Tuesday, September 24, 2013

Sitta aisuta CCM • Asema mafisadi wanashabikiwa kuelekea 2015 na Josephat Isango



na Josephat Isango

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema kuwa serikali imeshindwa kuwapa wananchi maisha bora, licha ya nchi kuwa na rasilimali nyingi.

Sitta ambaye pia ni spika wa zamani wa Bunge, alisema kuna dalili za wazi za watu kukata tamaa, na kwamba wako wachache wanajitajirisha, tena wengine kinyume cha katiba ya nchi na ile ya CCM inayosema ‘sitakitumia cheo kwa faida yangu’.

Sitta alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na kituo cha Star tv kwenye kipindi cha medani za kisiasa jana.

Alisema anasikitika kuona kuwa hadi sasa Watanzania wana maisha magumu.

Pamoja na kutokitaja moja kwa moja, ni wazi kuwa Sitta alikilenga Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani ndicho kinaongoza serikali aliyodai imeshindwa kuleta maisha bora yaliyoahidiwa kwa wananchi.

“Tumepoteza hadhi ya nchi yetu, ni aibu sana kusikia kuna vijana wa Kitanzania zaidi ya 600 waliopo katika magereza mbalimbali duniani kwa sababu ya suala la dawa za kulevya.

“Inaumiza tunapoelekea 2015 kwenye uchaguzi mkuu tunawashabikia viongozi walioliingiza taifa letu katika mikataba mibovu, zabuni za upendeleo na wengine bado wamewatumia vijana kama punda kubeba dawa za kulevya,” alisema.

Alisisitiza kuwa katiba mpya inayotengenezwa sasa ibane mianya hiyo.
Sitta aliongeza kuwa hali hiyo ya matabaka ya matajiri na masikini ikizoeleka, taifa linaweza kuingia katika machafuko makubwa.

Alisema hata mabilioni ya fedha zilizopelekwa mikoani kwa ajili ya kuwainua wananchi, maarufu kama ‘mabilioni ya Kikwete’ yametafunwa na wachache kwa kutumia miradi hewa.

“Tatizo hilo linaweza kumalizwa na katiba mpya. Tukiwa na katiba mpya nzuri na viongozi waadilifu, sera za nchi zitabadilika, Watanzania watapata maisha mazuri,” alisema.

Kuhusu uchaguzi mkuu ujao, alitahadharisha kuwa kuna hatari kupitia uchaguzi huo Watanzania wakapata rais aliyenunua uongozi kutokana na kusaidiwa kifedha na wafanyabiashara wasio waadilifu.

Sitta aliweka bayana kuwa uzalendo kwa viongozi nchini umeisha, na wale waliopo wanatanguliza ubinafsi tofauti na ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.

“Siku hizi baadhi ya viongozi wa siasa wanajisifia kumiliki magari ya kifahari na nyumba za kisasa wakati enzi za Mwalimu viongozi walikuwa wanaogopa hata kutaja kama wanamiliki nyumba au gari.

“Ilikuwa si jambo la kawaida watu kushabikia siasa za watu kununua wenzao, tofauti na ilivyo sasa. Watu wanazoea utamaduni wa kusifia wenye fedha nyingi ingawa wapo katika utumishi wa umma na hawasemi wamezipata wapi,” alisema.

Kuhusu suala la katiba mpya, Sitta alisema itasaidia kuwa na upeo mpana wa demokrasia, na hivyo kuwataka wananchi waondoe woga na kushiriki mchakato wake wa kuipata.

Sitta alisema upinzani nchini unaendelea kupata nguvu na kuna vyama vinafanya vizuri, lakini akashauri kuwa vingepata nguvu zaidi kama vingekuwa vichache.

“Upinzani utaimarika tukiweza kushindana katika sera na mitazamo ya wapi tunaipeleka nchi. Tumeishakwenda hatua fulani, lakini sasa inabidi hoja zitawale sio mabavu,” alisema.

Sitta aliongeza kuwa bado haoni tishio lolote la upinzani kwa kuwa hawana safu kubwa ya orodha ya viongozi wenye sifa za kugombea urais kama ilivyo kwa CCM, licha ya vyama hivyo kuwa na watu wengi kwenye mikutano yao.

Kuhusu kambi za urais ndani ya CCM, Sitta alisema zipo kwa kuwa wengine wanabebwa na wafanyabiashara, ingawa hawana nia ya kuwasaidia wanyonge.

Kuhusu kujitosa katika mchakato huo au la, alisema wakati bado na ukifika atapima wagombea ni akina nani na kama naye atatamkwa tamkwa, uwezo wa kugombea anao.


No comments: