Sunday, September 30, 2012

Tanzania yaishtaki Malawi, Umoja wa Mataifa


 
HATIMAYE Tanzania ’imeishitaki’ Malawi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa haina mpango wa kuingia vitani kwa ajili ya kugombania mpaka ndani ya Ziwa Nyasa.

Badala yake imesema itawasilisha madai yake katika Mahakama ya Kimataifa yenye dhamana ya utatuzi wa mgogoro iliyo chini ya umoja huo ambayo itakuwa na uamuzi wa mwisho wa mpaka huo.

Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa kauli hiyo wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 67 Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Alisema Tanzania imekuwa mpatanishi mkuu wa migogoro mbalimbali duniani ukiwamo wa Burundi uliokuwa ukisimamiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na kamwe haitakuwa kielelezo kibaya cha kudai inachokiamini kwa kutumia nguvu.

"Ushiriki wa marais wetu wastaafu kuanzia Hayati Nyerere, Benjamin Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete katika kutatua migogoro mbalimbali, ni sababu tosha ya kuifanya duniani iamini njia sahihi kwa Tanzania kutatua mgogoro ni kwa diplomasia tu," alisema Waziri Membe.

Kuhusu migogoro inayoendelea sehemu mbalimbali duniani, Membe alisema kushindwa kuvumiliana kwa wanaopingana katika nyanja tofauti kumekuwa sababu kuu ya kuzidisha migororo, jambo ambalo linahatarisha usalama wa watu na mali zao.

Membe ameuomba Umoja wa Mataifa kutafuta njia ya dharura ya kutatua mgogoro unaoendelea Syria kati ya majeshi ya Serikali na yale yanayompiga Rais Bashar Al Assad, kutokana na athari kubwa iliyojitokeza katika taifa hilo.

"Mheshimiwa Rais wa baraza hili, wote tunajua madhara ya migogoro na vita hasa maazimio ya Umoja wa Mataifa yanapokiukwa kama tunavyoona Syria.Hii ni moja kati ya mifano lazima tuwe makini kufikiria mapema njia za kutatua migogoro kabla ya madhara kutokea," alisema.

waziri Membe pia alisema kuwa Tanzania na nchi nyingine 12 zinazounda Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), zimekubaliana kuunda jeshi la pamoja na kukituma kikosi cha askari 4,000 kwa ajili ya kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mtanzania, Jumapili, 30.Septemba 2012



No comments: