Saturday, February 15, 2014

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza amesema rushwa imelifikisha taifa mahala pabaya


Askofu Dkt. Benson Bagonza


ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza amesema rushwa imelifikisha taifa mahala pabaya.
Kutokana na hali hiyo, amewataka viongozi wa dini kukemea hilo kwa nguvu zote.
Askofu Bagonza alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu sakata la kunyimwa dhamana kwa Mchungaji Jakson Kanyiginya katika mazingira yenye harufu ya rushwa.
Mchungaji huyo ambaye juzi alipandishwa kizimbani akituhumiwa kumpiga mfanyabiashara Joseph Gareba, alinyimwa dhamana baada ya mwendesha mashitaka Meja Juma Litafa kuzikataa barua za wadhamini hadi azifanyie uhakiki na kuamuru mchungaji huyo awekwe rumande hadi Februari 26.
Hata hivyo, mchungaji huyo aliachiwa kwa dhamana juzi baada ya maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa kanisa hilo waliokuwa kwenye mafungo kukatisha mafungo yao na kuandamana hadi katika Kituo cha Polisi cha Karagwe kushinikiza apate dhamana kabla ya Februari 26.
Mbali na Bagonza, maaskofu  wengine walioshiriki kwenye maandamano hayo ni Paulo Mkuta na Nelson Kazoba ambao waliandaa tamko na kulikabidhi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa.
Askofu Bagonza alivilaumu vyombo vya dola na mahakama kwamba vimejaa rushwa, hasa baadhi ya vijana waliopata ajira hivi karibuni ambao alisema wanataka mafanikio ya haraka kupitia rushwa.
“Rushwa imetufikisha mahala pabaya sana. Wapo vijana walioajiriwa kwenye mahakama zetu wanasema wanapokea rushwa kwa sababu wanataka kurejesha mikopo waliyopewa na serikali wakati wakisoma. Leo kanisa limeandamana kwa sababu mtu wetu kaguswa, jiulize wapo wangapi wanaonewa?” alisema Askofu Bagonza.
Akizungumzia chanzo cha mzozo huo, Askofu Bagonza alisema mfanyabiashara Gareba alikuwa na kesi ya ardhi na kanisa tangu miaka 80 na mahakama iliagiza ardhi hiyo isiguswe hadi kesi itakapomalizika.
Alisema mwaka jana, mfanyabiashara huyo aliingia kwenye eneo hilo na kuanza kukata miti, lakini waumini walipoona hali hiyo walimjulisha Mchungaji Jakson ambaye aliwachukua polisi na kumkamata Gareba na kumuweka ndani.
Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, baada ya tukio hilo, mfanyabiashara huyo alienda kufungua kesi ya kupigwa kwa siri bila kanisa kujua hadi juzi Mchungaji Jakson alipoitwa polisi na kufikishwa mahakamani.
Kutoka Tanzania Daima.


No comments: