Monday, April 09, 2012

Lilongwe, Malawi


Rais Banda amfukuza kazi mkuu wa polisi

Rais Joyce Banda wa Malawi.


Rais mpya wa Malawi Joyce Banda amemfuta kazi mkuu wa polisi Peter Mukhito, kwa mujibu wa taarifa zilizotangazwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali.

Bibi Banda aliapishwa kuwa Rais Jumamosi baada ya kifo cha Rais Bingu wa Mutharika wiki iliyopita. Amekuwa makamu wa Rais tangu mwaka 2009, lakini alikorofishana na Bw Mutharika na kujiondoa kutoka chama chake kinachotawala.

Hakuna sababu iliyotolewa ya kuondolewa kwa Bw Mukhito, lakini mwandishi wa BBC nchini humo anasema ameshtumiwa kwa uongozi mbaya wakati wa ghasia za kuipinga serikali zilizotokea mwaka jana.

Bw Mutharika, mwenye umri wa miaka 78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alkhamisi iliyopita ingawa kifo chake hakikuthibitishwa mpaka siku ya Jumamosi.

Alitawala Malawi kwa kipindi cha miaka minane lakini hivi karibuni alishtumiwa kwa kufisidi uchumi na kutawala kwa mabavu.

Malawi imekumbwa na ukosefu wa mafuta na fedha za kigeni tangu Uingereza na wahisani wengine kufuta misaada yao.

Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani akiwa mjini Blantyre anasema aliyekuwa mkuu wa polisi alianza kupata sifa mbaya mwaka uliopita baada ya kumhoji mhadhiri mmoja kwa kulinganisha vuguvugu la upinzani katika nchi za Tunisia na Misri kuwa sawasawa na mgogoro wa mafuta nchini Malawi.

Tukio hilo hatimaye lilisababisha kufungwa kwa tawi moja la chuo kikuu cha Malawi.

Mnamo mwezi wa Julai mwaka jana ,takriban watu 19 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kuipinga serikali kuhusu uchumi unaozidi kuzorota nchini humo.

Wakati huo huo maafisa wa serikali wanasema matayarisho yanafanywa kurudisha maiti ya Rais Muthariika kutoka Afrika ya Kusini ambako alisafirishwa baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.

Kutoka BBC Kiswahili

No comments: