Sunday, January 12, 2014

Jumatatu 13.Januari 2014 ni siku ya mapumziko kwa Watanzania wote kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar - atangaza Rais Jakaya Kikwete



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametangaza kuwa kesho, Jumatatu, Januari 13, 2014, itakuwa ni Siku ya Mapumziko kwa Watanzania wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Rais Kikwete ameutangaza uamuzi huo mjini Zanzibar ambako leo ameungana na Watanzania na Wazanzibari wote kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na mwasisi wa Zanzibar na Taifa la Tanzania, Hayati 
Abeid Amaan Karume yalifanikiwa kuung’oa madarakani utawala dhalimu wa Sultan na 
kuwawezesha kwa mara ya kwanza katika historia Waafrika walio wengine kujitawala ndani ya nchi yao wenyewe.

Yalikuwa ni Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofungua njia ya kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – miezi mitatu baada ya Mapinduzi hayo – Aprili 26, 1964.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Ali Mohamed Shein ametangaza kuwa kesho itakuwa Siku ya Mapumziko Tanzania Visiwani kusheherekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Shein alitangaza mapumziko hayo wakati alipohutubia wananchi kwenye Uwanja wa Michezo wa Amaan mjini Zanzibar katika kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi.

No comments: