Friday, August 10, 2012Mawaziri wa Jakaya Kikwete wapingana Bungeni, ni kuhusu wageni wanaofanya kazi kinyume nchini


na Danson Kaijage, Dodoma

KATIKA kile kinachoonekana kama hatua ya serikali kuwakingia kifua wawekezaji wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume na sheria, mawaziri wawili wa Rais Jakaya Kikwete wametoa kauli za kukinzana Bungeni kuhusu uhalali wa wafanyakazi hao katika hoteli ya kitalii ya Holes and Lodges Tanzania Ltd ya jijini Arusha.

Mawaziri hao, Dk. Emmanuel Nchimbi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Dk. Makongoro Mahanga, ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, walitofautiana wakati wakijibu hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA).

Mbunge huyo alimuuliza Waziri Nchimbi mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wabunge wakipitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, akitaka kujua kama serikali inatambua uwepo wa raia wa kigeni ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wageni wanaoishi nchini na kufanya kazi kinyume na sheria, sasa nimemwandikia waziri majina ya watu watatu raia wa India ambao wamekuwa wakiishi na kufanya kazi kwenye kampuni inayomiliki hoteli za Holes and Lodges Tanzania Ltd ya jijini Arusha, ambazo zamani zilikuwa zikimilikiwa na serikali.

“…Na watu hawa wanafanya kazi za kawaida za ufundi na uhasibu, ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, kwa hiyo naomba waziri atuambie wageni hao wanaishi nchini kwa kufuata vibali gani kwa muda huo wa miaka mitano,” alisema Nassari.

Hata hivyo katika ufafanuzi wake, Dk. Nchimbi licha ya kumshukuru Nassari kufanya kazi nzuri ya kuisadia Idara ya Uhamiaji katika mkoa wake, alisema kuwa taarifa alizozitoa na watu aliowataja, ilithibitika kuwa walikuwa na vibali halali vya kuishi nchini na mmoja wao kibali chake kilikuwa kimeisha muda wake.

“Kwa maana hiyo katika kumsaidia mheshimiwa Nassari ili awe anapata data kamili na za kusaidia, namwelekeza kwa Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha atoe ushirikiano kwa kumuelimisha azijue taratibu za uhamiaji,” alijibu Waziri Nchimbi, jambo ambalo halikumridhisha muuliza swali.

Mbunge huyo aliamua kulielekeza swali hilo kwa Wizara ya Kazi na Ajira, wakati wa kupitisha bajeti yao Jumanne wiki hii, ambapo katika majibu yake, Dk. Mahanga alitofautiana na Dk. Nchimbi kuhusu wageni hao.

Katika majibu yake, Dk. Mahanga alikiri kupokea taarifa za kuwepo kwa wageni hao na kuliezea Bunge kuwa, amewahi kufika hotelini hapo mwaka jana na kuamuru wafukuzwe nchini, na hivyo akashangaa kusikia bado wanaendelea kufanya kazi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nakubaliana na mheshimiwa Nassari, na nikiri kwamba natambua kuwepo kwa watu ambao waliingia nchini bila kuwa na kibali chochote, nimefika kwenye hiyo hoteli na nikaagiza waondoke nchini haraka...naagiza tena kuwa tukimaliza kupitisha bajeti yetu hii wawe wameondoka,” alisema Mahanga.

Majibu hayo ya mawaziri yalionekana kuwakoroga wabunge, huku baadhi yao wakihoji inakuwaje waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani hana taarifa za wageni waliowahi kufukuzwa nchini, lakini wakakaidi.

Akizungumza na Tanzania Daima, muda mfupi baada ya Bunge kuahirishwa juzi jioni, Nassari, alisema kuwa pamoja na serikali kudai ilimfukuza mfanyakazi huyo si kweli kuwa aliondoka nchini.

Alisema kuwa kilichofanyika ni kwamba alikimbilia Zanzibar katika hoteli ya kampuni hiyo na kujificha, lakini akasisitiza kuwa kimsingi bado yupo nchini bila kuwa na vibali halili.

Mbunge huyo, alishangazwa na hatua ya viongozi wa serikali kuwa na ujasiri wa kusema uongo bungeni wakati wakijua wazi kuwa mtu kuingia nchini kinyume na taratibu za nchi ni jambo la hatari ambalo linaweza kusababisha maafa makubwa kiusalama.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: