Saturday, August 18, 2012

Rais Kikwete wa Tanzania na Rais Banda wa Malawi wakutana mjini Maputo, Msumbiji




Picha kwa hisani ya blogu ya Ikulu Dar es Salaam: http://ikulublog.com 

Tanzania haina nia wala mpango wa kuingia katika vita na nchi jirani ya Malawi kufuatia tofauti zao kuhusu mpaka katika Ziwa Nyasa – JK
Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikutana na Rais wa Malawi Mhe. Joyce Banda mjini Maputo Msumbiji leo asubuhi kuzungumzia kutafuta suluhu katika mgogoro wa mpaka kati nchi hizo uliopo kwenye ziwa Nyasa.Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais wa Malawi Mhe. Joyce Banda na wameelezea nia ya nchi zao kufikia suluhu kwa njia za kidiplomasia kupititia kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo (picha na Freddy Maro).
Tanzania haina nia wala mpango wa kuingia katika vita na nchi jirani ya Malawi kufuatia tofauti zao kuhusu mpaka katika Ziwa Nyasa. Rais Jakaya Kikwete amesema hayo leo kufuatia mazungumzo baina yake na Rais aw Malawi, mheshimiwa Joyce Banda.
"Namhakikishia dada yangu na watu wote wa Malawi kwamba hatuna nia wala mpango we kuingia vitani, hatuna matayarisho ya jeshi wala jeshi halijasogea popote kwani hakuna sababu" amesema na kuongeza kuwa "Mimi ndiye kamanda Mkuu wa Majeshi na sijapanga wala kutoa maelekezo ya vita".
Rais amesema hayo, mbele ya Rais Banda na kuongeza kuwa Kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu kuhusu suala la mpaka na tayari maafisa wa pande zote mbili wameshaanza kulizungumzia Kwa nia ya kulitatua Kwa Amani.
"Tuviachie vyombo vyetu vifanye kazi, hebu tuvipe nafasi, wanasiasa na waandishi we habari wajiepushe na maneno haya yanayosababisha taharuki na chokochoko, hayana maana yeyote wwachie diplomasia ifanye kazi yake" Rais amesisitiza.Naye Rais Banda amesema amefurahishwa na kufarijika baada ya kuhakikishiwa kuwa hakuna vita na Rais Kikwete.
"Nimefarijika sana, swala hili limetusumbua sana, mpaka wa-Malawi wote wakaungana na kuwa kitu kimoja na kuzuia tofauti zao" amesema na kuvishukuru vyombo vya habari vya Malawi Kwa kuonyesha uzalendo na ukomavu katika suala hili.Rais Kikwete yuko Maputo, Msumbiji kuhudhuria kikao cha viongozi wa Jumuiya Ya Maendeleo Kusini Kwa Afrika (SADC) uliofunguliwa tarehe 17 August, 2021 na unatarajiwa kumalizika leo jioni ( tarehe 18.august 2012)
Katika kikao cha Jana Tanzania imechukua uenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Afrika ya Kusini ambapo uenyekiti wa SADC umechukuliwa na Msumbiji kutoka Angola, nafasi hizi ni za mwaka mmoja mmoja Kwa zamu.
Imetolewa na Premi Kibanga,Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi.18 August , 2012 Maputo, Msumbiji


No comments: