Wednesday, July 25, 2012



Kikundi hatari cha Mafia kimeingia Tanzania?

Barnabas Maro

ALIYEKUWA Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na baadaye Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Imran Kombe, aliuawa kinyama Juni 30, 1996 na askari wa Jeshi la Polisi kwa madai kuwa mwizi sugu wa magari aliyekuwa akisakwa kwa muda mrefu. Askari waliomuua walitokea Dar es Salaam.

Marehemu na mkewe walikuwa Hoteli ya Keys mjini Moshi wakila chakula cha mchana huku askari waliokuwa wakimfuatilia wakimsubiri nje bila yeye kujua. Kama alikuwa ‘mwizi sugu’ askari walikuwa na nafasi nzuri ya kumkamata ili awataje wenzake, lakini hawakufanya hivyo!

Bila kujua lililokuwa mbele yake, Kombe na mkewe waliondoka Hoteli ya Keys kuelekea nyumbani kwao. Askari waliokuwa wakimwinda, wakamfuatilia mpaka eneo la Mailisita, lililozungukwa na mashamba ya mihindi kando ya mji wa Moshi na kumwamuru asimame na kushuka katika gari alimokuwamo.

Walimfyatulia risasi kadhaa zilizokatisha uhai wake; na watu walipofika eneo la tukio walielezwa kuwa aliyeuawa ni ‘mwizi sugu’ wa magari waliyekuwa wanamsaka kwa muda mrefu.

Imran Kombe ni mtu aliyefahamika vizuri sana kiasi kwamba ingekuwa vigumu mno kutotambuliwa na askari, ingawa alikwisha staafu. Aliuawa kwa dhana kuwa alikuwa na mwelekeo wa upinzani, akikishabikia NCCR-Mageuzi; na serikali ilimwogopa kuwa angeweza kutoa siri nzito za serikali kwa upinzani.

Tuchukulie alikuwa ‘mwizi sugu’ kama ailivyodaiwa na waliomuua. Kwa nini hawakumkamata wakati akiwa anakula hotelini? Kwa nini walimfuatilia mpaka nje ya mji, tena eneo lililozungukwa na mihindi ndipo wamuue kinyama?

Kwa nini hawaakumsubiri mpaka afike nyumbani wakati nyumba yake ikiwa imezingirwa na askari wengine kisha wamwamuru ashuke garini mikono yake ikiwa juu halafu wamkamate na kuipekua nyumba yake kutafuta ushahidi muhimu?

Kadhalika huo ungekuwa wasaa mzuri kwao kumpeleka kituoni na kumhoji ili ataje wenzake anaoshirikiana nao. Yote hayo hayakufanyika na wala mbinu za kipolisi hazikutumika iingawa wauaji walikuwa askari wa Jeshi la Polisi waliopaswa kufanya kazi kwa kufuata kanuni za jeshi hilo!

Baada ya mauaji ikasemwa ilikuwa bahati mbaya. Waliomuua walihukumiwa kunyongwa mwaka 1998 lakini Oktoba mwaka 2011 waliachiwa huru! Askari wale walimuua kwa amri ya nani? Nakuachia wewe msomaji ufanye tafakuri.

Kama humfahamu, utakuwa umesoma habari/makala zake za uchunguzi zinazofichua maovu ya watumishi wakuu wa serikali. La bado hujamtambua, ni kijana shababi anayeongoza kundi la waandishi mahiri wa gazeti la MwanaHALISI litolewalo kila Jumatano jijini Dar es Salaam, Saeed Kubenea.

Akiwa na wenzake katika maandalizi ya gazeti lao kule Sinza, walivamiwa na kundi lililotumwa kuwadhuru, wakamwagiwa tindikali machoni na mwenzie aitwae Ndimara Tegambwage akakatwa kwa mapanga kichwani.

Ulifanyika uchunguzi na watuhumiwa wakakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake. Hatimaye waliachiwa huru kwa kuwa ushahidi uliotolewa haukutosha kuwatia hatiani! Hapa pia nakuachia msomaji utoe uamuzi wako kwani naogopa kukulisha maneno mdomoni.

Kulikuwa na orodha ya watu watano walioonekana “kujitia kimbelembele mno” katika mapambano dhidi ya mafisadi wanaofilisi uchumi wa nchi. Watu hao walikuwa katika orodha ya “kushughulikiwa” ili kuwaogofya wengine wenye “kiherehere” (pupa na papara ya mtu kutaka kupata au kujua jambo) kama wao.

Waliotajwa ni Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, mawaziri Samuel Sitta, Profesa Mark Mwandosya, Dk. Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.

Bila shaka wananchi wanakumbuka yaliyowapata kina Mwandosya, Mwakyembe na Slaa ambao mpaka sasa hali zao bado hazijatengemaa (kitendo cha jambo kuwa katika hali ya ukamilifu) ingawa serikali iliwapeleka Mwakyembe na Mwandosya India kupata matibabu yasiyopatikana humu nchini. Wahenga walinena kuwa “mchawi hulia sana msibani”. Nawaachia wenye meno wagugune bisi nilizowakaangia. Lisemwalo lipo na kama halipo li njiani.

Mvutano unaoendelea hivi sasa kati ya madaktari na serikali umezusha maswali mengi yasiyo na majibu. Daktari Stephen Ulimboka ambaye ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, alitekwa kitaalamu, akateswa kwa kupigwa na kutupwa msitu wa Pande pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam, usiku a Jumanne kuamkia Jumatano Juni 27.

Kwa mujibu wa maelezo yake (Dk. Ulimboka), alipigiwa simu na mtu aliyedai kufanya kazi Ikulu ili wakutane Leaders Club kule Kinondoni. Baada ya kutekwa na kuingizwa ndani ya gari jeusi lisilo na namba, aliadhibiwa humohumo wakati gari likiwa katika mwendo.

Alifikishwa kwenye nyumba fulani na kutakiwa aseme walio nyuma ya mgomo wa madaktari. Alisulubiwa kuanzia saa sita usiku mpaka saa kenda alfajiri ya Jumatano baada ya kung’olewa meno mawili na kunyofolewa kucha zake kisha akatelekezwa msituni, labda wakijua keshakufa!

“Sema ni nani aliye nyuma ya mgomo wa madaktari?” Ni swali zito lisiloweza kuulizwa na mtu asiyekuwa na sababu maalumu ya kuuliza hivyo. Mgomo wa madaktari unawahusu nini majambazi, kama kweli waliomteka walikuwa majambazi?

Swali la pili la kujiuliza ni hili: Baada ya kachero wa Polisi kufika Muhimbili na kugundua Dk. Ulimboka hajafa, yasemekana alikwenda chooni kupiga simu akiarifu kuwa “kumbe Dk. Ulimboka hakufa …”

‘Kumbe’ ni neno la mshangao linaloonesha kuwa mtamkaji hakuwa anajua ukweli; pia kutaja hali au jambo la kinyume cha lile uliloambiwa. Je, kachero huyo aliambiwa Dk. Ulimboka kafa na alipofika Muhimbili akashangaa kuona bado yu hai? Tafakari.


No comments: