Friday, March 23, 2012Nimeugua Dar es Salaam; Natibiwa Hapa Hapa, Sio IndiaNa Profesa Joseph Mbele


Profesa Joseph Mbele
Nimeugua Dar kuanzia siku chache zilizopita. Nimejikuta nikiwashwa hasa mikononi, miguuni, na mgongoni. Kwa siku mbili sikuweza kulala usiku. Katika kuulizia watu, nikaambiwa ni "allergy." Na mhudumu mmoja kwenye duka la madawa maeneo ya Sinza aliniambia niende Magomeni, kwenye hospitali ya Dr. Ole. 

Nilienda hapo. Wakati wa kuchukuliwa damu ili ipimwe, mpimaji alinipiga mchapo kuwa isije ikawa nimewekewa sumu ya unga. Akazidi kutonya, huku akijifanya ananyunyizia unga mezani, kuwa kaunga kidogo tu kanatosha. Nami nilijibu kuwa mtu huwezi kujua, kwani Bongo haina dogo. Tukawa tunacheka.

Ni kweli daktari alipochunguza ripoti ya upimaji amegundua nina "allergy," na akanielezea sababu zake. Pia alisema kuna bakteria katika damu. Aliniandikia sindano na vidonge vya aina mbali mbali. Alisema kuwa hiyo dozi itafuta kabisa hili tatizo. Nimedundwa sindano jana na vidonge nikaanza. Tayari nimeshaanza kujisikia nafuu. Naendelea vizuri kabisa.

Nimeleta habari hii binafsi kwa sababu maalum. Kwanza, mimi kama m-Tanzania nina imani na madaktari wetu. Ninafundisha Marekani, na ninapougua kule natibiwa kule. Ninapougua Tanzania natibiwa hapa. Tena, miaka yote ya maisha yangu, kabla sijaenda Marekani nilikuwa natibiwa hapa Tanzania, bila matatizo. 

Sioni kama kuna tofauti kati ya madaktari wa Marekani na wa kwetu. Kilichopo tu ni kuwa madaktari wa kwetu wapewe mahitaji yanayopasika katika kumshughulikia mgonjwa. Na hilo ni jukumu la serikali, wala isijaribu kukwepa, kwani Tanzania si nchi maskini. Nakerwa ninapowasikia viongozi wa nchi hii wakidai kuwa sisi ni nchi maskini. Juzi hapo nimemsikia waziri kwenye kipindi cha televisheni akitoa huo upupu kwamba Tanzania ni nchi maskini. 

Nawashangaa wa-Tanzania waoendelea kuwapigia kura mbumbumbu wa aina hiyo, wasio na upeo kiuongozi, hawana fikra za kuijengea jamii ari ya maendeleo, badala yake wana upeo wa kudumaza na kukatisha tamaa. Nawashauri wajifunze kutoka kwa Rais Obama, ambaye katika mazingira yoyote yale, hawakatishi tamaa raia wake, bali anawahakikishia kuwa Taifa litapambana na litashinda, litafanikiwa. Lakini viongozi wa kwetu, kila kukicha ni vilio kuwa sisi ni nchi maskini!

Uwezo wa kuimarisha hali ya mahospitali yetu tunao, tukizingatia rasilimali nyingi tulizo nazo katika nchi hii. Pia, magonjwa mengi tunayopata hayahitaji daktari bingwa. Yanatibiwa vizuri, iwe ni Marekani au Tanzania. Tena yako magonjwa ambayo ni ya nchi kama zetu, ambayo wataalam wake ni hao madaktari wentu. Mifano ni malaria. Usidhani kuwa ukipata malaria, ukimbilie Marekani. Unaweza ukafia kule, kwa sababu sio madaktari wengi wanaijua malaria na namna ya kupambana nayo kama wanavyojua madaktari wa nchi kama Bongo. Hao madaktari wetu wanasomea magonjwa ya hapa kwetu. Ninavyofahamu, wanapoenda kusomea Ulaya, utakuwa wanasomea "tropical medicine" ambayo ndio uwanja wa mapambano katika nchi kama yetu.

Madaktari wetu wana ujuzi wa hali ya juu, utawakuta wako katika nchi mbali mbali. Ninawafahmu baadhi ambao wako Marekani, katika hospitali mbali mbali, kama vile Mayo Clinic, ambayo ni maarufu sana duniani. Yaani inashangaza kuwa ukienda hizo hospitali, unawakuta madaktari wengi wa kutoka Afrika, yaani madaktari kama hao wanaonyanyasika Tanzania kwa sababu ya viongozi wetu kutokuwa na upeo upasao.

Kwa hiyo, serikali yetu inachopaswa kufanya ni kuwekeza katika huduma za mahospitali yetu hapa hapa nchini. Iweke vifaa na miundombinu, ili madaktari wetu waweze kutumia ujuzi wao ipasavyo. Wakipata vifaa na miundombinu, na wakilipwa ipasavyo, watafanya yale yale ambayo baadhi ya watu nchini wanayatafuta India au ughaibuni. Tunapowapeleka watu nje eti kuchekiwa afya, wakati hizi ni taaluma za madaktari wetu pia, au tunawapeleka watu kutibiwa ugonjwa kama niliopata mimi wiki hii, ambao madaktari wetu wanajua namna ya kuutibu, ni kuwadhalilisha madaktari wetu, na mimi sitalilazia damu suala hilo.

Miezi michache iliyopita, nilipata fursa ya kumsikiliza Daktari m-Marekani, Mark Jakobson, ambaye ni mwendeshaji wa 
hospitali ya Selian, Arusha. Alikuwa akitoa mhadhara Minnesota, kuhusu shughuli za hospitali hiyo. Siku moja, Insh'Allah, nitaelezea hotuba yake katika hii blogu yangu. Jambo mmoja ninalokumbuka ni jinsi alivyowapigia debe madaktari wa ki-Tanzania wanaofanya naye kazi. Anatamani tu angekuwa na uwezo wa kuwalipa vizuri zaidi, ili wasipate vishawishi vya kwenda sehemu zingine.

Makala hii nimeiandika pia kwa sababu juzi hapo niliandika makala 
kuhusu mgomo wa madaktari nikaishutumu serikali kwa kudiriki kugombana na madaktari. Kwa hivi, nimejichukulia fursa hii kuelezea zaidi hisia zangu. Kati ya mambo niliyosema ni kuwa kisaikolojia, daktari anapaswa awe kazini akiwa amefurahi na moyo mkunjufu. 

Huyu jamaa aliyenipima damu alitoa mchapo na tukacheka. Muuguzi au daktari anapokuwa na moyo mkunjufu na ucheshi, anapokuwa hana msongo wa mawazo, ni baraka kwa wagonjwa. Watafiti wa masuala ya saikolojia ya wagonjwa na matibabu wanathibitisha hilo. Ndio maana niliishutumu serikali kwa kutotambua umuhimu wa kuwaridhisha madaktari.


No comments: