Sunday, September 16, 2012

Mauaji ya Daudi Mwangosi: Ushuhuda wa kilichotokea hadi kifo chake


SEPTEMBA 2, 2012, polisi waliua kikatili mwandishi wa habari wa kituo cha Channel TEN, Daudi Mwangosi, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa. Alikufa mbele ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, wakati polisi hao walipovamia ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuwatawanya wasifungue tawi la chama chao katika kijiji hicho.

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio zima, ni mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Khamis. Ifuatayo ni simulizi ya kile alichokiona wakati polisi wanaondoa uhai wa Mwangosi.

SIKU hiyo asubuhi tulipata taarifa kuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo (RPC), Michael Kamuhanda, alipanga kukutana na waandishi wa habari majira ya saa 2.30 ambapo waandishi walifika akiwemo Daudi Mwangosi.

Tukiwa katika chumba cha mikutano katika jengo la polisi Mkoa wa Iringa, Kamanda wa mkoa huo, alifika akiongozana na maafisa wake wawili na kuanza kutusomea taarifa ya zuio la mikutano ya CHADEMA iliyokuwa iendelee siku hiyo baada ya kupisha zoezi la awali la sensa.

Alitusomea zuio hilo na kutuambia hata viongozi wa CHADEMA wameshataarifiwa usiku wa Septemba Mosi. Tukamuuliza mbona taarifa za sensa zinaeleza kuwa kuna mafanikio kwa asilimia 95 na waliobaki wanatakiwa waende kwa viongozi wao? Akatujibu kuwa hilo ni agizo na linapaswa litekelezwe na CHADEMA.

Waandishi hawakuchoka kumuuliza maswali RPC na moja ya maswali yaliyoonekana kumkera kamanda huyo ni lile lililotoka kwa Daudi Mwangosi kuwa mbona wakati wa mwanzo walipozuia mikutano ya CHADEMA mkoani humo mikutano mingine ya CCM ndani ya mkoa huo na sehemu nyingine nchini ilikuwa inaendelea.

Swali lingine la Mwangosi lilimtaka kamanda huyo kutumia busara katika hali iliyopo kwa lengo la kuepusha maafa yanayoweza kutokea endapo angeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakuna mkutano wa aina yoyote utakaofanyika.

Baada ya maswali hayo, tulimuona Kamanda Kamhanda akiwa amekunja sura kama ishara ya kuchukizwa na maswali ya Mwangosi ambaye aliongeza swali lingine kwamba, “inaonekana Kamanda umechukia kutoka ndani ya moyo wako” na kamanda akajibu “ni lazima nichukie na nawachukia hawa CHADEMA kwa kuwa ninaipenda kazi yangu na pia ninakaribia kustaafu na sitaki kustaafu vibaya.”

Baada ya hapo maafisa waliokuwa na RPC waliandika ujumbe kwenye karatasi na wakamfikishia mkuu wao, na baada ya muda mkutano huo ulimalizika huku kukiwa na kauli za utani wa hapa na pale kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari juu ya kwenda kuripoti matukio ya siku hiyo.

Tulipokuwa nje ya jengo, Mwangosi, kwa kuwa ni mwenyeji wa mkoa huo, alikuwa akitaniana na mmoja wa askari aliyevaa kiraia, ambaye alimwambia kuwa, “huko hakutakuwa na kujuana na kuna uwezekano wa watu kufa.”

Mwangosi alijibu papo hapo kuwa hilo haliogopi kwa kuwa kifo ni ada ya mja yeyote na kwamba ataogopa kama mtu atamuahidi kuishi milele.

Baada ya hapo, kila mmoja alitawanyika katika eneo lake, na majira ya saa saba mchana baadhi ya waandishi walikutana ili kuanza safari katika Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya kuripoti mkutano wa ndani wa CHADEMA na ufunguzi wa matawi.

Waandishi wa habari hao pamoja na mimi ni Godfrey Mushi (Nipashe), Olver Motto (Star Tv), Renatus Mutabuzi (ITV), Clement Sanga (Mwananchi), Joseph Senga (Tanzania Daima) na Tumaini Makene (Ofisa Habari wa CHADEMA).

Tulipofika katika mji wa Mafinga, tulipata chakula cha mchana kabla ya kwenda katika Kijiji cha Nyololo, na muda wote huo Mwangosi alikuwa hajaungana nasi.

Tuliondoka Mafinga kuelekea Nyololo huku mwenzetu Clement Sanga akiwasiliana na Mwangosi aliyesema yuko katika basi na angeungana nasi tukiwa Nyololo. Tulipofika pale tuliona askari wachache wakiwa wamesimama barabarani huku gari lao moja likiwa linajaza mafuta katika kituo cha mafuta kilichopo eneo hilo.

Tukiwa njia ya kwenda Mbeya, mita kama 100 kutoka katika mji wa Nyololo, kushoto kwetu tuliziona ofisi za CHADEMA zikiwa zimepambwa kwa bendera nyingi, na kulia kwake tuliona magari manne ya askari waliokuwa na silaha.

Baada ya kupita eneo hilo, gari moja la polisi lilikuwa likitufuata, na hapo tulishauriana kugeuza gari kurudi katika eneo la mji. Tulipofanya hivyo, na gari la polisi lilisimama.

Wakati tunarudi katika eneo la mji, tuliegesha gari pembeni. Baadhi ya waandishi wa habari waliingia mitaani kwa makubaliano kuwa baada ya dakika 10 tuwe tumerejea kwa ajili shughuli iliyotuleta – kushuhudia ufunguzi wa tawi hilo jipya la CHADEMA.

Muda huo ulipofika, tulirejea, lakini Mwangosi alikuwa hajaungana nasi. Baadaye tulianza kuona baadhi ya magari yakiwa na bendera ya CHADEMA yakipita moja baada ya jingine.

Kuwasili kwa Mwangosi eneo la Nyololo

Saa 10.22 Mwangosi aliwasili kwa basi ambalo sikumbuki kama ni Hood au Abood; na muda huo huo tukawaona askari wakiyatoa magari yao kutoka mafichoni na kuingia upande wa kulia wa mji wa Nyololo kwenye ofisi za kata za CHADEMA.

Wakati askari wakiwa wanapita walikuwa wakisema Dk. Slaa anatokea eneo la Wami. Waandishi wa habari wakawa wamejiandaa kwenda kwa kufuata njia hiyo.

Tuliegesha gari letu mbali. Mwangosi ambaye hakuwepo awali, akataka kuchukua pikipiki ili awahi. Kwa kuwa muda huo nilikuwa naye, nikamsihi kuwa hana haja ya kuingia gharama kwa kuwa gari la waandishi wa habari lipo. Akanielewa, na tukaingia katika gari hilo, huku akiwa amempakata Oliver Motto wa Star Tv.

Tulipoenda kama mita 50 hivi, tulikutana na msafara wa CHADEMA ukiwa unaelekea tunakotoka. Gari la waandishi wa habari na magari ya polisi yakalazimika kukaa pembeni kuyapisha, kisha wakaungana nao kuelekea katika ofisi za tawi za chama hicho.

Ofisi za tawi za CHADEMA katika mji huo wa Nyololo zipo mita zaidi ya 100 upande wa kushoto wa bararara ya kuelekea Mbeya. Awali polisi walikuwa wameegesha magari yao barabarani wakati CHADEMA wakielekea katika ofisi zao.

Hakukuwa na vurugu yoyote. Ghafla kiongozi wa polisi ambaye alikuwepo pale – tulimtambua kwa jina la Mnunka – aliwaamuru askari wake watoe ilani kwa kunyoosha bendera kubwa nyekundu juu na kuwataka CHADEMA waondoke katika ofisi zao. Tukapiga picha tukio hilo.

Wakati askari wakijiandaa kuwafuata wana CHADEMA katika ofisi zao, alitokea mtu aliyevaa shuka na kujifunga kitambaa kichwani ambaye baadaye alijitambulisha kama mkuu wa upelezi mkoa (RCO), akawaamuru wenzake waende katika ‘target’ lakini wasithubutu kutumia nguvu bila amri.

Hapa ndipo tulipoanza kupata wasiwasi ni nani anatoa amri kwa kuwa yule wa mwanzo, Mnunka alijiapiza kuwa wamechoka kuvumilia, na kwamba siku hiyo CHADEMA watawatambua. Hata tulipomuuliza maana ya kauli ile, hakutupa jibu la kueleweka.

Katika hali hiyo, mtu aliyejitambulisha kama ndie RCO alizungumza na viongozi wa CHADEMA, wao wakamwambia wako katika kikao cha ndani. Yeye akasema jukumu lake ni kuhakikisha usalama unakuwepo, na kwamba kama ni suala la kikao cha ndani hawawezi kuzuia.

Tulitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kutoka kwa RCO ambaye alikuwa akizungumza kwa simu na mtu ambaye baadaye ilikuja kubainika kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), akawa anamueleza kuwa hali ni salama. Alituahidi waandishi wa habari tuvute subira “kwa kuwa mwenye mkoa amewasili.”

Baada ya kuwasili kwa RPC Kamuhanda, Kamanda wa FFU, Mnunka alienda akamnong’oneza jambo. Pale pale, Kamuhanda akaonekana kukasirika. Akaagiza CHADEMA wasimamishe shughuli yao mara moja.

Tulitaka kujua tafsiri ya mkutano wa ndani kwa Jeshi la Polisi ni ipi, ni kwa wahusika kukaa ndani au ni ule mkutano utakaowahusisha wanachama peke yao kama ambavyo CHADEMA walikuwa wanasema pale. RPC akatujibu kuwa hilo halielewi na yeye si mwanasiasa.

Baada ya maelezo hayo, waandishi wa habari tulimbana RPC kwa maswali hata ikafikia hatua ya kamanda huyo kuanza kuwanyooshea vidole baadhi yetu, huku alimlalamikia Mwangosi kwamba kwanini hakushiba na majibu aliyopewa tangu asubuhi.

RPC akaniambia mimi kwamba nauliza maswali yanayopingana na mtazamo wa jeshi hilo; akamwambia Mutabuzi kuwa anamfahamu.

Baada ya hali hiyo, CHADEMA walimaliza mkutano wao katika ofisi za tawi na wakawa wanaelekea katika ofisi za kata. Gari lililotubeba lilikuwa nyuma ya gari la RPC ambaye baadaye dereva wake aliendesha kwa kasi kwenda mbele kutaka kuzuia msafara wa CHADEMA.

Lakini viongozi wa CHADEMA walikuwa wameshafika katika ofisi yao ya kata na tukashuka kwenda kushuhudia kinachoendelea. Hapo ndipo tulimkuta Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zanzibar, Hamad Yusuph na viongozi wengine wakisaini katika kitabu cha wageni.

Ghafla, RPC akatoa amri ya kuwakamata viongozi wa CHADEMA waliokuwa katika ofisi yao. Baada ya amri hiyo, wanachama wa CHADEMA waliokuwa pale wote walikaa chini wakinyoosha mikono juu.
Balaa linaanza kwa amri ya RPC Kamuhanda

Baada ya RPC kutoa amri hiyo, polisi walioipokea walianza kurusha mabomu ya machozi kuelekea sehemu waliyokaa wanachama wa CHADEMA. Mabomu hayo yalirushwa na kuumiza wengi, wakiwamo waandishi wa habari. Mimi nilipigwa na kitu chenye kishindo, nikajeruhiwa mkono wa kushoto na sehemu ya paja la mguu wa kulia.

Jitihada za polisi kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA zilifanikiwa. Baadhi ya watu na viongozi waliwekwa chini ya ulinzi, sisi tukiwa tunaendelea kufanya kazi yetu ya kukusanya taarifa ili kuhabarisha umma juu ya kile kinachoendelea katika eneo hilo.

Wakati hali hiyo ikiendelea, ofisi za kata za CHADEMA hazikuwa na mtu. Askari wakawa wanapiga mabomu kuelekea ndani ya ofisi hiyo tupu.

Tuliendelea kupiga picha tukio hilo. Ghafla askari mmoja akamgeukia mwandishi wa gazeti la Nipashe, Godfrey Mushi, akaanza kumpiga.

Baada ya kuona mwandishi huyo anapigwa, Mwangosi aliwasogelea askari akitaka kujua sababu za kumshambulia mwandishi wakati yupo kazini kama ambavyo askari hao walivyokuwa wakiwajibika.

Swali la Mwangosi likavuta askari wengine. Wakamzunguka na kuanza kumpiga kwa marungu, mateke na ngumi. Wakati hayo yakifanyika, RPC alikuwa pale anashuhudia.

Baada ya kuona kipigo kimekuwa kikali, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Mafinga aliingilia kati kutaka kumnusuru Mwangosi.

Wakati Mwangosi akiwa anashambuliwa, mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga, naye alikuwa katika wakati mgumu baada ya askari kumdhibiti na kuanza kumpekua mifukoni, huku mwenyewe akijitahidi kujinasua mikononi mwao.

Mbali na mimi na Senga, muda huo hakukuwa na raia yeyote katika eneo lile, isipokuwa Godfrey Mushi wa Nipashe ambaye sina hakika kama alikuwa anafahamu kinachoendelea maana alikuwa amepigwa sana, yuko hoi.

Baada ya kuona kipigo kinazidi kwa Mwangosi huku Senga akiendelea kupiga picha, uzalendo ulinishinda, nikaamua kumfuata Kamanda wa Polisi mkoani humo aliyekuwa mita zisizozidi kumi ndani ya gari lake, akishuhudia tukio lile. Nikamuomba asaidie kumnusuru Mwangosi na kipigo kile.

RPC alishusha kioo cha gari lake, akaniangalia, kisha akafunga kioo, huku dereva wake akawa anapiga honi. Sikujua maana ya honi hiyo.

Baada ya kuona hakuna msaada wowote kutoka kwa RPC, nilisogea karibu kwa ajili ya kuendelea kupata picha ya tukio, ili umma ujue juu ya madhila yanayowapata waandishi wa habari mikononi mwa polisi.

Wakati nikiwa naendelea kuchukua picha, nilimwona askari mmoja akinyoosha mkono juu na mwingine aliyevaa kiraia akiwa ameshika bastola yake kuelekeza juu, huku wengine wakiwa wanaendelea kumpiga Mwangosi aliyekuwa anajitahidi kuinuka kwa kumshika mmoja wa askari wale.

Katika harakati za Mwangosi kujinasua, nilimshuhudia mmoja wa wale askari akiwa kama anainama akaelekeza mtutu wa bunduki usawa wa tumbo la Mwangosi aliyekuwa katika hali ya kutaka kusimama huku akipiga kelele “msiniuee, msiniuee…”

Mara nikasikia mlipuko mkubwa pale pale walipo; baadhi ya nyama zikarushwa na kutapakaa, nyingine zikanirukia mimi na kuchafua fulana yangu.

Kumbe walikuwa wamemlipua Mwangosi! Nikapiga picha ya mwili uliosambaratika na kukatika vipande vipande. Nikaona askari wale wanambeba askari ambaye naye alijeruhiwa na mlipuko uliomuua Mwangosi. Nikakimbia kujinusuru na askari wale.

Sikuona tena usalama wangu mbele ya polisi wake. Sikumwamini tena RPC kama angeweza kulinda maisha yangu. Nikatimua mbio kuelekea nisipopajua.

Nikiwa nakimbia nilichomoa kadi ya kamera kutoka katika kamera yangu ili nisipokonywe. Hapo ndipo nilipokutana na mwandishi mwingine, Francis Godwin, nikamwambia asielekee nilikokuwa natoka mimi – ambako ndiko alikuwa anataka kwenda – kwa kuwa Mwangosi ameshauawa na polisi!

Wakati naachana na Godwin, nilichukua simu yangu na kumpigia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, ambaye ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti hili kwa ajili ya kumpa taarifa. Bahati mbaya simu yake haikupokelewa.

Nikamfuata Makene (Tumaini, afisa habari wa CHADEMA) aliyekuwa amejikinga katika gogo, alikokuwa pamoja na Oliver Motto, nikawaambia eneo hili halitufai watatuua. Ndipo nikampigia simu Bakari

Kimwanga, mwandishi wa gazeti la Mtanzania, nikamfahamisha kuwa Mwangosi ameuawa na polisi. Tukakimbilia porini kujificha, kila mtu akiwa analia kivyake.

Baada ya kukaa porini kwa muda, tuliamua kubadilisha nguo zetu ili tusitambulike kirahisi. Tukatoka mafichoni kuangalia hali ya usalama. Tukaanza kuwatafuta wenzetu ambao tulipoteana nao. Baadaye tulikodi teksi kuwafuata wenzetu ambao wakati huo walishakimbia kutoka eneo hilo la hatari.

Tukiwa katika hoteli ya MR mkoani Iringa, mwananchi mmoja alikuja kutueleza kuwa alifanikiwa kukusanya sehemu ya mwili wa marehemu Mwangosi pamoja na mabomu yaliyoachwa katika eneo la tukio na walipoangalia wakaona ni sehemu ya nyama ya utumbo iliyowekwa katika mfuko pamoja na mabomu ya machozi na kuyapanga yale mabomu juu ya meza ya hoteli hiyo na kuyapiga picha huku utumbo wa Mwangosi ukiendelea kuwa katika mfuko uliowekwa.

Hadi sasa sijajua endapo sehemu hiyo ya utumbo ilizikwa usiku ule mkoani Iringa au uliunganishwa na sehemu nyingine ya mwili wake uliotawanywa na bomu hilo kiasi cha kushindwa kujua kama ni mwili wa binadamu au ni ng’ombe aliyechinjwa tayari kwa mauzo.

Hivi ndivyo tulivyompoteza mwandishi mwenzetu, Daudi Mwangosi, akiwa mikononi mwa polisi.


Chanzo: http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/320875-mauaji-ya-daudi-mwangosi-ushuhuda-wa-kilichotokea-hadi-kifo-chake.html 

No comments: