Sunday, May 06, 2012


Aachwa na mume kwa kuzaa watoto wa ajabu


Sofia Rashid (22) mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam yupo njia panda kwa kutojua hatma ya watoto wake wawili ambao wote wamekumbwa na maradhi ya ajabu ya kujaa maji kichwani.
Watoto hao Omar Mohamed (4) na Maulidi Mohamedi mwenye umri wa miezi minne wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kupatiwa tiba.
Akiongea akiwa wodini, Sofia alisema anakabiliwa na mateso moyoni mwake pale anapowaona watoto wake wanavyoteseka kwa maradhi hayo.
Alisema watoto wake wote walizaliwa wakiwa na maradhi hayo ambapo walipofikia miezi miwili walianza na tatizo la kichwa kukua kwa haraka na kusababisha ashindwe kuwabeba.
Sofia alisema kwamba kutokana na matatizo ya watoto wake, mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mohamed alimpa talaka kwa madai hawezi kuishi naye kwa sababu anazaa watoto wa ajabu.
Alieleza toka apewe talaka baba wa watoto hao hajakwenda kumjulia hali wala kumpatia huduma muhimu kwa ajili ya watoto hao.
“Inaniuma sana nikiona hali hii, mimi sikupenda kuzaa watoto hawa ila Mungu amepanga, lakini mwenzangu ananiona kama mimi ndiye mwenye tatizo na kuamua kuniacha,” alisema.
Endapo ukifika kwa mara ya kwanza na kuwaona watoto hao wakiwa wamelala kwenye kitanda kimoja wodini hapo, hautaweza kugundua kwa haraka umri wao kama hautaelekezwa na mama yao ambaye muda wote anakaa karibu nao kwa ajili ya kuwapatia msaada.
“Hawa hawajazaliwa wakati mmoja, huyu Omar ana miaka minne na mdogo wake ana miezi minne tu, lakini kutokana na ugonjwa hauwezi kumtambua nani ni mkubwa kiumri,” alisema mama yao baada ya kuulizwa umri wao na mwandishi wa gazeti hili.
Hata hivyo, alisema licha ya kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu kwenye hospitali hiyo, bado anapambana na matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa pesa ya kununulia chakula pamoja na mavazi ya watoto hao pamoja na yeye mwenyewe.
“Hapa nilipo sina nguo wala chakula kwa ajili ya watoto na mimi mwenyewe, namshukuru dada yangu kwa kunipa msaada lakini kutokana na kutokuwa na kazi maalum inakuwa vigumu kunitosheleza mahitaji,” alisema.
Sofia aliwaomba wasamaria wema watakaoguswa na matatizo yake kumsaidia kwa hali na mali kwa ajili ya kumsaidia kumpatia pesa za kujikimu akiwa wodini hapo.
Afisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa alisema Sofia na wanawe walifikishwa hapo miezi minne iliyopita, ambapo madaktari wanajitahidi kutoa huduma za kuokoa maisha ya watoto hao ikiwemo kuwafanyia upasuaji wa kichwa.
Alisema baada ya kuwafanyia uchunguzi imebainika watoto hao wanasumbuliwa na matatizo ya kichwa kujaa maji na tiba yake inafanyika hospitalini hapo.
Kwa yeyote anayetaka kumsaidia Sofia kwa huduma ya chakula, mavazi awasiliane na Afisa Uhusiano wa Moi Almas au afike ofisi ya gazeti la Nipashe Mikocheni na kuwasiliana na Moshi Lusonzo kwa namba +255 717 336368. 

No comments: