Monday, November 25, 2013

Taarifa ya Dk. Kitila Mkumbo kwa Umma kuhusu Kuvuliwa nafasi za mamlaka ndani ya CHADEMA





1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA. Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi ujao ndani ya chama. 

2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa hoja za watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani ya chama hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa kukubali ombi langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na kueleza kuwa nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida hadi hapo chama kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote. 

3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe) tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo: 

a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama chetu.

b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini. Chama hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo. Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’. Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho nilijisababishia matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho chama kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa. 

c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa imani niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo demokrasia, na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.

d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani. Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi mkali sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda uteuzi wa kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha Democrat mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka maalumu wa siri ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne tu bila yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya Hillary Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha urais. Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi. 

e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yoyote kuuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari. 

f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua nafasi yangu moja kwa moja. 

Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa nayo. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria. 

4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa. 

5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe. 

Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za ukomunisti katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika nchi. Zilikuwa ni njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena. 

6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania. 

Mungu ibariki Tanzania. 

Dkt. Kitila Mkumbo 
Dar es Salaam 
Jumapili, 24 Novemba 2013.

No comments: