Thursday, June 28, 2012


Mipaka ya Tanzania haiko salama;
Wageni wanapita watakavyo


KWAMBA wazamiaji 45 kutoka Ethiopia wamekufa na wengine 72 wako mahututi kutokana na kukosa hewa wakiwa katika lori mkoani Dodoma ni habari ambazo bila shaka zimewasikitisha wananchi wengi. Maiti za watu hao na wenzao ambao hali zao ni mbaya waligundulika juzi asubuhi katika msitu wa Chitego, wilayani Kongwa kilomita chache kutoka mjini Dodoma.
   
Serikali imekiri kutokea kwa tukio hilo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima alifika katika eneo la tukio juzi na kushuhudia wazamiaji wengi ambao walikuwa bado hai wakiwa wamedhoofika sana kutokana na njaa na maradhi. Waziri Silima alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa, wazamiaji hao walikuwa wakifa mmoja baada ya mwingine na dereva aliyekuwa akiwasafirisha katika alipogundua hali hiyo aliona hakuwa na njia nyingine isipokuwa kuwatupa porini.
   
Sisi tumesikitishwa sana na vifo vya raia hao wa Ethiopia, pamoja na ukweli kwamba watu hao waliopoteza maisha ni wahalifu walioingia katika nchi yetu kinyume cha sheria. Tunasema hivyo kwa sababu hakuna binadamu anayefurahia kifo cha binadamu mwenzake kwa sababu zozote zile, hata kama ni kweli kwamba wazamiaji wengi kutoka Ethiopia kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakiingia nchini kinyume cha sheria na kusababisha kero kubwa kwa wananchi na Serikali kwa kulazimika kutumia fedha nyingi za wananchi kuwagharimia, ikiwa ni pamoja na kuwarudisha makwao.
   
Hata hivyo, suala la msingi hapa ni kushindwa kwa Serikali na vyombo vyake vya dola kudhibiti wazamiaji ambao sasa wanapita katika mipaka yetu na kuingia nchini kama watakavyo. Limekuwa jambo la kawaida sasa kusikia wazamiaji wamekamatwa katika eneo fulani au wamekufa kwa ajali wakati wakisafirishwa na wafanyabiashara wazalendo kwenda nchi jirani za Malawi na Msumbiji. 
   
Kinachotushangaza ni ukimya wa Serikali na kigugumizi iliyonacho siyo tu katika kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la wazamiaji, bali pia kushindwa kujifunza kutokana na matukio mengi ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakijirudia kila kukicha. Pengine ndiyo maana baadhi ya wananchi wamekuwa wakidai kwamba biashara ya kusafirisha wazamiaji ni mradi wa baadhi ya viongozi serikalini, ikiwamo Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa.
   
Vinginevyo inatuwia vigumu kuamini kwamba tatizo hilo la wazamiaji liko juu ya uwezo wa Serikali na vyombo vyake. Maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu jinsi wazamiaji hao wanavyoweza kuingia nchini kiholela pasipo vyombo vya dola kushtuka, hasa tukizingatia maelezo ya baadhi ya vyanzo vyetu vya habari katika Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi nchini vinavyodai idadi ya wazamiaji wanaokamatwa ni ndogo mno kulinganisha na idadi ya wazamiaji wanaoingia nchini bila kutambulika. 
   
Pamoja na ukweli kwamba tangu tatizo la wazamiaji lianze kujitokeza katika nchi yetu zaidi ya miaka 30 hivi iliyopita na kwa kuwa maelfu ya wazamiaji walikamatwa katika kipindi hicho, haiingii akilini kwamba Serikali muda wote huo imeshindwa kuelewa mbinu, ujanja na mikakati inayotumiwa na wazamiaji kupita katika mipaka yetu pasipo kuonekana. Ingetosha tu kuwahoji na kuwabana wazamiaji hao ili wawafichue wale waliowasafirisha, nani waliwawezesha kupita mipakani na wapi ilipo mitandao inayoendesha biashara hiyo haramu. 
   
Inasikitisha kuona Serikali bado inaonekana kuchanganyikiwa  kila mara matukio hayo yanapotokea wakati matukio hayo siyo mapya. Inasikitisha pia kuona kuwa, pamoja na wazamiaji wengi wanaoingia nchini kutoka nchi za Somalia, Eritrea na Ethiopia Serikali imeshindwa kuona umuhimu wa kuzungumza na serikali za nchi hiyo ili zilipe fidia na kuhakikisha raia wake hawatoki nje tena pasipo kufuata sheria. Vinginevyo, tatizo la wazamiaji litaendelea kuongezeka na usalama wa nchi yetu utaendelea kuwekwa rehani kutokana na udhaifu wa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama. 

Kutoka gazeti la Mwananchi, 27.06.2012

No comments: