Tuesday, May 08, 2012

Rais Mstahafu Benjamin Mkapa
“Niliruhusu ununuzi wa jengo la ubalozi Italia”

Rais Mstahafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, kutoka ushahidi wake katika kesi inayomkabili  aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu anayekabiliwa na shtaka la kuhujumu uchumi.


RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa , aliandika historia mpya nchini baada ya hatua yake ya kutinga katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na kutoa ushahidi wake katika kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya mbili inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ambapo alidai kuwa ni yeye kwa niaba ya Serikali ndiyo aliyempatia idhini Mahalu kununua jengo la Ubalozi kwa thamani ya Euro Milioni 3 kwa njia ya mikataba miwili na kwa akaunti mbili kwa njia ya mdomo.
Rais Mkapa ambaye ni shahidi wa Profesa Mahalu, aliingia mahakamani hapo saa 3:45 asubuhi akiwa amepanda kwenye gari aina VX lenye namba za usajili T 745 BQE na gari jingine aina hiyo yenye namba za usajili T 941 BES huku akiwa akiongozwa na walinzi na maofisa wa toka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS = Tanzania Intelligence & Security Service), ambao wengi wa maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa walionekana kuingia katika viwanja vya mahakama hiyo kabla ya kiongozi huyo kuwasaili, kwa tofauti tangu saa mbili asubuhi kwaajili ya kuakikisha ulinzi wa kiongozi huyo na mazingira hayo unaimarika.
Sekunde chache baada ya Rais Mkapa walimuingiza katika ofisi ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ambapo aliketi kwaajili ya kusuburi upande wa Jamhuri umalize kumhoji Mahalu ndipo yeye aitwe kwenye chumba Na.9 ambacho ndicho kilikuwa kikikutumiwa kuendeshea kesi hiyo ambayo ilifanya hadi baadhi ya wananchi mawakili waliokuwa wakiendesha kesi nyingine kuingia ndani ya chumba hicho kumshuhudia rais huyo akitoa ushahidi wake na wakati wote huo maofisa wa usalama wa Taifa walikuwa wameketi ndani ya chumba cha mahakama na kwenye mlango wa chumba hicho kilichokuwa kikiendeshea kesi kwaajili ya kuimarisha ulinzi.
Mkapa aliongozwa na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa kutoa ushahidi wake alianza kwa kula kiapo ambapo alieleza kuwa kati ya mwaka 1995-2005 alikuwa ni Mkazi Dar es Salaam na alikuwa ndiye Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba anauzoefu wa Kimataifa kwani kabla hachaguliwa kuwa
Rais aliwahi kushika wadhifa wa Ofisa wa Mambo ya Nje, Balozi wa nchi Canada, Nigeria na Washngton DC.
Alidai kuwa alivyokuwa Rais wa Jamhuri alifahamu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia na kwamba jengo hilo lilinuliwa kwa thamani ya Euro 3,098,741.40 kwa maagizo ya serikali ambayo alikuwa akiingoza yeye na kwamba mwaka 2003 yeye ndiye aliyekwenda mjini Rome-Italia kuzindia jengo hilo ambalo alidai ni jengo la zuri la kisasa na wakati huo balozi alikuwa ni Profesa Mahalu na kwamba anamfamu vyema mshitakiwa huyo.
“Serikali yangu iliarifiwa bei na taratibu za kulinunua jengo hilo na aliyetufahamisha ni aliyekuwa balozi wetu kule kwa kipindi hicho Mahalu.Katika manunuzi hayo mimi kama rais wan chi nilitaarifiwa kuwa muazi wa jengo hilo alitaka malipo yafanywe mara mbili tofauti katika akanti za muuzaji …na serikali ilitoa baraka zake mimi niliarifiwa na na sikuzuia na kwaniaba ya serikali yangu nikatoa idhini jengo linunuliwe kwa mtindo huo nilioutaja hapo juu”alidai Rais Mkapa.
Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili Mgongolwa, Marando dhidi ya Rais Mkapa:
Mawakili:Katibu Mkuu Kingozi wa enzi za utawala wako, Martin Lumbanga ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa Jamhuri alieleza mahakama kuwa hana taarifa kama serikali ya awamu ya tatu ilitoa kibari kwa mshtakiwa anunue jengo hilo?

Mkapa: Ninashangaa sana Lubanga kusema hilo. Ila mimi kama Rais nafahamu nilitoa idhini kwaniaba ya serikali ya unununuzi wa jengo hilo kwa utaratibu ambao nimeishautaja.

Mawakili: Kama wewe rais ulijua kuwa ulitoa idhini , inawezekana Lumbanga asiweze kujua kuwa wewe ulitoa idhini kwaniaba ya serikali?

Mkapa: Tetee! Inawezekana Lumbanga asijue lakini inakuwa vigumu sana.Watu akaangua vicheko.

Mawakili: Ebu soma kwa sauti hii kumbukumbu ya Bunge “Ansard ‘ ya mwaka 2004 iliyomnukuu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya awamu ya tatu, Jakaya Kikwete ili mahakama isikie?

Mkapa: “Naibu Spika wizara yangu inunua jengo la Ubalozi wa Italia , lengo likiwa kupunguza gharama za kupanga na kwamba taratibu za sheria ya manunuzi ya umma zilifuatwa na fedha hizo zilitumwa kwa awamu tatu ambapo mara ya mwisho kuzituma ilikuwa ni Agosti 26 mwaka 2002 ambapo jumla serikali ilituma Sh bilioni 2.9, baada ya hapo serikali ilifuata taratibu za manunuzi na baadae ilikuja kuzuka taarifa kuhusu ubadhilifu lakini ripoti ya CAG ,ilisema ubalozi wa Italia hakupata achafu’.

Mawakili: Je maneno hayo ya Waziri Kikwete ambaye kwa sasa ndiye rais wa nchi katika Ansard hiyo ya bunge?

Mkapa: Maneno hayo ya Kikwete ni sahihi.

Mawakili: Wewe au serikali ya awamu ya tatu iliwahi kupokea malalamiko toka serikali ya Italia kuwa ubalozi wetu nchini humo ulivunja sheria kuhusu mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo?

Mkapa: Hapa,kamwe sijawahi kupokea malalamiko.

Mawakili: Uwakiwa rais hujawahi kupokea malalamiko kuwa fedha za serikali yetu zilizotumwa kwa ajili ya kumlipa muuzaji wa jengo hilo kuwa hazijamfikia?

Mkapa: Hadi leo hii natoa ushahidi hapa mahakamani sijawahi kupokea malalamiko ya aina hiyo.

Mawakili: Uliwahi kupata malalamiko toka kwa CAG, Wizara ya Mambo ya Nje, Katibu Mkuu Kiongozi, Wazari wa Mambo ya Nje, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala Ofisi ya DPP kuhusu ubadhirifu wa ununuzi wa jengo hilo?

Mkapa: Sijawahi kupata.

Mawakili: Nini ufahamu wako kuhusu utumishi wa Profesa Mahalu?

Mkapa: Namfahamu kama msomi mzuri, mchapakazi,mhadilifu na kiongozi anayetenda haki.

Mawakili: Mawasiliano kati ya Serikali na Balozi yanafanyika kwa njia zipi?

Mkapa: Balozi anaweza kuwasiliana na serikali yake kwa njia ya Barua kwa Wizara ya Mambo ya Nje,Katibu Mkuu Kiongozi,rais au kwa njia ya mdomo.Na mawasiliano siyo lazima yafanyike kwa njia ya maandishi tu kwasababu maelekezo mengine ambayo anapewa balozi na serikali yake ni ya siri kwa maslahi ya taifa hivyo anaweza kuitwa nyumbani na kupatiwa maagizo hayo kwanjia ya mdomo.

Mawakili: Kwa wadhifa wako ule wa urais,kabla ya kwenda kuzindua jengo hilo Januari 23 mwaka 2003, hukuwai kupokea taarifa toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP za kukukataza usiende kuzindua jengo hilo kwasababu kwasababu kuna harufu za ubadhilifu wa fedha za umma?

Mkapa: Ofisi hizo hazikuwahi kunipatia taarifa hizo.
Yafuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa serikali Ben Lincoln, Vicent Haule na Ponsian Lukosi dhidi ya Rais Mkapa:

Mawakili: Ebu ieleze Mahakama ni kwanini bei za jengo zinatofautiana maana risiti ya manunuzi ya jengo hilo zinaonyesha jengo lilinuliwa kwa Euro milioni 3 na Ansard ya bunge iliyosomwa na Kikwete bungeni mwaka 2004 inasema jengo lilinuliwa kwa Shilingi bilioni 2.9?
Mkapa: Kazi yangu siyo kufanya uthamini wa fedha za kigeni kwamba wakati huo hizo Euro Milioni 3 zilikuwa na thamani gani kwa fedha Tanzania. (Watu wakacheka).
Mawakili: Nani aliagiza upelelezi wa manunuzi ya jengo la Italia ufanyike?

Mkapa: Sijui.

Mawakili: Uchunguzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wewe ukiwa madarakani ?

Mkapa: Sijui, milikuja kuona Balozi Mahalu kashtakiwa mwaka 2007 nikiwa tayari nimestaafu.Siku ya kwanza ya kwanza alipofikishwa kortini na keshi yake nilithibitisha taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kuwa ni kweli Mahalu ameshtakiwa.

Mawakili: Nani alikupa taarifa za muuzaji wa jengo hilo anataka kulipwa kwa mtindo huo wa akaunti mbili?

Mkapa: Ni Mahalu na alinipa taarifa kwa mdomo na alikuwa ameandaa ripoti juu ya ununuzi na akawa anaomba ridhaa ya serikali na aliomba ridhaa ya serikali kabla ya kununua jengo.

Mawakili: Ulisema hukuweza kuzuia ununuzi wa jengo, Je ulikuwa na madaraka ya kuweza kuzuia lisinunuliwe?

Mkapa: Eh! Mimi ndiye nilikuwa rais wa nchi nilikuwa na madaraka pia ya kuzuia serikali isitoe fedha kununua hilo jengo na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye mahitaji mengine ila kwasababu nilikuwa ninajua umuhimu na faida ya nchi kununua jengo lile ndiyo maana nikaridhia kwa mdomo jengo lile linunuliwe.

Wakili: Ulitoa maelekezo kwa nani?

Mkapa: Nilitoa maelekezo jengo linunuliwa kwa njia yam domo kwa watendaji na maagizo hyo yalipaswa yatekelezwe na wizara ya Mambo ya NJe na ilikuwa jukumu la Mahalu la kuieleza wizara hiyo na ubalozi watekeleze maagizo yangu.

Wakili: Kwa hiyo unaieleza mahakama kuwa wizara ya Mambo ya Nje, ilituma malipo kwa mtindo wa akaunti mbili tofauti?

Mkapa: Ina husu nini sasa?mimi nilitoa maagizo kwa Mahalu jengo linunuliwe hivyo ni jukumu la balozi mahalu kuieleza wizara yake sasa suala la hayo makaratasi ya kufanya mchakato wa kulinunua jengo hilo,mimi kama rais siwezi kuingilia. Nilitoa maelekezo kwa watendaji,watendaji walipaswa watekeleze.

Mawakili: Utajisikiaje yule muuzaji aliyetuuzia jengo kuwa uamuzi wake wa kutuuzia jengo kwa mtindo wa akaunti mbili ,alikuwa akikwepa kodi kwa serikali ya Italia?

Mkapa: Aaah! Misioni tatizo kikubwa hapa Tanzania tumepata jengo lengo, Aliamundulai. (watu wakacheka).

Mawakili: Ujisikiaje ukisikia Mahalu alitumia zile Euro milioni tatu zilizonunulia jengo kwa matumizi yake binafsi?

Mkapa: Nitashangaa sana. Pia wewe wakili wa serikali ndiyo nitakushangaa zaidi kwani Ansard ya bunge iliyosomwa na Kikwete bungengi imetamka bayana kuwa serikali ilimlipa muuzaji wa jengo na kwamba taratibu na sheria ya manunuzi ya umma zilifuatwa na kwamba hadi sasa huyo muuzaji hajawahi kujitokeza kulalamika kuwa hajalipwa fedha zake.

Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa ushahidi wa Mkapa ambapo Hakimu Mugeta aliairisha kesi hiyo hadi leo ambapo mshtakiwa wa pili ambaye alikuwa ni Meneja wa Utumishi na Utawala wa Ubalozi huo, Grace Martin ataanza kujitetea.

Mkapa akaondoka saa 7:29 mchana ndani ya chumba cha mahakama huku akiwa akiongozwa na walinzi wake zaidi ya watato ambao walimuongoza hadi nje ya viwanja vya Mahakama hiyo na kupanda gari ambapo aliondoka kwa msafara ambao uliongozwa na pikipiki iliyokuwa ikilia king’ora iliyokuwa ikiendeshwa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani .

Habari ni kwa hisani ya Bi. Happiness Katabazi. Mwandishi wa magazeti yenye kumilikiwa na kampuni ya Free Media Company. Ni mmiliki na mwendeshaji wa blog ya Fukuto la Jamii. Unaweza kuwasiliana naye kupitia 
katabazihappy@yahoo.com, au kuungana naye kwenye ukurasa wake wa Facebook kwa kubonyeza hapa.

No comments: