Tuesday, October 08, 2013

Høyre (The Conservative) na Fremskrittspartiet (Progress Party) zakubaliana kuunda serikali ya mseto. Wanachukua madaraka wiki ijayo.


Waziri Mkuu mteule wa Norway, Bi. Erna Solberg (kulia) na Bi. Siv Jensen, kiongozi wa Progress Party (kushoto) jana usiku kwenye hoteli ya Sundvolden.


Waziri Mkuu mteule wa Norway, Bi. Erna Solberg wa chama cha Høyre (The Conservative) na Bi. Siv Jensen, kiongozi wa chama cha Fremskrittspartiet (Progress Party) jana usiku kwenye hoteli ya Sundvolden wametoa tamko la pamoja kuwa wamemaliza mazungumzo yao na wamekubaliana kuunda serikali ya mseto. Makubaliano hayo yako kwa Kinorwejiani: Politisk plattform for en regjeringutgått av Høyre og Fremskrittspartiet. Hii ni mara ya kwanza kwa Progress Party kuingia madarakani hapa Norway toka kilipoanzishwa mwaka 1973.

Bi. Solberg na Bi. Jensen, wamezungumzia nini watafanya wakiingia madarakani ili kuleta mabadiliko makubwa hapa Norway. Yafuatayo ni baadhi yaliyomo kwenye makubaliano hayo:
 • Umri wa mtu atakayetaka kumleta mke au mme mwenza utakuwa kuwa miaka 24 kuendelea. Kiwango cha chini cha mwaka cha kuonyesha kama mtu anaweza kumudu kumleta mwenza kitaongezwa toka kroner laki moja na nusu kwa mwaka.
 • Muda wa mtu mwenye asili ya kigeni kuomba kibali cha kudumu cha kuishi utaongezwa toka miaka 3 hadi miaka 5.
 • Kabla mtu hajakubaliwa kupewa uraia wa Kinorwejiani, lazima mwombaji afaulu mtihani wa kuzungumza Kinorwejiani na kufaulu mtihani wa uraia.
 • Sheria za uhamiaji zitakazwa kamba. Pale penye nyufa patazibwa. Watu wanaokuja kuomba hifadhi za kisiasa na watakuwa wanachujwa kama tui la nazi. Wale watakaoonekana kuwa wanapaswa kupewa hifadhi watawekwa kwenye kambi za aina yake na wale ambao wataonekana hawafai kupewa hifadhi wataweka kwenye kambi zenye ulinzi tayari kurudishwa walikotoka.
 • Uwezekano wa kumchungulia rafiki, ndugu, jamaa au jirani kuwa amepata kiasi gani cha mapato ya mwaka kwenye orodha ya kodi, sasa basi. Watakaopata nafasi hiyo ni watu na taasisi maalumu zinazoruhusiwa kumwangalia mtu hata pale anapoomba mkopo toka benki.
 • Wataruhusu maduka ya vyakula na masupa maketi kufunguliwa Jumapili. Maduka ya kawaida ya chakula na masupa maketi hayaruhusiwi kufunguliwa Jumapili hapa Norway. Yanayofunguliwa na maduka ya vyakula yasiyozidi mita za mraba 100.
 • Watahakikisha watu ambao hawana kazi na wanapokea msaada wa serikali wa kujikimu na kuweza kuishi wanafanya kitu cha kutolea jasho huo msaada pale inapobidi.
 • Wataimarisha, watakarabati na kujenga haraka njia za mawasiliano na barabara. Moja ya hatua hiyo ni kuanzisha kampuni ya taifa ya ujenzi.
 • Wataimarisha ulinzi na usalama wa raia na nchi. Watahakikisha kuwa wote wanaomaliza chuo cha polisi wanapata kazi kwenye jeshi la polisi. Tofauti na serikali iliyopita ambayo iliongeza idadi  ya wanaoingia kuchukua mafunzo ya upolisi lakini kushindwa kuwaajiri wote waliomaliza.
 • Wataruhusu polisi wa nchi hii kubeba silaha wakiwa kazini. Norway ni nchi chache zilizobaki hapa duniani ambapo polisi wanatembea bila silaha. Wanaruhusiwa kubeba silaha pale tu panapokuwa na shughuli za hatari.
 • Wadau wa elimu wataruhusiwa kuanzisha shule za binafsi na kupata ruzuku kutoka serikalini.
 • Watapunguza urasimu uliokisiri kuanzia ofisi za manispaa hadi za serikali.
 • Watapunguza idadi za manispaa 428 za Norway. Hawajaamua zitakuwa ngapi.
Nawapongeza Høyre na Fremskrittspartiet na namtakia kila la heri Waziri Mkuu Mteule, Bi.Erna Solberg na serikali yake ya mseto.


Semboja, Mwamedi Juma4

No comments: