Sunday, April 13, 2014

HOTUBA YA MH. TUNDU LISSU ILIYOKATISHWA NA TBC - MAONI YA WAJUMBE WALIO WA WACHACHE KATIKA KAMATI NAMBA NNE KUHUSU SURA YA KWANZA NA SURA YA SITA YA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA



Mheshimiwa Mwenyekiti,

Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (‘Rasimu’) ndizo msingi ambao Rasimu yote imejengwa juu yao. Wakati Sura ya Kwanza inagusa suala la muundo wa Muungano katika ibara moja tu kati ya ibara tisa, Sura yote ya Sita inahusu ‘Muundo wa Jamhuri ya Muungano.’ Suala la Muungano na hasa Muundo wake limetawala mjadala wa kisiasa na kikatiba wa Tanzania kwa zaidi ya miaka thelathini. Ndio maana katika waraka wake wa siri kwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (‘CCM’), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya chama hicho imetamka kwamba “muundo wa Muungano ndiyo moyo wa Rasimu na ndiyo unaoamua ibara nyingine zikae vipi.”

Suala hili pia limetawala mchakato wa Katiba Mpya tangu ulipoanza miaka mitatu iliyopita. Kama alivyosema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Joseph Sinde Warioba wakati wa kuwasilisha Ripoti ya Tume yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar tarehe 30 Disemba, 2013: “Moja ya mambo ambayo yamejadiliwa sana na kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa ... ni Muungano wa Tanzania. Jambo kubwa limekuwa juu ya muundo wa Muungano.”...




No comments: