzu aliyeshinda bahati nasibu  akaamua kununua kila kitu mtaani kwake, hadi kituo cha basi.
Waziri kwa  mishahara yetu ni mtu maskini labda kama ni mwizi.
Ndiyo, yeye ni mbunge  mwenye maposho, lakini bado alipataje mali zote hizi?
2.   Katika hali ya kawaida, mwanasiasa anasafiri na laptop tatu za nini?
Huu ni ulimbukeni wa kujua kompyuta na kuweza kuzipata kirahisi au kupewa  hovyo hovyo tu; vinginevyo nini kinaweza kuwa sababu?
3.   Vinasa sauti, je, yeye amekuwa mwandishi wa habari au mpelelezi anayetafuta ushahidi wa sauti? Nini hasa?
4.   Simu tatu, bahati mbaya ni utamaduni wa hapa nchini Tanzania lakini pia sijawahi kusikia Blackberry ya gharama zote hizi karibu zaidi ya dola 3,400 za Marekani.
Hiki ni kioja na ushamba mwingine. Ina nini hiyo simu? Inavaa chupi?
5.   Pete mbili ni sawa lakini bado alipoongea na waandishi alikuwa amevaa  mapete mengine. Sasa yote ya nini?
6.   Dola za Marekani zote hizo kwa safari ya vijijini ni za nini? Au alizitoa huko huko?
7.   Fedha za Tanzania nadhani ni sawa maana yake alihitaji kulipia gharama  kadhaa. Pia, kadi mbili za benki ni sawa na hata mabegi matatu ya nguo si  ajabu, kama alikuwa na safari ndefu na hata baraghashia mbili si tatizo.
8.   Nyaraka za serikali, hii ni fedheha kubwa kwa kuwa kama naibu waziri  alipaswa kujua jinsi ya kutunza nyaraka za serikali mara aingiapo  hotelini  au popote pale. Huwezi kuziweka nyaraka nyeti hovyo hovyo tu.
9.   Pasipoti mbili zote za nini? Alihitaji kwenda nazo Morogoro za nini?
Huenda moja ni ya kidiplomasia na nyingine ya utumishi serikalini ama ya  kiraia, lakini za nini zote hizo?
10.  Kwenye silaha hapa ni suala la uhalifu kwa mujibu wa sheria zetu labda  kama kuna maelezo mengine.

SMG ni silaha ya kivita, labda kama yeye na  polisi wa Morogoro wanamaanisha kitu kingine kwa kutumia maneno "SMG".

Huu ni uvunjaji wa sheria na wala hakuna haja ya kujiuliza kwamba anaogopa  nini au analinda nini, mbona ameshindwa kulinda mali alizoibiwa?

Ingeibiwa angekuwa amewaweka raia wengi sana na  hata polisi hataraini. Nashangaa wale waandishi hawakuuliza mapema ili  tupate maelezo. SMG?

Hii ninayoita element ya excessiveness ni ulimbukeni wa kiafrika haswa  kwamba sasa una madaraka, kwa hiyo unataka kila kitu kijazane kwako tu  kwa  kuwa hela zipo na "haki" ipo hata kama haikubaliani na sheria zetu.

Mavitu, makompyuta, mahela, masilaha, mavinasa sauti, mapete, madude mengi  tu - Swali ni je, kuna busara hapo? Kuna utu-uzima hapo? Hii ni sifa  nzuri  ya kiongozi kweli kujijazia mavitu hovyo hovyo tu na kuishiwa  kuibiwa kirahisi namna hii bila haya?

Lakini kutokana na utamaduni wetu wa kulindana unaojengeka siku hizi, huyu  hataguswa.

Hii ni aibu kubwa mno kwa taifa letu na yeyote anayetetea  mambo  kama haya, hana nia njema na taifa hili. Pana tatizo hapa, ni zaidi ya  kuibiwa naibu waziri fulani.

Kwa maoni kuhusu makala hii (Gazeti la Tanzania Daima), wasiliana kwa simu +255 713260071

No comments: