Friday, August 03, 2012



Wanawake wawili wakamatwa JNIA wakipeleka bangi Uturuki



Na Otilia Paulinus, Dar es Salaam

WAKAZI wawili wa Ubungo Shekilango, Sasha Farahani (34) na Khadija Magesa (42), wamekamatwa na Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa tuhuma za kukutwa na kilo 35 za dawa za kulevya aina ya bangi, walizotaka kuzipeleka Uturuki.

Wafanyabiashara hao ambao inadaiwa ni mara yao ya kwanza kusafirisha biashara hiyo, walikamatwa katika uwanja huo Julai 29, 2012, saa tatu usiku, baada ya kukaguliwa katika mabegi yao.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Renatus Chalya, alisema mbinu walizotumia akina mama hao ni kuziweka bangi hizo katika paketi 62 na kuzipanga chini ya sanduku, huku juu yake wakiwa wamepanga nguo zao za kuvaa.
 

“Bangi hizo zilikamatwa sehemu ya Screening Machine eneo la Terminal II, ambalo linahusika na upekuzi wa mizigo na hapo ndipo Askari wa zamu, Damian No D.1974 D/SSG7 alipolitilia shaka sanduku hilo.
 

“Walisaidiana na walinzi wa uwanja kwa kupekua na kufanikiwa kupata bangi hiyo ambayo walikuwa wanataka kusafirisha nje ya nchi kwenda kuiuza,” alisema Chalya.
 

Hata hivyo, alisema hali ya ulinzi na usalama inazidi kuimarika katika viwanja vya ndege, hivyo si rahisi kwa mtu yeyote kutaka kusafirisha biashara haramu kupeleka nje ya nchi bila kukamatwa.
 

Alisema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kujibu shitaka linalowakabili.

Chanzo: Mtanzania

1 comment:

Anonymous said...

Malimbukeni kweli hao wanawake! Wanafikiri wangeshuka Ankara bila kukamatwa? Hawajui walinda mipaka siku hizi wako makini na mbinu zinazotumiwa na wavusha madawa? Wangekuwa wanafuatilia vipindi vya mbinu zinazotumiwa na wavusha madawa kuona jinsi watu wanavyojaribu kila mbinu na wanakamatwa wasingethubutu kukubali kubeba hizo bangi!