Monday, July 09, 2012

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibuka na tuhuma nzito kuwa kuna mkakati unaofanywa na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS = Tanzania Intelligence & Security Service), kutaka kuwaua viongozi wake kama njia ya kudidimiza harakati za chama hicho mbele ya Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alidai Serikali inatumia maofisa wake ambao wamefikia hatua ya kutoa vitisho kwa viongozi wa ngazi wa chama juu ya uhai wao. 
Aliwataja viongozi ambao, wamekuwa wakitishwa kuuawa kuwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbles Lema.

Alisema kutokana na taarifa mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitapa tangu Mnyika aliposimama bungeni na kutoa kauli kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ni amekuwa akifuatiliwa ndani na nje ya Bunge, huku akipokea vitisho vya kuuawa.

“Mnyika, alisimama na kutoa kauli juu ya udhaifu wa Serikali bungeni, sasa imeonekana nongwa hata kufikia kutishiwa maisha yake pamoja na Dk. Slaa, jambo hili tunasema ni hatari kwa viongozi wetu.

“Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa, vinaeleza kuwa mpango huo, unaratibiwa na kiongozi mkubwa (jina tunalo) na ofisa mmoja anayefahamika kwa jina la Rama. Hawa kila wakati wamekuwa wakifuatilia nyendo za viongozi wetu, ikiwemo kutoa vitisho dhidi yao.

“Kutokana na hali hiyo, tumelazimika kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kesho (leo), ili kujadili kwa kina suala hili na moja ya ajenda, itakuwa ni hali ya vitisho kwa viongozi wetu,” alisema Mbowe.

Alisema chama chake hakitarudi nyuma kupigania haki za Watanzania pamoja na kupokea vitisho hivyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, kumekuwa na kugeuza ajenda ya mgomo wa madaktari na kukinasibisha chama chake hali ya kuwa hawahusiki na kuwaambia madaktari kugoma kama inavyodaiwa na baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndani ya Bunge.

Kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea, alisema Serikali inapaswa itafakari upya uamuzi wake kwa kukaa pamoja na madaktari, ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu, kuliko kuwafukuza.

“CHADEMA haikuwaambia madaktari wagome na wala haihusiki na mgomo wao…. ila tutakuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya kila kundi kwa mujibu wa utaratibu uliopo,” alisema.

Chanzo: Mtanzania 

No comments: