Sunday, December 30, 2012

Afrikanere i Norge gjennom 400 år. Miaka 400 ya Waafrika Norway


Mwaka jana Yacoub Cisse (pichani) amechapisha kitabu kiitwacho "Afrikanere i Norge gjennom 400 år" (Miaka 400 ya Waafrika nchini Norway - tafsiri yangu).

Chanzo cha kitabu hiki kilianzia mwaka Novemba 1996. Nilikuwa natembea kupitia mtaa wa Akers (Akersgata) nikapitia kwenye ofisi ya gazeti la VG na kusoma habari kuhusu Burundi/Rwanda/Kongo na nchi za Balkan. Picha ya kusikitisha ya nilichokuwa nakisoma. Sikupenda nilichokuwa nakisoma. Nikajiwa na wazo la kubadili picha hiyo. Nikataka kufanya onyesho la Waafrika waliofanikiwa hapa Norway.

Tatizo lilikuwa: Wapi nitaanzia? Je, kuna sehemu yoyote au masjala ya bayana yoyote naweza kwenda kuchambua historia ya Waafrika hapa Norway?

Kipindi hicho, niliona kulikuwa kunachorwa picha hasi za Waafrika na nilitaka kufanya kitu kitachoonyesha picha chanya. Nilikuwa na wazo zuri lakini ilikuwa kazi kubwa kweli. Nilikuwa mtupu wa pa kuanzia.

Niliamua kuanzisha asasi niliyoiita "Anta Diop Project" na baadae niliibadilisha jina na kuiita "organisasjonen Afrikanere i Norge".

Historia ya kwanza niliipata kibahati bahati:

Mwaka 1997 nilikutana na msanii/mchoraji mtaani Oslo. Ndo kwanza nilikuwa nimetoka London kwenye maonyesho yanayoitwa "Black Child Conference" na nilinunua picha kadhaa za kuchorwa. Nia yangu ilikuwa kumwuzia huyo mchoraji hizo picha. Lakini hakuwa kabisa na hamu ya picha, bali alitaka kujua historia yangu. Aliniuliza; unatoka wapi? Nikamjibu: Mimi ni raia wa hii dunia. Akaendelea: Nimekuuliza hivyo kwa sababu shangazi yangu ni "neger". Unaweza kuzungumza nae kama unapenda (Neger ni neno ambalo halitumiki siku hizi ni sawa ni kumwita mtu mwenye asili ya bara la Afrika "nigger")  sikutilia maanani neno "neger". Niliingiwa na hamu ya kuzungumza na huyo shangazi yake. Baada ya siku kadhaa nikampigia huyo shangazi yake anayeitwa Ida Anderson. Alikuwa anakaa maeneo ya Grunnerløkka. Alizaliwa Oslo mwaka 1925 (Kipindi hicho Oslo ilikuwa inaitwa Kristiania).

Historia ya pili na yenyewe niliipata kibahati:

Ilikuwa historia ya Anne Johansen, niliyekutana nae kibahati kwenye kituo cha basi cha IKEA Furuseth Desemba 1998 kabla ya Krismasi. Nilikuwa nimechacha kweli. Nimetoka IKEA kumnunulia zawadi ya Krimasi binti mdogo wa rafiki yangu. Anne Johansen akawa anasema: "Watu wanatumia hela nyingi kununua zawadi za Krimasi bila sababu." Sikumsikia vizuri, kwa sababu mawazo yangu kwenye hela kidogo nilizobaki nazo baada ya kununua zawadi ya Krimasi. Wakati tukiwa ndani ya basi, Anne Johansen akaendelea "Nina shoga yangu mwenye rangi kama yako anaitwa Jossie Pollard ana miaka kwenye thelathini hivi.

Baada ya muda nikawasiliana na kaka wa Jossie anaitwa Pete Brown...

Baada ya hapo nikaendelea na mradi wa uandishi wa kitabu hiki. Kilichukua muda kumaliza kwa sababu mbali mbali..

Madhumuni hasa ya kuandika kitabu hiki "Afrikanere i Norge gjennom 400 år" ni kuwakilisha historia ya Waafrika nchini Norway kwa miaka 400. Kuwa uhamiaji wa Waafrika kuingia hapa Norway haukuanzia miaka ya 60 kama wengi wanavyodhania.

Je, unajua kuwa Christian Hansen  alikuwa Mwafrika na alikuwa PostaMasta wa Kragerø mwaka 1681?

je, unajua mchoraji maarufu Mnorweji Edvard Munch amemtumia Mwafrika kwenye picha zake maarufu sita alizochora?

Ni kitabu ambacho kinapaswa kusomwa na kila mtu.

Kitabu kinapatikana kwenye maduka ya kuuza vitabu: Tanum Oslo City na Grønland, Ark, Notabene na Akademica.

Au unaweza kuagizia moja kwa moja kwa kutuma baruapepe kwa: cisse208@yahoo.no

Unaweza pia kutuma SMS kwenye namba: +47 45 67 06 69

facebook: http://www.facebook.com/#!/afrinboka

Imeandikwa na Semboja, Mwamedi Juma4.


No comments: