Friday, July 27, 2012

Kuitetea Zanzibar katika Muungano – Balozi Ali Karume

Balozi Ali Karume.


Muungano, hawezi wakati huo huo kudai Muungano uvunjike. Iwapo Muungano utavunjika, hiyo Zanzibar utaiteteaje katika Muungano ambao umeshavunjika? Lazima kuitetea Zanzibar katika mfumo wa Muungano ambao unatoa haki sawa kwa nchi mbili ambazo zimeungana. Mwanzo wa haki hizo ni katika kuongoza Muungano kwenye safu zote za Serikali ya Muungano, kuanzia ngazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchi mbili zikiungana huwa zinasaka "Equity" kwenye huo Muungano. Uwiano wa haki huleta usawa kwa pande zote mbili na kuchelea upande mmoja kujihisi wametawaliwa au wamemezwa. Kujihisi au kuwa na hesia ya kutawaliwa huleta unyonge wa kuhisi kuna ukosefu wa utetezi; maana kwenye utetezi kamili, hakuna kupunjwa, kunyanyaswa, au kuonewa. "In politics, perception is everything". Kwenye siasa, kilakitu hutokana na hesia. Ukihisi unadhulumiwa, huwachi kulalamika.

Kwenye nchi zinoungana kisiasa, tatizo la kwanza ni kupanga safu ya uongozi utoridhisha sehemu zote za Muungano. Mara nyingi, katika kuepuka vurugu za kuchagua Rais mpya wa Muungano, mapendekezo ni kwamba Rais wa nchi moja ndie awe Rais mpya wa huo Muungano. Hii humaanisha kwamba Rais wa ile nchi nyengine awe Makamo wa Rais, ili wale Marais wawili kabla ya Muungano, waongoze serikali ya Muungano kwenye safu ya Rais na Makamo wake. Pia, humaanisha kwamba baada ya kipindi au vipindi muafaka, na yule Makamo au kiongozi mwengine kutoka nchi yake, aweze kuongoza kwenye safu ya Urais wa Muungano. Na upande wa pili wa Muungano utowe Makamo wa Rais.

Katiba ambayo tumepania kuibadili, imetamka wazi kwenye hilo, na watetezi wa Zanzibar hilo wamelifurahia. Katika Katiba mpya, bora hilo libaki, na katika kutilia mkazo "Equity" na uwiano utaochelea migogoro na malalamiko ya kuelemewa, ni bora Katiba itamke wazi juu ya suala la kupishana na kuwepo zamu kwenye Urais na vyeo vyengine vya juu.

Kila Katiba huwa na Yaloagizwa, Yaloelezwa, na Yanotegemewa kutokana na itikadi. "Traditions" ni kitu muhimu katika uteuzi wa viongozi, na katika Muungano ni lazima kujenga itikadi ya kuteua viongozi kutoka pande zote mbili. Watetezi wa nchi zao ni lazima kusimamia hilo. Lazima kuwe na "Deliberate attempt" Jaribio la makusudi na la dharura kutoa zamu kwenye uongozi, ilimradi watoteuliwa wakidhi sifa zinotegemewa. Hayo yamefanyika katika historia ya Muungano wetu, na sioni kwanini iwe mwiko kuirejea historia hiyo. Katika demokrasia, wengi wape kutokana na wingi wa kura, na tusipofanya jaribio la makusudi na la dharura kuwapata viongozi wa safu za juu kutoka sehemu zote za Muungano wetu, basi wengi watatoka sehemu moja na kuendelea kujenga hisia kwamba sehemu moja ya Muungano imeelemewa. Ndio maana kuna wengine wanajihisi wamesakamwa na wanaomba waachiwe wapumuwe.

Tunapopata fursa ya kuchagua viongozi wa juu, kama vile Rais wa Jamhuri ya Muungano, ni vyema wale wanaodai kuitetea Zanzibar wawe mstari wa mbele katika kumpata mgombea bora kutoka Zanzibar na kumsaidia ili ateuliwe. Hili ni muhimu kufanyika, hasa baada ya uongozi wa ngazi ya juu kabisa kukamatwa na viongozi kutoka sehemu moja ya Muungano kwa muda mrefu. Mwenyekuitetea Zanzibar kikweli kwenye hilo, hawezi kudai kwamba hakuna Mzanzibari anofaa kwenye wadhifa huo. Anayechukua msimamo huo, anachangia Zanzibar kusakamwa na kukosa pumzi. "Tuacheni tupumuwe" aambiwe na yeye pia.
Mzanzibari anayewakataa wagombea wote kutoka Zanzibar na kumuunga mkono mgombea kutoka bara kwa hali na maji aendelee kutawala, asidai kwamba anaitetea Zanzibar na kudai "Tuacheni tupumuwe". Kwani kwenye kusakamwa na Bara, na yeye si alichangia? Ya yeye alichangia katika kutukosesha pumzi, ilimradi yeye apumuwe vizuri zaidi baada ya kutuuza. "We were sold down the river to the highest bidder by our own kith and kin". Kikulacho kinguoni mwako.

Umefika wakati Watanzania tuwe makini sana. Tutetee haki zetu kwenye Muungano wetu, na tujizatiti katika kuepusha "Dhana" ya aina yoyote ya kwamba upande mmoja wa Muungano wetu, umeelemewa. Tuunde Katiba mpya itoondowa dhana ya kutawaliwa na tutoe fursa kwa pande zote ziachwe zipumuwe. Tukishindwa kwenye hilo, tutajitakia maradhi. Na wahenga walisema "Maradhi ya kujitakia; Mtu hapewi pole".

Balozi Ali Abeid Amani Karume.


No comments: