Saturday, March 02, 2013

Tafakuri jadidi - Kikwete anapoomba msaada wa mashushushu wa FBI…!..WIKI jana niliandika na kusema kwamba, tangu Mwalimu Nyerere afariki dunia, tumesahau kujitawala, na kwamba tunapaswa kujifunza upya namna ya kujitawala wenyewe.

Nilisema kuwa ushahidi kwamba tumesahau namna ya kujitawala wenyewe ni jinsi tunavyoshabikia mikopo na misaada kutoka nje hata kwa yale mambo ambayo yamo ndani ya uwezo wetu wenyewe kuyatenda.

Nilisema kwamba hali ya utegemezi imefikia pabaya kiasi kwamba sasa kijiji kinadiriki kuomba fedha za mfadhili ili kujenga choo cha shule au kuomba fedha za Mzungu ili kujenga bwawa la kufugia samaki!

Ilikuwa niufunge mjadala huu wa suala hili la utegemezi (dependency syndrome), lakini wiki iliyopita nilipata mfano mwingine mzuri zaidi wa jinsi tunavyobweteka kiasi kwamba kila tatizo linaloibuka nchini mwetu tunaomba misaada ya wageni kutusaidia kulitatua; hata kwa yale masuala yanayohusu ulinzi na usalama wetu wenyewe!

Naamanisha kitendo cha wiki iliyopita cha Serikali ya Rais Kikwete kuomba msaada wa mashushushu wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kuwakamata waliohusika na mauaji ya Padri Evaristi Mushi yaliyofanyika Februari 17 kule Zanzibar.

Kwa yeyote yule mwenye kufikiri sawasawa, hatua hiyo ya Serikali ya Kikwete inaweza kuwa na tafsiri mbili. Ya kwanza ni kwamba pengine Rais alitaka kuuonyesha umma wa Watanzania kwamba amekerwa na kufadhaishwa mno na mauaji hayo, na ndiyo maana amewaita hata mashushushu wa FBI ili wahusika wakamatwe haraka.

Lakini tafsiri ya pili inaweza kuwa kwamba Rais wetu Kikwete anajua moyoni udhaifu mkubwa wa Jeshi letu la Polisi na idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) kiasi kwamba anaamini kuwa vyombo hivyo haviwezi kuwakamata wauaji wa Padri Mushi bila kusaidiwa na mashushushu wa FBI.

Vyovyote vile; hebu tuzijadili tafsiri zote mbili na kuona zinatufundisha nini au zinaashiria nini. Tafsiri ya kwanza kwamba amewaita mashushushu hao wa FBI ili kuwaonyesha Watanzania kuwa anajali na amekerwa mno na mauaji hayo, haina mashiko makubwa.

Haina mashiko makubwa kwa sababu hiyo siyo mara ya kwanza kwa kiongozi wa kanisa nchini kuuawa na waumini wa dini ya kiislamu wenye hisia kali dhidi ya ukristo.

Kwa hakika,ni hivi karibuni tu ambako Mchungaji Mathayo wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God aliuawa kule Buseresere, Geita na waumini hao hao wa Kiislamu wenye hisia kali dhidi ya ukristo.

Na hata huko Zanzibar kwenyewe, ni mwaka jana tu (Desemba 25) Padri mwingine, Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Tomondo, alinusurika kufa baada ya kupigwa risasi kichwani na waumini hao hao wa Kiislamu wenye hisia kali dhidi ya ukristo.

Sasa, kama matukio hayo yalitokea na hatukumsikia Mheshimiwa Rais akiwaita mashushushu wa FBI, inakuaje tukio la mauaji ya Padri Mushi, awaite? Naamini mpenzi msomaji unaweza kuwa na jibu lako mwenyewe kwa swali hilo!

Tukirejea kwenye hoja ya pili kwamba pengine Rais ameomba msaada wa mashushushu wa FBI kwa sababu hana imani na vyombo vyake mwenyewe vya ulinzi na usalama – yaani Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), hapa kunaweza kukawa na mantiki kubwa, lakini inayoanika udhaifu mkubwa kwake wa kiutendaji.

Nasema hivyo, kwa sababu takriban miaka mitano sasa Watanzania wamekuwa wakilalamika mno kuhusu udhaifu wa vyombo hivyo, lakini Rais Kikwete amekuwa akiziba masikio yake juu ya malalamiko hayo. Kwa mfano; mara kadhaa Jeshi lenyewe la Polisi limehusishwa na mauaji ya raia wasio na hatia. Usalama wa Taifa nao umehusishwa na kashfa kubwa ya ufisadi wa fedha za EPA.

Ni kwa sababu ya madoa kama hayo vilio kuhusu kufumuliwa na kuundwa upya kwa Jeshi la Polisi na TISS (Usalama wa Taifa) vimekuwa vikubwa.Vyama vya siasa vimelalamika, NGOs zimelalamika, asasi za dini zimelalamika, waandishi wa habari kupitia safu mbalimbali wameandika na kulalamikia asasi hizo mbili za dola, na hata wananchi wa kawaida nao wamelalmika; lakini Mheshimiwa Rais amechagua kuziba masikio yake juu ya kelele hizo.

Na hata sasa ambako kelele hizo zimeongezeka maradufu baada ya Padri Mushi kuuawa kule Zanzibar, Rais bado amewakumbatia watendaji wakuu wa asasi hizo mbili muhimu.

Na katika hali ya kushangaza kabisa, anawaita mashushushu wa FBI kufanya kazi ambayo ilipaswa kufanywa na asasi zetu hizo mbili za nyumbani. Anawaalika mashushushu wa FBI kumsaidia hata kabla hajawawajibisha mabosi wakuu wa asasi zetu hizo!

Hiyo maana yake ni nini? Hiyo maana yake ni kwamba sasa dependency syndrome ya Serikali yetu imefikia mahali ambapo tunahitaji msaada wa FBI hata katika masuala yanayohusu ulinzi na usalama wetu wenyewe ambayo tuna uwezo nayo kuyashughulikia.

Au kuna asiyeamini kuwa kama kungekuwa na dhamira ya kweli (na si kucheza “usanii”), maofisa wetu wa Jeshi la Polisi na TISS wasingeshindwa kubaini mapema mipango ya mauaji ya Padri Mushi na Mchungaji Mathayo, na hivyo kuizima kabla mauaji hayajatekelezwa? Vivyo hivyo jaribio la kumuua Padri Ambrose.

Nijuavyo mimi, kama kungekuwa na dhamira ya kweli, mauaji hayo yasingetekelezwa; kwani viashiria vya mauaji hayo kuwa yangefanyika vilikuwa vingi kiasi cha kuwezesha kuyazuia mapema.

Kwa mfano, kwenye mtandao wa kijamii wa facebook wa kikundi cha Uamsho cha kule Zanzibar, kulikuwa na postings zinazochochea Waislamu wenye hisia kali kuwadhuru viongozi wa makanisa kule Zanzibar, lakini TISS na Jeshi la Polisi, hawakufanya lolote kuhusu viashiria hivyo.

Aidha, nina hakika maofisa wa TISS na polisi wetu wanasoma mtandao huo, na kwamba wanasoma hata na magazeti yao,na hata kusikiliza jumbe kwenye u-tube, redio zao, CD na video za mahubiri ya kidini ya chuki, lakini pamoja na kufanya hivyo, mpaka sasa hatujasikia operesheni yoyote maalumu waliyoianzisha ya kuwanasa wahusika.

Na ndiyo maana sasa wahusika hawaishii tu katika kutoa tu mahubiri ya chuki dhidi ya dini nyingine; bali wamekwenda mbali zaidi na kufikia hata hatua ya kutoa roho za watu wengine!

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, kukoswakoswa kuuawa kwa Padri Ambrose na mauaji ya Padri Mushi na Mchungaji Mathayo, si vitu vilivyotokea kwa ghafla tu. Viashiria vyake vilikuwepo kwa muda mrefu, na polisi wetu na maofisa wetu wa TISS, waliviona lakini hawakujali kuchukua hatua zozote, na matokeo yake ni kwamba mauaji yalitekelezwa, na yalipotekelezwa ndipo Serikali inakurupuka hadi kuwaita FBI kuchunguza!

Hivi kweli tunahitaji utaalamu wa FBI kuwakamata wauaji hawa hapa nchini wenye mwelekeo wa kigaidi wa Al Qaeda au Al Shabab? Hivi kweli tunahitaji mashushushu wa FBI kutuelemisha kwamba kama tungedhibiti kikundi hiki cha Uamsho, kama tungedhibiti mahubiri ya kidini ya chuki, redio za chuki, magazeti ya chuki, kanda na video za chuki, tungeweza kuzuia (pre empty) mapema mipango ya mauaji hayo isitekelezwe? Kweli tunahitaji mgeni kutwambia hilo?

Ndugu zangu, ni mtazamo wangu kwamba kama Rais Kikwete ameomba msaada wa mashushushu wa FBI katika suala hili la muaji ya Padri Mushi, ni kwa sababu tu amezoea kuomba misaada ya nje, lakini si kwa sababu vyombo vyetu vya dola haviwezi kuwakamata wahusika au kuzuia mauaji kama hayo yasitokee kama vingekuwa na dhamira ya kweli ya kufanya hivyo.

Ni kwa nini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama (TISS na Polisi) havina dhamira ya kweli ya kudhibiti chuki za kidini zinazoenezwa kwa kasi nchini, ni jambo ambalo, mpaka leo, linasumbua kichwa changu kupata jibu.

Yaani sina jibu lake au fununu ya jibu lake! Vipeperushi vinavyohubiri chuki dhidi ya Ukristo vinasambazwa, lakini hakuna anayekamatwa. Mtu anamwaga sumu kwenye u-tube au kwenye facebook ya chuki za kidini zinazohamasisha umwagaji damu kutokea, na vyombo vyetu vya dola vipo na vinaona; lakini hakuna anayekamatwa.

Kuna redio kutwa nzima zinahubiri chuki za kidini, na vivyo hivyo magazeti kadhaa. Kuna maduka yanauza CD na kanda zenye mahubiri ya chuki za kidini, na hata wengine wanaziuza nje ya nyumba za ibada, lakini hakuna wanaokamatwa au vyombo vya habari vinavyojihusisha na kusambaza chuki hizo vinavyofungiwa.

Aidha, kule kwenye kisiwa cha Ukerewe kuna chuo cha kigeni kimefunguliwa ambacho tumefahamishwa kuwa wanafunzi hufundishwa karate na judo na matumizi ya silaha kadhaa. Licha kwamba habari hizo za uchunguzi zimeripotiwa kwa kina na gazeti la Mtanzania, lakini hakuna hatua zozote zimechukuliwa na TISS au na Polisi kuishauri Serikali kukifunga chuo hicho.

Kwa ufupi, Serikali hii ya Rais Kikwete haichukui hatua madhubuti juu ya mambo yote hayo yanayohatarisha usalama wa nchi yetu, na kisha mauaji ya kidini yanapotokea, inakimbilia Marekani kuomba msaada wa mashushushu wa FBI!

Hivi tunasubiri kuambiwa na mashushushu wa FBI kwamba kule kisiwani Ukerewe kuna chuo kitakachozalisha mabingwa wa kueneza chuki za kidini na wafuasi wa Al Qaeda na Al Shabab ndipo Serikali ichukue hatua ya kukifunga?

Tuambizane ukweli. Hapa kwetu Tanzania, Serikali yetu katika suala la kudhibiti viashiria na matukio ya udini, imekuwa legelege sana. Mafundisho ya kujenga chuki na kuhimiza mauaji yamekuwa yakifanywa wazi lakini Serikali haichukui hatua zozote za msingi na za kuweza kuonekana.

Tumefikia pabaya kiasi kwamba mwaka jana peke yake zaidi ya makanisa 20 yalichomwa moto na baadhi ya waumini wa kiislamu wenye hisia kali dhidi ya Ukristo.

Na pengine ni kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi hiyo ya makanisa yanayochomwa moto baadhi ya viongozi wa makanisa na baadhi ya waumini wao nao wameanza kujibu mapigo kwa kuendesha mahubiri ya chuki dhidi ya Uislamu, na bado vyombo vyetu vya dola vimelala usingizi.

Kama alivyosema mchangiaji mmoja kwenye mtandao wa jamiiforum; Umakini wa uongozi ni kufanyia kazi viashiria, na siyo kusubiri mpaka watu wamekufa ndipo Rais, Waziri Mkuu na mawaziri wanajipanga kusafiri kwenda kutoa rambirambi na kuunda ‘kamati za uchunguzi’.

Huo siyo utendaji makini wa Serikali iliyo makini.

Serikali ina vyombo vingi ikiwa ni pamoja na hiyo ambayo inaitwa ‘intelijensia’. Kazi kubwa ya vyombo hivi ni kung’amua matukio yanayoweza kutokea baadaye kabla hayajatokea na kuyafanyia kazi.

Tunaposhindwa kufanya hivyo na mambo hayo yakatokea, na kisha tukakimbilia Marekani kuomba msaada wa FBI kuchunguza, maana yake ni kwamba tuna walakini kiuongozi. Hatujiwezi wenyewe kujiongoza!

Na ndiyo maana narudia kusema kuwa, tangu Mwalimu Nyerere afariki dunia, tumesahau namna ya kujitawala wenyewe, na hivyo tunapaswa kuanza upya kujifunza kujitawala wenyewe, na kuacha kukimbilia nje kuomba misaada hata kwa masuala yanayohusu usalama wetu wenyewe ambayo, nina hakika, tukiwa na dhamira ya kweli na wachapakazi hodari, tunaweza kuyamudu wenyewe!

Nihitimishe kwa kuwaambia Wakristo wenzangu kwamba kuhubiri chuki na umwagaji damu dhidi ya Uislamu ni kuupa Ukristo jina baya. Na pia niwaambie ndugu zangu Waislamu kwamba kuhubiri chuki na umwagaji damu dhidi ya Ukristo ni kuupa Uislamu jina baya.

Kazi ya kushawishi waumini kutoka dini moja kwenda nyingine ni kazi inayoweza kufanywa kwa amani kabisa, na kwa namna inayompendeza Mungu wetu sote; maana suala la imani ni suala la mtu binafsi.

Tafakari.

Na Johnson Mbwambo - Gazeti la Raia Mwema mtandaoni.

No comments: